MakalaSiasa

Je, mabalozi hawa walikataliwa walikotumwa?

February 7th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

BAADHI ya mabalozi wapya walioteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta hawajaanza kutekeleza majukumu katika mataifa ya kigeni walikotumwa kuwakilisha Kenya, zaidi ya miezi minane baada ya kuidhinishwa na bunge.

Duru kutoka Wizara ya Mashauri ya Kigeni zinasema kuwa baadhi ya mabalozi hawajaanza kuchapa kazi baada ya kukataliwa na mataifa walikotumwa.

Baadhi ya wale walioathiriwa na hatua hiyo ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) Ndegwa Muhoro ambaye alikuwa amependekezwa kuwa balozi wa Kenya nchini Malaysia.

Bw Muhoro alipigwa msasa na kuidhinishwa na wabunge licha ya pingamizi kutoka kwa wakili Ahmednassir Abdullahi aliyemhusisha na ufisadi.

Wabunge walipuuza ushahidi ambao Bw Abdullahi aliwasilisha lakini akasema wakili huyo akaapa kuwa angeiandikia Malaysia kuitaka imkatae Bw Muhoro.

“Nimewasilisha bungeni ushahidi kuhusu sababu yangu kuhusu ni kwa nini nahisi kuwa mkuu wa zamani wa DCI, Bw Muhoro, hafai kuhudumu kama Balozi wetu nchini Malaysia. Nitawasilisha ushahidi huo huo kwa Waziri Mkuu na Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Malaysia.,” akasema.

“Na bunge ikifeli kushughulikia ushahidi wangu, nitawasilisha kesi kortini,” akasema Bw Abdullahi ambaye ni wakili mkuu.

Malaysia imeichukua msimamo mkali dhidi ya ufisadi haswa baada ya kuchaguliwa kwa Mahathir bin Mohamad kuwa Waziri Mkuu wan chi hiyo.

Johnson Kimani Ondieki, ambaye alipendekezwa kuhudumu kma Balozi wa Kenya nchini Uturuki pia hajapata idhini kutoka taifa hilo ambako alitarajiwa kufanya kazi.

Ondieki ni jenerali wa zamani katika Jeshi la Kenya (KDF) ambaye alikuwa ameteuliwa kuongoza jeshi la Umoja wa Mataifa (UN) nchini Sudan Kusini. Alifutwa kazi katika hali ya kutatanisha.

Aliyekuwa Mbunge wa Kasipul Kabondo Paddy Ahenda pia hajapata ruhusa ya kupokewa nchini Qatar huku baadhi ya mabalozi wakiwa hawajaaza kazi licha ya kupata idhini katika mataifa walikotumwa.

Hassan Wario na Richard Ekai walirejea nyumbani kutoka

Austria na Urusi, mtawalia kabla ya wao kuwasilisha stakabadhi zao za marais wa mataifa hayo.

Hii ni baada a wao kustakiwa kwa makosa yanayohusiana na ufisadi.

Sheria za Kimataifa zinahitaji Kenya, kupitia Wizara ya Mashauri ya Kigeni, kuandikia mataifa ambako wateule wametumwa kabla ya kuwasilisha majina yao.

Baadaye taifa pokezi litachunguza mtu huyo aliyeteuliwa kabla ya kuijibu serikali kupitia barua. Inaweza kukubali au kukataa mteule bila kutoa sababu zozote.