Makala

Wakenya kurudi kwa ugali ghali baada ya nchi jirani kuparamia na kuzoa mahindi kwa wingi

Na BARNABAS BII April 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KAMPUNI za kusaga unga wa mahindi zimeonya kuwa uhaba mkubwa wa mahindi katika eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa utasababisha kupanda kwa bei ya unga kwa kiasi kubwa.

Baadhi ya viwanda vya kusaga unga vimesitisha shughuli na kupunguza wafanyakazi kutokana na ukosefu wa mahindi.

Imebainika kuwa wakulima wengi waliuza mahindi yao mara baada ya mavuno kwa wafanyabiashara waliokuwa wakipeleka mazao hayo Uganda na Sudan Kusini kwa sababu ya bei nzuri.

Gunia la kilo 90 linauzwa kwa Sh4,200 katika soko la ndani, huku likiuzwa kwa Sh4,600 Uganda na Sh5,200 Sudan Kusini.

“Tunatazama janga linalonukia kwa kuwa usambazaji wa mahindi katika soko unazidi kupungua baada ya wakulima wengi kuuza mazao yao mara baada ya kuvuna. Wengine walipeleka mazao hayo Uganda na Sudan Kusini kwa sababu ya bei nzuri,” alisema Bw David Kosgei anayemiliki kampuni ya kusaga unga mjini Eldoret.

Sehemu nyingi za Uganda hazikupata mavuno kutokana na ukame mkali, hali iliyowafanya wafanyabiashara kugeukia Kenya kupata zao hilo.

“Wakulima wengi wameuza mahindi yao yote kutokana na mahitaji makubwa na bei ya juu katika maeneo ya Uganda na Sudan Kusini,” aliongeza Bw Jackson Kemboi, mtaalamu wa kilimo kutoka Kaunti ya Uasin Gishu.

Kwa kawaida, Sudan Kusini hutegemea mahindi kutoka Uganda lakini kutokana na uhaba, imeanza kununua mahindi kutoka Kenya na mataifa ya kusini mwa Afrika kama Zambia, Zimbabwe na Afrika Kusini.

“Mahitaji ya mahindi ni makubwa sana na hakuna mahindi yanayoingizwa kutoka Tanzania, Zambia, Zimbabwe wala Afrika Kusini. Kutatokea upungufu mkubwa wa mahindi utakaosababisha bei kupanda hadi watu wa kawaida wasiweze kumudu,” alisema Bw Kipng’etich Mutahi anayehudumu Eldoret.

Viwanda kadhaa vya kusaga unga Magharibi mwa Kenya vimesitisha shughuli kwa sababu ya uhaba wa mahindi. Angalau viwanda 10 vimetuma baadhi ya wafanyakazi likizoni baada ya kupunguza shughuli zao kutokana na uhaba huo.

“Tumekuwa tukifanya kazi chini ya uwezo wetu kwa wiki mbili zilizopita hali iliyotulazimu kusimamisha shughuli hadi tutakapopata mahindi ya kutosha,” alisema mmiliki mmoja wa kampuni ya kusaga unga.

“Watumiaji tayari wanateseka kutokana na bei ya juu ya unga, ambayo sasa ni zaidi ya Sh150 kutoka Sh120 kwa pakiti ya kilo mbili,” aliongeza, akisema baadhi ya viwanda vimefungwa kwa sababu mahindi mengi yanasafirishwa kwenda Uganda na Sudan Kusini ambako yanauzwa kwa bei ya juu.

Wizara ya Kilimo imekiri kuwa kuna uhaba unaokuja wa mahindi kutokana na ushindani mkubwa kati ya watengenezaji wa chakula cha mifugo na kampuni za unga.