Upeperushaji wa kipindi cha ufichuzi wa BBC kuhusu mauaji Juni 25 wapigwa breki
UPEPERUSHAJI wa kipindi cha ufichuzi wa BBC kuhusu mauaji ya waandamanaji Juni 25, 2024 umepigwa breki kufuatia shinikizo kutoka kwa maafisa wa utawala, msemaji wa shirika hilo la habari amesema.
Awali, shirika hilo lilikuwa limetangaza kwamba kipindi hicho, ambacho tayari wamekipakia kwenye mtandao wa YouTube, kilikuwa kipeperushwe kwenye runinga ambapo umma wote ungepata fursa ya kutazama.
Ujumbe kutoka kwa msemaji wa shirika hilo ulielezea kusikitishwa kwao na hatua ya kusitishwa kwa upeperushaji huo.
“Tumevunjika moyo sana kwamba hatutaweza kupeperusha kipindi hicho kwenye runinga pamoja na kuwa na mjadala na wachangiaji studioni kama ilivyokuwa imepangwa. Kwa sasa, watazamaji wanaweza kuangalia katika chaneli yetu ya YouTube,” ikasema taarifa.