Kihika, aliyerejea nchini majuzi, atakiwa aamuru masomo ya chekechea kuwa bila malipo
MASOMO katika shule 2,400 za chekechea katika kaunti ya Nakuru hayatalipiwa ikiwa Gavana Susan Kihika atatekeleza pendekezo la hoja iliyopitishwa na bunge la kaunti ya Nakuru.
Hoja hiyo iliyodhaminiwa na Diwani wa Shabab David Wathiai ilipitishwa kwa kauli moja na madiwani wote wiki jana.
Madiwani hao walisema wanataka kuhakikisha watoto wote wanapata elimu ya msingi.
Wazazi wamekuwa wakilipa karo ya kati ya Sh200 na Sh3,500 kila muhula kama karo kwa watoto wao wanaosomea katika shule za chekechea.
“Masomo ya chekechea ni muhimu katika ukuaji wa binadamu. Hii ndio maana tunataka kuondoa ada zote zinazotozwa wanafunzi. Hatua hii inalandana na hitaji la Katiba kwamba elimu ya msingi itolewe kwa watoto wote bila malipo,” akaeleza Bw Wathiai.
Endapo Gavana Kihika ataidhinisha uamuzi huo wa Bunge la Kaunti ya Nakuru, serikali yake itatenga pesa za kufanikisha utekelezaji wa sera hiyo.
“Tumepitisha mswada huo na sasa tunataka Gavana Susan Kihika atekeleze pendekezo lake kwamba shule zote za chekechea zitoe elimu bila malipo. Bunge la Kaunti linaweza pia kutenga fedha za kufanikisha utekelezaji wa pendekezo hilo hatua ambayo itafanyika kila mwaka,” Bw Wathiai akasema.
Diwani wa London Benard Gatuso alisema hoja kama hiyo ilikuwa inahitajika kupitishwa mapema na bunge hilo.
“Karo inayolipwa katika shule za chekechea zinazoweza kuonekana kama kidogo, lakini ni mzigo mkubwa kwa wazazi wakati huu ambapo uchumi umezorota. Kwa kupitisha hoja hii, tumewawezesha watoto wetu kupata elimu ya msingi kwa urahisi,” akasema Bw Gatuso.