Habari za Kitaifa

Mtangazaji nyota Edward Kwach aaga dunia

Na BENSON MATHEKA April 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MTANGAZAJI maarufu wa redio, Edward Kwach, amefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mfupi, hali iliyomfanya alazwe hospitalini jijini Nairobi wiki mbili zilizopita, familia yake imetangaza.

Kifo cha Kwach aliyekuwanmtangazaji wa redio ya Spice FM, kilithibitishwa na msemaji wa familia, Michael Okwiri, ambaye alieleza kuwa marehemu alifariki usiku wa Aprili 28, 2025, akiwa na umri wa miaka 44.

“Kwa huzuni kubwa, tunatangaza kifo cha mpendwa wetu mwana na kaka yetu, Carey, aliyefariki usiku wa kuamkia Aprili 28, 2025, akipokea matibabu ya homa ya uti wa mgongo (meningitis),” alitangaza Okwiri.

“Kifo chake ni pigo kubwa kwa wote waliomfahamu binafsi na kwa wengine wengi waliomuunga kupitia kazi yake,” aliongeza.

Kwach alifariki dunia akipokea matibabu baada ya kugunduliwa kuwa na meningitis, ambayo ni uvimbe wa utando wa kinga unaozunguka ubongo na uti wa mgongo.

Okwiri alimtaja marehemu kama mtu atakayekumbukwa si tu kwa upole na uchangamfu wake, bali pia kwa  kupenda  muziki.

Okwiri alisema kwamba Kwach aligusa maisha ya wengi kupitia sauti  akitangaza na kuwa rafiki wa karibu na wa kuaminika kwa wasikilizaji kote nchini.

Kwach alikuwa akipokea matibabu kwa kipindi cha wiki mbili zilizopita na hivi majuzi aliomba msaada wa damu, ambapo Wakenya walijitokeza kwa wingi kumsaidia.

Kabla ya kifo chake, Kwach alikuwa mtangazaji wa kipindi cha Spice Drive katika redio ya Spice FM. Kipindi hicho kilirushwa hewani kila siku ya wiki kuanzia saa tisa alasiri hadi saa moja jioni.

Ucheshi wake wa kipekee  na uchezaji wa muziki  akiwa studio vilivutia watu wengi, na kumpatia heshima miongoni mwa wasikilizaji wake.

Kwach pia aliwahi kufanya kazi katika redio za Urban Radio na Capital FM.