Habari za Kitaifa

Wakenya wasimulia Seneti kwa majuto kuhadaiwa na serikali yao kuhusu ajira za ng’ambo

Na COLLINS OMULO April 30th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAKENYA wamelia kwa majuto wakielezea maumivu yao mbele ya Kamati ya Seneti, baada ya kudanganywa kwa ahadi za ajira katika nchi za kigeni na serikali yao.

Simulizi hizi za mateso, zilizojaa machozi, zilishangaza maseneta, huku waathiriwa wakielezea kwa uchungu jinsi walivyoarifiwa kuhusu ajira Mashariki ya Kati na kulazimishwa kulipa fedha, lakini walibaini ahadi hizo zilikuwa hewa tupu.

Bila kujali umri wala jinsia, waathiriwa walikusanyika mbele ya kamati ya Seneti kuhusu Leba wakielezea jinsi walivyolipa kati ya Sh15,000 na Sh55,000 kwa matumaini ya kupata ajira nzuri nje ya nchi.

Walikiri kuwa ajira hizo zilikuwa hewa tupu, kwani hakuna nafasi zilizotokea wala kurejeshewa fedha zao.

Moja ya hadithi hizo za kusikitisha ni ya Bw Godfrey Githae, kutoka Nyeri, ambaye alielezea kwa uchungu jinsi alivyokopa Sh55,000 kutoka kwa mkewe na familia ya mke wake kwa matumaini ya kupata ajira ng’ambo.

Alilipa Sh15,000 kwa vipimo vya afya na Sh40,000 kwa stakabadhi za usafiri, lakini ndoto yake ya kufika Iraq ili kubadilisha maisha ya familia yake ilitibuka.

“Nilijua kuwa kazi hii ingeweza kubadilisha maisha ya familia yangu. Lakini leo hii, hakuna ajira na biashara yangu nyumbani imeporomoka. Ilikuwa ni hewa tupu,” alisema Bw Githae huku akilengwalengwa na machozi.

Maelezo ya waathiriwa yalijenga picha halisi ya janga kubwa linalowakumba Wakenya wengi wanaotafuta ajira ng’ambo.

Hii ni sehemu ya mpango wa serikali wa kuunda ajira milioni moja kila mwaka kupitia Wizara ya Leba na Ulinzi wa Jamii, lakini ahadi hizi zimegeuka kuwa mtego wa udanganyifu.

Wakiwa mbele ya kamati ya Seneti, waathiriwa walielezea jinsi walivyohudhuria mikutano mbalimbali ambapo walidanganywa kuwa ajira hizo zilikuwa za bwerere, lakini walijikuta wakitakiwa kulipa fedha taslimu badala ya kutumia huduma za malipo za kidijitali.

Walijua kuwa walikuwa wanajiandaa kwa kazi walizonuia kujijenga, lakini kwa miezi kadhaa sasa, hakuna majibu wala kazi.

Bi Doreen Biyaki, alielezea jinsi walivyoshawishika kwenda kuhudhuria vikao vya maelezo vya serikali, kwa matumaini ya kupata ajira nzuri nchi za kigeni, lakini walipoenda KICC walitakiwa kulipa Sh15,000 kwa vipimo vya afya, kinyume na ahadi walizopewa.

Walilazimika kutoa fedha taslimu.

“Tulijua kuwa ajira hizi za kigeni zingeweza kubadilisha maisha yetu. Lakini leo hii, tunashangaa ajira hizo zilikuwa wapi, kwa kuwa hatujapata majibu yoyote,” alisema Bi Biyaki.

Waathiriwa hawa walielezea jinsi walivyokuwa na matumaini makubwa lakini walijikuta wakikosa usaidizi kutoka kwa serikali.

Serikali ilikusudia kuanzisha mpango huu ili kupambana na kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira nchini, ambapo idadi ya watu wasio na ajira sasa inazidi milioni tano.

Hata hivyo, malalamishi ya waathiriwa hawa yanaonyesha kuwa kuna pengo kubwa katika utekelezaji wa mpango huo.

Ingawa Wizara ya Leba na Ulinzi wa Jamii imetenga fedha na kuanzisha mikakati mbalimbali, waathiriwa wanadai kuwa hawajapata msaada wowote wala kazi walizoahidiwa.

Kamati ya Seneti sasa inataka kufahamu kwa undani kuhusu hali ya ajira hizo na inatarajia kumuita Waziri wa Leba, Dkt Alfred Mutua, ili kutoa maelezo zaidi.

Seneta Seki Lenku wa Kajiado, alisisitiza kuwa waathiriwa wanastahili kupata haki zao na waziri lazima ajibu kwa kushindwa kutimiza ahadi.