Akili MaliMakala

Wazamia teknolojia kuongeza mazao mabichi thamani

Na SAMMY WAWERU April 30th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

HISTORIA ya waliochangia kukuza sekta ya uzalishaji matunda nchini ikiandikwa, Peter Wambugu, ambaye ni mwasisi wa Shamba la Wambugu Apples bila shaka hatakosa kujumuishwa.

Wambugu, alitafiti na kuzindua tufaha maalum inayojulikana kama Wambugu Apple miaka 40 iliyopita.

Matufaha yake yakiwa yanakuzwa na zaidi ya wakulima 2,500 Kenya na kupenya nchi 36 Barani Afrika na Asia, matunda yake yameidhinishwa na Taasisi ya Mbegu na Ustawishaji wa Mimea Nchini (Kephis).

Matufaha yanayolimwa na Peter Wambugu. Picha|Sammy Waweru

Mapema mwaka huu, 2025, chini ya mojawapo ya matawi mashirika yake, alizindua kiwanda cha kukausha matunda yanayojumuisha matufaha, ndizi, joka (dragon fruits), stroberi na maembe.

Kilele chake majuzi kimekuwa kupanua huduma, na kuanzisha ugandishaji wa matunda hayo (freeze-dried fruits).

Ni shughuli ya uongezaji thamani mazao mabichi ya shambani inayosifiwa kuongeza muda wa kuyadumisha.

“Kwa kawaida, mazao mabichi kama vile matunda na mboga hudumu siku saba pekee yanapovunwa. Yakikaushwa na kugandishwa, muda wake unarefushwa kwa mwaka mmoja,” anasema Mathew Njenga, Mkurugenzi Mkuu Wambugu Apples.

Mathew Njenga, Mkurugenzi Mkuu Wambugu Apples na Kate Wambugu wakionyesha bidhaa zilizokaushwa na kugandishwa. Picha|Sammy Waweru

Shughuli za kugandisha mseto huo wa matunda, zinaendeshwa kupitia Afriavo Orchard Limited, kampuni ambayo pia huyakausha kwa kutumia sola.

Njenga, kwenye mahojiano wakati wa uzinduzi rasmi wa matunda yaliyogandishwa mnamo wikendi, alifichua kwamba wanatumia teknolojia ya sublimation.

Pia, ikijulikana kwa Kiingereza kama Lyzophilization, ni mfumo wa kukausha matunda na kuyagandisha kwa kuhifadhi virutubisho vyake, harufu nzuri na maumbo yake (shape).

“Lengo letu, awali, lilikuwa kuongeza thamani matufaha, ila baadaye tukagundua mwanya mwingine wa matunda ya joka, ndizi, stroberi na maembe,” Njenga akaelezea, akidokeza kwamba kwa sasa wanalenga masoko ya ndani kwa ndani.

Matufaha na maembe yaliyokaushwa na kugandishwa na Afriavo Orchard Limited. Picha|Sammy Waweru

Wambugu Apple, huuza nje ya nchi matufaha na miche yake.

Njenga anasikitika kwamba wakulima wengi nchini wanalenga mazao yao kuuzwa ng’ambo, badala ya kuboresha soko la ndani kwa ndani.

Anaamini uongezaji mazao thamani, ndio chanzo cha kuhamasisha ulaji wa ndani kwa ndani.

“Oda tunazopata ni tele. Kinachotushika mikono ni kukosa wakulima wa kutusambazia mazao,” akasema Njenga, ambaye pia ni Mwenyeketi wa Muungano wa Wakuzaji Matufaha Kenya na Uuzaji Nje ya Nchi (KAGEA).

Kutosheleza mahitaji ya soko, anasema wanahitaji kuwekeza kwenye mashine na mitambo ya zaidi ya Sh100 milioni.

Ndizi zilizoiva, tayari kukaushwa na kugandishwa. Picha|Sammy Waweru

Mashine wanazotumia kukausha na kugandisha matunda, zimewagharimu kima cha Sh48 milioni.

Kulingana na Kate Wambugu, bintiye Wambugu, ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu na Balozi wa matufaha yake, hawalengi kukoma kwa aina tano pekee ya matunda wanayoongeza thamani.

“Aina mbili zingine za matunda zi njiani zaja,” Kate akaambia Akilimali.

Kulingana na Mamlaka ya Mseto wa Mimea Inayochukua Muda mfupi Kukomaa (HCD), Kenya inauza ng’ambo asilimia tano pekee ya mazao hayo, asilimia moja pekee ikiwa ni bidhaa zilizosindikwa.

Hii inaashiria kuwa ulaji wa ndani kwa ndani ni asilimia 95, data hiyo ikionyesha mwanya uliopo kwa wakulima hasa kuwahi masoko ya ng’ambo.

“Maua yanawakilisha asilimia 50, matunda asilimia 30 na mboga asilimia 20,” anasema Christine Chesaro, Mkurugenzi Mkuu HCD.

Ndizi (katikati) zilizokaushwa, zikagandishwa na kupakiwa. Picha|Sammy Waweru

Taasisi hiyo hudhibiti sekta ya mimea inayochukua muda mfupi kukua na kukomaa.

Kulingana na Afisa Christine, mwaka uliopita, 2024, thamani ya matunda yaliyouzwa masoko ya ng’ambo ilikuwa Sh32 bilioni, Sh23 bilioni zikiwakilisha avokado, na Sh9 bilioni maembe.

“Tunahimiza wakulima na wadauhusika kukumbatia uongezaji thamani mazao ya kilimo, ni mtandao unaoteka soko la haraka,” Christine anasema.

Kenya, hupoteza kati ya asilimia 30 hadi 40 ya mazao shambani na baada ya mavuno, kwa sababu ya ukosefu wa miundomsingi dhabiti.

Uongezaji thamani unatajwa kwamba utasaidia kuziba mwanya huo.

Afriavo Orchard Limited, chini ya mwavuli wa Wambugu Apples, inaendeshea huduma zake eneo la Ruiru, Kiambu.

Matufaha yaliyoongezwa thamani na Afriavo Orchard Limited, kampuni inayohudumu chini ya Wambugu Apples. Picha|Sammy Waweru