Habari za Kitaifa

Dakika za mwisho za Mbunge Charles Were kabla ya kuuawa

Na STEVE OTIENO May 1st, 2025 Kusoma ni dakika: 3

MBUNGE wa Kasipul, Charles Ong’ondo Were, ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi Jumatano usiku, alikuwa akilalamika hadharani kuwa maisha yake yalikuwa hatarini.

Aliweka wazi kwa umma na polisi kuwa alikuwa akiishi kwa hofu, akisema mara kadhaa kwamba  alikuwa “mtu aliyelengwa kuuawa”.

Miezi miwili kabla ya mauaji hayo,  Februari 8, Mbunge huyo aliyepigwa risasi karibu na Nairobi Funeral Home katika barabara ya Ngong kabla ya saa mbili usiku, alieleza matukio mawili yaliyoonyesha mtu aliyekuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu maisha yake.

Siku hiyo, Were alikemea ongezeko la visa vya ghasia katika eneo bunge lake, akidai kuwa vilikuwa vikitekelezwa na watu kutoka nje.

Kwa mujibu wa Mbunge huyo, watu wasiokuwa wakazi wa eneo hilo walikuwa wakivuruga mikutano yake ya hadhara.
Alitaja tukio lililotokea wiki moja kabla huko Nyatindo, Wadi ya East Kamagak, wakati wa mazishi ambapo alikumbana na kundi la wahuni.
“Mara tu nilipowasili pale, mmoja wa wahalifu maarufu kutoka Kachien, anayeitwa Aboy, alisema kuwa sitazungumza hapo. Wanakijiji walikasirika sana, na jambo hilo liko mikononi mwa wapelelezi,” alisema.

Siku moja kabla ya tukio hilo, Were alieleza kuwa gari lake lilizuiwa alipokuwa akiondoka kwenye mazishi mengine, na kuongeza kuwa kama hangekuwa na walinzi wake, angevamiwa.

Katika video inayosambazwa mitandaoni, Mbunge huyo alidai kuwa kulikuwa na kundi lililoandaliwa kumuua.

“Kuna MCA wa zamani na mtu aitwaye Ongaki. MCA alisema wanangoja mkutano wa hadhara nitakaohudhuria walete polisi kutoka nje ya Kasipul na vijana kutoka Kisumu ili wachochee fujo ili niuawe humo,” alisema huku watu waliomsikiliza wakishtuka na kulaani vikali njama hiyo.

Kwa masikitiko makubwa, hofu yake ilitimia. Muuaji aliyekuwa abiria kwenye pikipiki inayodhaniwa kumfuatilia kutoka Bunge Jumatano usiku, alimpiga risasi na kumuua papo hapo.

Baada ya kuwasili katika Hospitali ya Nairobi, Mbunge wa Rangwe, Lilian Gogo, ambaye pia ni shemeji yake Were, alidai kuwa muuaji anajulikana.

“Shemeji yangu alikuwa Mbunge shupavu ambaye hakuwa akikosa vikao vya Bunge. Aliripoti kuwa maisha yake yalikuwa hatarini. Nasema haya nikiwaangalia kwenye kamera, muuaji anajulikana. Kuna ghasia zinazidi katika siasa za Homa Bay na hali hii lazima idhibitiwe na idara za usalama,” alisema Bi Gogo.

Kwa Were, siku yake ya mwisho ilikuwa ya kawaida kwa Mbunge aliyekuwa na vikao na mikutano mingi Bungeni.
Kwa mujibu wa Mbunge wa Kabondo Kasipul, Bi Eva Obara, alitumia alasiri yote na Were, ambaye alikuwa mwenye furaha siku hiyo.

“Tulikunywa chai pamoja na kuzungumza kuhusu mambo mbalimbali. Nilimuaga saa moja jioni akiwa anaelekea nyumbani. Baadaye nilipigiwa simu na dereva wangu aliyewasiliana na dereva wa Were kuniambia kuwa rafiki yangu amepigwa risasi na kuuawa. Nimeshtuka sana, sina maneno,” alisema.

Kauli yake ilithibitishwa na Mwakilishi wa Wanawake Kaunti ya Homa Bay, Bi Joyce Atieno Bensuda, ambaye alisema alimuona Were akiwa na wenzake wabunge Jumatano jioni.

“Alikuwa akizungumza na wabunge wengine. Alikuwa akihutubia wenzake waliokuwa wakimsikiliza,” alisema.

Kiongozi wa Wachache Bungeni, Junet Mohamed, alisema kuwa Were aliondoka Bungeni dakika 30 kabla ya kuuawa.

“Alikuwa Bungeni mchana kutwa. Nataka polisi wachunguze suala hili kwa kina. Natoa rambirambi zangu na za chama (ODM) kwa familia ya Were. Kiongozi wetu wa chama (Raila Odinga) pia alikuwa hapa na ameondoka,” alisema.

Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula, alitaja mauaji hayo kama “kitendo cha uoga kilichofanyika usiku.”

“Mauaji haya yametupokonya Mbunge mahiri, mtetezi jasiri wa watu wake, na mtu aliyejitolea kwa demokrasia na huduma kwa wananchi. Hili ni pigo si kwa familia yake tu bali pia kwa taifa zima,” alisema.

Gavana wa Homa Bay, Gladys Wanga, alisema kifo cha Were ni “pigo kubwa kwa watu wa Homa Bay hasa Kasipul.”

“Tumepoteza mwana wetu mahiri, baba na mume,” alisema.

Hata hivyo, Were hakuwa mtu asiye na utata. Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na visa vya ghasia, majeraha makubwa na hata watu kutoweka katika eneo lake, hali iliyowafanya baadhi ya wakazi wa Kasipul kumshutumu kwa kuhusika.

Polisi, katika taarifa waliyotoa usiku wa manane, wametaja kifo cha Were kuwa “cha kulengwa mahsusi na kilichopangwa kabla.”

“Katika hatua hii, bado ni mapema kutoa maelezo zaidi. Maafisa wakuu wa polisi na wapelelezi wanachunguza kwa kina mazingira ya kifo hicho. Huduma ya Polisi ya Kitaifa inalaani vikali uhalifu huu wa kikatili na usio na maana, na haitasita kufanya kila juhudi katika uchunguzi wa tukio hili,” ilisema taarifa hiyo.

Mwili wa Were ulihamishwa hadi Lee Funeral Home Jumatano usiku.