Matiang’i: Azma yangu ya kung’oa Ruto 2027 imetokana na vilio vya Wakenya
ALIYEKUWA Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i amesema yuko tayari kumkabili Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Waziri huyo aliyehudumu chini ya serikali ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, alitangaza azma yake ya kutaka kuingia ikulu, imechochewa na vilio kutoka kwa Wakenya wengi ambao alisema wanalia kutokana na utawala mbaya wa serikali iliyoko mamlakani.
Waziri huyo alisema hayo jana alipozuru ngome yake ya Gusii kwa mara ya kwanza kabisa tangu arejee nchini kutoka Amerika.
“Mnajua mimi ni mchapakazi na mlijionea nilipokuwa waziri. Muda wangu ulipokwisha, nilikwenda kufanya kazi nyingine kwa kuwa watu wengine walipata nafasi hiyo.”

“Lakini nilipokuwa uko nje, nilipokea jumbe nyingi kutoka kwa Wakenya wa kila matabaka wakiniambia kuhusu utawala mbaya ulioko nchini. Waliniomba nirudi nyumbani na ikiwa niko tayari. Sasa nawahakikishia, niko tayari kwa kazi hiyo,” Waziri huyo wa zamani aliambia umati mkubwa wa watu uliomkaribisha ugani Gusii.
Dkt Matiang’i aliongeza, “nitarudi kwa watu walionipa kazi hiyo ya Ughaibuni. Nitawaandikia barua nzuri ya kuwaeleza ni kwa nini najiuzulu na nirudi huku kwa kampeni.”
Waziri huyo aliwataka Wakenya wasife moyo licha ya masaibu yanayowakumba kwa sasa na kuongeza kuwa watakaposhikana na viongozi wengine wenye maono sawa na yake, watalikomboa taifa hili kutoka kwa minyororo ya uongozi mbaya.
Dkt Matiang’i alikaribishwa kishujaa katika ngome yake na halaiki kubwa ya watu waliojitokeza kando kando ya barabara kumshangilia
“Watu wangu, ninawapenda sana. Lakini ule upendo ambao mmenionyesha leo, sijawahi kuuona katika maisha yangu. Mungu awazidishie,” Dkt Matiang’i aliongeza.

Biashara nyingi zilitatizika eneo la Gusii wakati msafara mkubwa wa waziri huyo wa zamani ulikuwa ukizunguka eneo hilo.
Baadhi ya akina mama, wazee na vijana walisimama barabarani wakimpungia mkono na kucheza kwa furaha.
Katika ziara hiyo, Dkt Matiang’i alisindikizwa na magavana Simba Arati (Kisii) na Amos Nyaribo (Nyamira).
Wabunge Joash Nyamoko (Mugirango Kusini), Clive Gisairo (Kitutu Masaba), Obadiah Barongo (Bomachoge Borabu), Anthony Kibagendi (Kitutu Chache Kusini) na Patrick Osero (Borabu) pia walikuwepo.
Seneta wa Kisii Richard Onyonka, mwenzake wa Nyamira Okong’o Omogeni na seneta mteule Gloria Orwoba pia hawakuachwa nyuma.
Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni pia aliandamana na Dkt Matiang’i katika sherehe ya kwanza katika ngome yake.
Seneta Onyonka, ambaye amekuwa akimvumisha Dkt Matiang’i kabla ya urejeo wake, alitumia fursa hiyo kuwaeleza watu wa Gusii kujiandikisha kwa wingi kama wapiga kura zoezi hilo litakapong’oa nanga.
‘Tunataka kutoa ujumbe kwa taifa zima kuwa pia sisi tunamtuma mwana wetu kukitafuta kiti cha urais. Tunamwambia azunguke kote nchini kuzungumza na viongozi wenza ili waunde kikosi imara kitakachomng’oa Ruto mamkakani,’ Seneta Onyonka alisema.
Baadhi ya vijana walisikika wakiimba nyimbo za ‘Ruto Must Go’ kila mara viongozi walipokuwa wakihutubu.

Gavana Simba Arati alisema ujio wa Dkt Matiang’i ni mwamko mpya katika siasa za Gusii.
Mbunge huyo wa zamani wa Dagoretti Kaskazini alisema ujio wa Dkt Matiang’i umejiri wakati unaofaa, wakati ambapo jamii inahitaji mtu wa kuiunganisha jinsi ilivyokuwa enzi za aliyekuwa kigogo wa siasa za Gusii marehemu Simeon Nyachae.
Gavana Arati alidai jamii ya Abagusii imekuwa ikitengwa mno katika uteuzi serikalini na kumtuma mmoja wao kuwania urais kutaifanya jamii kuheshimiwa.
Wabunge Gisairo, Kibagendi, Nyamoko, Barongo na Osero, waliweka todauti zao za vyama kando na wote kwa kauli moja wakasema ni wakati sasa kwa jamii ya Abagusii kuungana chini ya mtu mmoja.
Wabunge hao walitoa onyo kwa wenzao wanaopinga azma ya Dkt Ruto kuwa wataadhibiwa debeni na wapiga kura jinsi ilivyokuwa mwaka 2002 wakati marehemu Nyachae aliulizia urais.
“Hapa ndipo aliko Mkisii. Yule atakayekwenda kinyume na jamii, shauri yake,” Bw Kibagendi alisema.
Kabla ya kuzuru Gusii, Dkt Matiang’i mnamo Jumanne wiki hii alikutana na viongozi wengine wa upinzani kupanga mikakati kuhusu umoja wao.
Mkutano huo uliwakutanisha waziri huyo wa zamani, kiongozi wa chama cha People’s Liberation Party (PLP) Martha Karua, kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, kiongozi wa Democratic Action Party of Kenya (DAP-K) Eugene Wamalwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua
Pia katika mkutano huo, alikuwepo mwanasiasa Dkt Mukhisa Kituyi na mawaziri wawili waliofutwa katika serikali ya rais Ruto Mithika Linturi na Justine Muturi.
Katika ziara yake ya jana, Dkt Matiang’i alizuru kaunti zote za Gusii. Alianzia Kijauri, akaenda Keroka, Keumbu, Kisii Mjini, Kemera, Nyamira mjini, Ikonge na kumalizia chepilat.