Watayarishaji filamu waliokamatwa kwa kuhusishwa na kipindi cha BBC waachiliwa huru
VIJANA wanne watayarishaji wa filamu wa Kenya, waliokamatwa kwa kuhusishwa na makala ya uchunguzi ya Blood Parliament ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) wameachiliwa huru baada ya kulala seli katika vituo tofauti vya polisi jijini Nairobi.
Haya yamejiri huku BBC ikieleza Jumamosi kwamba watayarishi hao hawakuhusika kwa vyovyote na utayarishaji wa makala hiyo.
Tumefahamishwa kuhusu kukamatwa kwa wanahabari wanne nchini Kenya. Ili kuwa wazi, hawakuhusika kwa njia yoyote katika utayarishaji wa makala ya BBC Africa Eye: Blood Parliament – Afisi ya habari ya BBC katika taarifa
Wanne hao walikamatwa Ijumaa usiku, siku chache baada ya makala hayo kufichua mauaji ya waandamanaji waliokuwa na amani wakati wa maandamano ya kupinga mswada wa ushuru Juni 2024, ambapo baadhi ya watu walivamia majengo ya Bunge.
Makala hayo yaliwataja maafisa kadhaa wa usalama wanaodaiwa kuhusika moja kwa moja katika kuwaua waandamanaji wasiokuwa na silaha.
Kwa mujibu wa wakili wao Ian Mutiso, watayarishi hao — Nicholas Gichuki na Brian Adagala — walizuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Pangani, huku Mark Denver Karubiu na Chris Wamae wakizuiliwa Muthaiga.
Wanne hao waliachiliwa Jumamosi, Mei 3, dakika chache baada ya saa nne asubuhi, kufuatia kilio cha umma kuhusu kukamatwa kwao.
Mutiso alisema atachukua hatua za kisheria dhidi ya polisi kwa kuwakamata wateja wake na kwa kuchukua vifaa vyao vya kazi bila kibali cha mahakama.
“Polisi wanajua kwamba ili wachukue vifaa kama hivyo, wanatakiwa kuomba idhini ya mahakama na kuwapa wateja wangu fursa ya kuwa na wakili wao. Ikiwa watajaribu kutumia vifaa au taarifa walizopata kwa njia yoyote isiyo halali, tutaziondoa mara moja kutoka rekodi za ushahidi,” alisema.
Nicholas aliwashukuru Wakenya kwa kuwaunga mkono.
“Tunawashukuru wote waliotuma jumbe kuhusu kukamatwa kwetu kupitia mitandao yote ya kijamii,” alisema.
Jumatatu, maafisa wa Kenya walizima makala hiyo kupeperushwa, jambo ambalo wengi wachukulia kama jaribio la kukandamiza uchunguzi huo na kuzuia uchunguzi zaidi. BBC ilithibitisha kuwa ilizimwa dakika za mwisho na serikali kuonyesha makala hayo.
Mnamo Ijumaa, Mwenyekiti wa Chama cha Wataalamu wa Filamu na Televisheni Kenya (KFTPA), Ezekiel Onyango, alithibitisha kukamatwa kwa watayarishi hao wanne na kueleza wasiwasi mkubwa kuhusu tukio hilo.
“Ninaweza kuthibitisha kuwa wako chini ya ulinzi wa polisi. Nimewatembelea binafsi Pangani ambako Nicholas na Brian wanazuiliwa, na Muthaiga ambako Mark na Christopher wanazuiliwa” alisema.
Onyango alisema hatua hiyo ni tisho kwa uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari kama inavyolindwa na Katiba. Chama hicho kilisisitiza kuwa jukumu lake ni kutetea haki na maslahi ya watayarishi wa filamu na kuitaka serikali kuheshimu haki za kikatiba.
Chama hicho kilisema kuwa watayarishi hao walikabiliwa na mashitaka ya kuchapisha taarifa za uongo na unyanyasaji kupitia mtandao madai ambayo yameibua hofu kuhusu matumizi mabaya ya sheria ili kuzuia uhuru wa kujieleza.
“Tumeambiwa kuwa wanakabiliwa na mashtaka hayo. Tunaitaka serikali kutoa maelezo kamili kuhusu mashitaka hayo, ushahidi uliopo na hali ya kuzuiliwa kwao,” alisema.
Kukamatwa kwao kulichochea hasira mitandaoni, huku raia na wanaharakati wakitumia alama ya reli #FreeTheFilmmakers kuwatetea na kulaani kile walichotaja kama shambulizi dhidi ya uhuru wa ubunifu.