Habari za Kitaifa

Majangili waua polisi wa akiba karibu na mkutano wa Murkomen

Na FLORA KOECH May 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

POLISI mmoja wa akiba (NPR) aliuawa kwa kupigwa risasi, huku watu wengine wanne wakijeruhiwa vibaya katika shambulio jipya la majangili katika kijiji cha Chemoe, eneo la Baringo Kaskazini.

Tukio hilo lilitokea saa nane mchana hatua chache kutoka eneo ambalo waziri wa masuala ya ndani Kipchumba Murkomen alikuwa na mkutano wa usalama

Watu wasiojulikana waliokuwa na silaha walivamia kijiji hicho na kuwashambulia wachungaji kabla ya kuondoka na idadi isiyojulikana ya mifugo inayodaiwa kumilikiwa na Ezekiel Kaptum.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Baringo Kaskazini, Mohammed Abdi, polisi wa akiba, Evans Kamworor, aliuawa kwa risasi wakati wa shambulio hilo.

“Majangili wanaoshukiwa kutoka jamii jirani walivamia kijiji cha Chemoe majira ya saa nane mchana na wakaondoka na mifugo ya mkazi mmoja. Polisi wa akiba aliyekuwa miongoni mwa waliokabiliana nao aliuwa, huku wengine wanne wakijeruhiwa. Vikosi vya pamoja vya usalama vinaendelea kuwafuatilia wavamizi hao,” alisema Bw Abdi.

Kifo hicho kinafikisha watu 16 waliouawa katika Bonde la Kerio tangu mwanzo wa mwaka huu, huku wengine wengi wakiuguza majeraha ya risasi.

Tukio hilo lilitokea umbali wa kilomita chache kutoka Kampi Samaki, ambapo Waziri Murkomen alikuwa akifanya kikao cha usalama na makamanda wa usalama wa kaunti na maafisa wa utawala kutoka eneo hilo.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Eliud Lagat, mwenzake Gilbert Masengeli, Kamishna wa eneo la Bonde la Ufa Hassan Abdi, Kamanda wa Polisi wa eneo hilo Jasper Ombati, na maafisa wengine wa usalama wa kaunti ya Baringo.

Baada ya shambulio hilo, viongozi wa eneo hilo pamoja na wakazi walikosoa vikali idara za usalama kwa kushindwa kuimarisha ulinzi katika maeneo yanayokumbwa na mashambulio ya mara kwa mara, wakidai kuwa polisi wa akiba walikuwa wameitwa Bartabwa huku maafisa

“Ni huzuni kubwa kuona kuwa wakazi wa kijiji cha Chemoe walitelekezwa na kuachwa mikononi mwa wahalifu wenye silaha. Wakati mashambulio hayo yalipotokea, NPR wote walikuwa wameitwa Bartabwa kupigwa msasa, na maafisa wengine wa usalama walikuwa kwenye kikao cha waziri,” alisema Mbunge wa Baringo Kaskazini Joseph Makilap.

Mbunge huyo alituhumu serikali kwa kutokuwa na msimamo mkali dhidi ya wahalifu hao wanaoleta uharibifu mkubwa vijijini.

“Waziri wa Usalama anadai wakazi wanamiliki bunduki haramu. Kwa nini hazijatwaliwa? Kwa nini hajawakamata wahalifu waliowaua wananchi? Hii inaonyesha ameshindwa kukabiliana na hali ya usalama inayodorora,” alisema.