Habari za Kitaifa

ODM yatishia kuvunja mkataba na Serikali mauaji ya Were yasipotatuliwa upesi

Na GEORGE ODIWUOR   May 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

CHAMA cha ODM kimetishia kuvunja Mkataba wa Makubaliano ambao Rais William Ruto alitia saini na kinara wa Upinzani Raila Odinga iwapo mauaji ya Mbunge wa Kasipul Charles Ong’ondo Were hayatatatuliwa.

Baadhi ya wanachama anasema usuluhishaji wa mauaji tatanishi ni mojawapo ya vipengele kwenye mkataba huo uliotiwa saini mwezi Machi ambao malengo yake ni kuendeleza taifa kwa umoja na haki.

Mwenyekiti wa kitaifa wa chama hicho Gladys Wanga anasema upinzani ulikuwa umekubaliana kufanya kazi na serikali ila haikumaanisha kwamba wanachama wake wahangaike.

“Hatukutia saini mkataba wa kuruhusu mauaji ya wanachama wetu,” akasema.

Bi Wanga alisema ODM inataka suala hilo lichunguzwe kwa kina na kwamba Wakenya wanastahili kujua wauaji wa mbunge huyo.

Alisema sharti wauaji na waliopanga watupwe jela.

Kulingana na Gavana huyo wa Homa Bay, mauaji ya Were yaweza kuwa njama ya kudhoofisha ODM na viongozi wake.

“Unaweza kuona simba amenyeshewa ukadhani ni paka,” alisema akimaanisha kwamba hawatanyamazishwa.

Alisema mmoja wa waliokuwa wanalengwa ni kinara wao Raila Odinga.

“Nataka kusisitiza kwamba hii ni ngome ya ODM na hatutakubali watu wengine kuwatishia.

Alilinganisha mauaji hayo na boma ambapo maafisa wa usalama wanavamiwa kabla mwenye nyumba kufikiwa.

“Alikuwa mmoja wa watu wangu wa mkono. Kuuawa kwake kunaweza kuaminisha wahusika kwamba watanififisha mimi. Lakini hawatafaulu,” akasema.

Bi Wanga alitaka wafuasi wa ODM kuungana na kutokubali ‘nguvu za nje’ kuwagawanya.

Alikuwa akizungumza katika makazi ya marehemu Were, Kachien, Homa Bay alipowasili kwa maombolezo.

Mazishi ya marehemu yatafanyika Mei 9, 2025.

Bi Wanga alikuwa pia na Kiongozi wa Wachache Bungeni Junet Mohamed.

Alisema kwamba hadithi kuhusu maisha ya Were ni njama ya kugeuza mkondo kuepusha uwajibikaji kuhusu mauaji yake.