• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
KERICHO: Shule ya chekechea ilivyogeuzwa danguro

KERICHO: Shule ya chekechea ilivyogeuzwa danguro

ANITA CHEPKOECH na CHARLES WASONGA

SHULE moja ya chekechea katika Kaunti ya Kericho sasa imegeuzwa kuwa danguro kijijini baada ya ujenzi wake kukwama miaka kadha iliyopita.

Kabirer Early Childhood Development Education (ECDE) iliyoko katika kaunti ndogo ya Sigowet Soin ni miongoni mwa shule kadhaa za chekechea ambazo ujenzi wazo umekwama lakini ripoti ya serikali ya kaunti kuhusu hali ya kukamilishwa kwa miradi inaonyesha kuwa miradi hiyo ilikamilishwa.

Taifa Leo Dijitali ilipofika katika shule hiyo, iliipata bila ua huku unyamavu ukitanda kote, na nyimbo na kelele za watoto ambazo husikika katika madarasa ya watoto yakikosekana.

Mlango una maandishi ya kondomu aina ya “Sure condom”. Na baada ya kufungua mlango tunapata vipande vya kondomu vikiwa vimetapakaa kote katika sakafu ya darasa hilo ambalo halitumiki.

Bw Wesly Bor na Bi Ruth Kirui ambao ni wakazi wa kijiji cha Kabirer walisema ujenzi wa jengo hilo ulianza mnamo mwaka wa 2014 chini ya ufadhili wa serikali ya Kaunti ya Kericho.

“Jengo hili halijawahi kutumika. Halina madawati, ubao wa kuandikia na choo. Pia halijawekewa ua. Tunaiomba serikali ya kaunti ikamilishe ujenzi wake ili watoto wetu waweze kuitumia,” akasema Bw Bor.

Wakati wa kijiji hicho, hata hivyo, walisema wako tayari kugharamia kukamilishwa kwa choo na ununuzi wa madawati ili watoto wapate mahali pa kusomea badala ya kutembea mwendo mrefu wakitafuta shule.

Bw Wesley Bor ambaye ni mkazi wa kijiji cha Kabirer aonyesha jengo zima la shule hiyo ya chekechea. Picha/ Anita Chepkoech

 

Lakini baadhi yao wanasema walipata habari kwamba watu fulani wasiojulikana wanataka kituo hicho kisalie bila kutumika ili baadaye waweze kukibadili kuwa shule ya kibinafsi.

“Mwanakandarasi alichimba choo ya shimo na kuiacha bila kujenga. Hatufahamishwa kuhusu mwelekeo wa mradi huu,” akasema Bi Kirui.

Serikali ya Gavana Paul Chepkwony ilikuwa imeahidi kujenga jumla ya shule 650 za chekechea na vyoo 17 katika kila wadi katika kaunti ya Kericho kati ya mwaka wa 2013 na 2017.

Lakini Taifa Leo Dijitali imebaini kuwa ingawa mmoja kati ya miradi hiyo iliyoorodheshwa kama iliyokamilika, ujenzi wa mingine mingi haujafika viwango vinavyohitajika. Hii ni kwa sababu majengo hayo hayana samani, vyoo, ubao wa kuandikia kati ya mahitaji mengine ya kimsingi.

ECDE hizo ni pamoja na; Ogirgir, Kisabei, Lemeiywet, Kapcheluch, Chepkin, Koiyet, Kibolgony, Sosit, Koitalel, na Kimugul iliyoko katika eneo bunge la Kipkelion Mashariki. Ujenzi wa shule hizi zote aidha haujakamilishwa au uko katika hali ya kutoweza kutumika na wanafunzi.

Ujenzi wa shule ya Kesainet iliyoko katika kaunti ndogo ya Sigowet- Soin, haukuanza licha ya kutengewa Sh750,000 katika bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2014/2015.

Na ingawa shule ya Sosit inatumika, kuta zake tayari zimeanza kupata nyufa, sakafu ikichimbuka huku ikiwa na madawati matano pekee ambayo hayawatoshelezi mahitaji ya takriban wanafunzi 30 waliosajiliwa kusomea hapo.

Vipande vya kondumu vilivyotapakaa kwenye sakafu ya jengo la shule hiyo ya chekechea. Ujenzi wa darasa hilo ambao ulisitishwa mnamo 2014 na sasa linatumika na wapenzi kulishana uroda. Picha/ Anita Chepkoech

Wanafunzi husomea katika hali ngumu huku walimu wakiendesha shughuli zao chini mti kwa sababu shule hiyo haina chumba cha walimu.

Bi Fancy Ngeno, ambaye ni kaimu mwalimu mkuu katika shule hiyo, alisema kuwa wanaomba vyoo kutoka kuwa shule jirani ya msingi ya Sosit.

“Hii ina maana kuwa watoto hawa wadogo hulazimika kuchanganyana na wale wakubwa kutoka shule hii jirani, hali ambayo husababisha usumbufu,” akasema.

“Mwanakandarasi alichimba shimo la choo na akaliacha wazi hali inayohatarisha maisha ya watoto. Tangu Julai 2014 hatujasikia habari zozote kutoka kwa serikali ya kaunti kuhusu mwelekeo kuhusu mradi huu na tunaiomba kukamilisha mradi huu kisha watununulie madawati,” Bi Ng’eno akaambia Taifa Leo Dijitali.

Bw Benard Korir, aliyekuwa Afisa Mkuu wa Elimu (ambaye sasa amehamishwa hadi katika idara ya ICT) alitetea serikali ya kaunti akisema shida ilitokea kwa sababu wakuu waliamua kuangazia idadi ya shule kuliko suala la ubora.

“Serikali ya kaunti ya Kericho iliamua kujenga vituo 600 vya ECDE kwa gharama ya Sh750,000 kila kimoja. Lakini baadhi yao waligundua kuwa bajeti hiyo ilikuwa ndogo hali iliyopelekea wao kufanya kazi chwara na kutokamilisha kazi inavyohitajika,” akasema Bw Korir.

Vile vile, alisema hapo bajeti ya awali ya ujenzi wa ECDEs ilikuwa Sh74 milioni lakini baadaye ikapunguzwa hadi Sh25 milioni, hali iliyoathiri ujenzi wa vyoo katika shule hizo.

Hata hivyo, Bw Korir anasisitiza kuwa baadhi ya shule ziko katika hali nzuri.

Mwalimu Mkuu wa shule ya chekechea ya Sosit Fancy Ng’eno (kulia) awaelekeza wafunzi chini ya mti ambao hutumika kama ofisi ya walimu. Picha/ Anita Chepkoech

Mapema mwezi huu Seneta wa Kericho Aaron Cheruiyot alifanya kikao na madiwani wa kaunti hiyo ambapo miongoni mwa masuala mengine, walijadili kero la kutokamilishwa kwa miradi mbalimbali kwa wakati.

Seneta huyo, kiongozi wa wengi Hezron Cheruiyot na Spika wa Bunge Dominic Rono walisema wanaandaa orodha ya miradi ambayo imekwama ili wafahamu kiini cha hali hiyo na afisa wa kulaumiwa.

“Tunashughulikia malalamishi ya wakazi kuhusu miradi yote, ikiwemo ile ambayo imekwama japo imefadhiliwa kwa pesa za umma. Baada ya hapo tutajua maafisa ambao tutawawajibisha,” akasema seneta Cheruiyot.

Spika huyo alisema bunge hilo limefanya kila liwezalo kuhakikisha kuwa pesa za miradi zinatengwa, lakini “inasikitisha kuwa baadhi ya miradi iliyotengewa fedha haijakamilishwa.”

“Katika siku 14 zijazo, kwa kuzingatia sheria za bunge na sheria za serikali za kaunti, tutachukua hatua kali dhidi ya maafisa husika,” akasema Bw Rono.

Naye kiongozi wa wengi akasema: “Nimewaomba madiwani wote kunipa orodha ya miradi iliyokwama katika wadi zao. Kisha tutazunguka tukikagua miradi hii na kuhakikisha kuwa maafisa husika wanawajibikia utepetevu wao kazini.

Miradi mingine ambayo imechukua muda mrefu kabla ya kukamilishwa licha ya kufyonza mamilioni ya fedha ni pamoja na Kiwanda cha Mananasi kilichoko eneo la Roret ambacho tayari mwanakandarasi mmoja amelipwa Sh7 milioni, upanuzi wa eneo la kuwapokea wagonjwa katika hospitali ya Kapkatet uliogharimu Sh10 milioni miaka mitatu iliyopita lakini haijaanza kutumika.

Pia kuna mradi wa maji wa Chepcholio katika eneobunge la Kipkelion Kaskazini uliogharimu Sh10 milioni lakini haujazinduliwa na visima kadha vilivyochimbwa lakini havina maji.

You can share this post!

Grace Msalame kushtaki UG kwa kutumia picha zake kuvumisha...

Furaha kwa Awiti na wafuasi wake mahakama kuamuru alibwaga...

adminleo