Pambo

Siri ya kugusa kina cha moyo wa akina dada

Na BENSON MATHEKA May 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KUNA mambo ya msingi ambayo wanawake hushabikia sana kwa wanaume, mambo ambayo yakizingatiwa, hujenga misingi imara ya mahusiano ya kudumu na yenye furaha.

Wanawake wanathamini sana mwanaume mkweli. Si rahisi kwao kuamini haraka, na hivyo mwanaume anayesema ukweli hata katika hali ngumu kwa ana thamani.

“Hii huwajengea imani na huwafanya wajihisi salama kimapenzi na kihisia,” asema mwanasaikolojia Jane Kamau.

Anasema japo maneno matamu yanaweza kuvutia mwanamke, ni vitendo thabiti vinavyomfanya agande kwa mwanamume.

“Wanawake hushabikia mwanaume ambaye huonyesha upendo kwa vitendo;kumjali, kumpa muda, na kufanya jitihada kumfurahisha,” aeleza.

Mara nyingi mwanamke hutaka tu asikizwe, sio kupewa suluhisho. Wanawake hushabikia mwanaume anayejua kusikiliza kwa makini, bila kukatiza au kutoa hukumu. Hili humfanya ajihisi anapewa nafasi na heshima.

“Na wanawake huona muda kama kipimo cha upendo. Zawadi hazitoshi ikiwa mwanaume haonyeshi uwepo wake wa kihisia na kimwili.

Kupiga simu ya kujulia hali au ujumbe wa haraka wa “nakupenda” ni zaidi ya zawadi ya thamani,” ashauri Kamau

Daisy Kwamboka, mshauri wa masuala ya mahusiano anasema wanawake hujitoa kwa moyo wote katika mahusiano, na mara nyingi hujikuta wakichukuliwa wa kawaida.

“Mwanaume anayemthamini, kumpongeza, na kumsaidia mwanadada katika ndoto zake huvutia zaidi. Hili linafanya mwanamume kujijengea heshima ya kina kwa mwanamke,” aeleza.

Kulingana na Kwamboka, kila mwanamke ni wa kipekee.

“Wanawake huchoshwa na wanaume wanaowalinganisha na wapenzi wa zamani, wanawake maarufu au mitazamo ya kijamii. Wanapenda mwanaume anayewajua wao kama wao, anayejifunza tabia na ndoto zao binafsi,” asema.

Anaongeza kuwa wanawake hushabikia mwanaume asiyebadilika ghafla, aliye na msimamo wa tabia, mapenzi na kauli. Uaminifu katika tabia humfanya mwanamke ajihisi salama na kujitolea kujenga maisha kwa pamoja kwa uhakika.

Na ana ushauri kwa wanaume wanaodhani wanawake wanatambua ngono kama msingi wa mahusiano.

“Ingawa wanawake hufikiria kuhusu ngono, hawataki mahusiano yajengwe tu kwa msingi huo. Wanapenda mwanaume anayegusa moyo wao kwanza, anayewaelewa kihisia. Hii huongeza ukaribu wa kihisia na hata wa kimwili,” asema.

Kamau anasema wanaume bahili wa hisia hawana chao kwa kuwa wanawake wanapenda kuonyeshwa mapenzi hadharani kama ilivyo faraghani.

“Mwanaume anayeshika mkono wake hadharani, kumwangalia kwa jicho la upendo na kumwita kwa jina la heshima mbele za watu humfanya mwanadada ajihisi maalum na kujivunia uhusiano wao,” asema.

Mwanaume mwenye maono maishani, aliye thabiti na mwenye kujitambua ni mvuto mkubwa kwa kina dada. Mwanadada hushabikia mwanaume mwenye dira, aliye tayari kushirikiana naye katika ndoto na changamoto za maisha.

Kamau na Kwambok wanakubaliana kuwa kupendwa na mwanamke ni baraka, lakini ni jukumu la mwanaume kuhakikisha anapanda mbegu bora ya upendo, heshima, na uaminifu.

Wanawake hawahitaji mwanaume mkamilifu, bali mwanaume anayejitahidi kuwa bora kila siku kwa ajili ya upendo wao.

Wakipata hilo, hawachelewi kuleta baraka, uzuri, na ongezeko katika maisha ya mwanaume kama huyo.