Habari za Kitaifa

Uhuni Gusii Stadium mashabiki wakiumia katika mechi kati ya Shabana na Gor Mahia

Na WYCLIFFE NYABERI May 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

UHUNI katika soka ya Kenya ulijitokeza tena Jumapili katika Uwanja wa Gusii, Kaunti ya Kisii, mashabiki wa Shabana na Gor Mahia FC wakilimana makonde kabla ya mechi ya ligi baina ya timu zao.

Vurugu hizo ambazo zimesababisha mashabiki kadhaa kujeruhiwa, zilizuka baada ya mashabiki wa Shabana na K’ogalo kuzozania maeneo ya kukaa katika majukwaa ya raia wa kawaida, maarufu kama terraces.

Majukwaa ya terraces katika uwanja huo, yanaangaliana na jukwaa la watu wa kiwango cha juu maarufu kama VIP.

Mashabiki wakiwa katika hali ya mshikemshike ugani Gusii Stadium, Kisii. Picha|Wycliffe Nyaberi

Majukwaa hayo ya raia wa kawaida, yamepewa majina kuanzia G1 hadi G13.

Kando na jukwaa la VIP ambalo lilikuwa wazi kwa mashabiki wa timu zote mbili, waandalizi wa pambano hilo waliwatengea mashabiki wa Shabana stendi 10 za kawaida huku Gor Mahia wakipewa tatu tu.

Hata hivyo, stendi hizo tatu hazikutosha kuwasitiri mashabiki wengi wa Gor Mahia ambao walijaza haraka uwanja huo mapema kufikia saa tano asubuhi, huku mechi ikiratibiwa kuanza saa nane alasiri.

Walipoona kuwa mashabiki wa Shabana wametengewa nafasi nyingi kuliko wao, mashabiki wa Gor Mahia walianza kuingia kwa nguvu kwenye stendi zingine.

Vurugu katika Gusii Stadium muda mfupi kabla ya mechi kati ya Shabana na Gor Mahia. Picha|Wycliffe Nyaberi

Kutokana na hali hiyo, vurugu zilizuka huku mashabiki wote wakianza kujibizana kwa urushaji mawe na vifaa vingine butu.

Mazingira ya uwanja yaliyokuwa yamesheheni mbwembwe na hanham za kila aina, yaligeuka haraka na kuwa uwanjwa wa masumbwi huku mawe yakitawala anga za uwanja huo.

Maafisa wa polisi waliomwagwa uwanjani humo kuleta usalama, walilemewa kuwatuliza mashabiki hao.

Kutokana na fujo hizo, mashabiki kadhaa, wengi wao wakiwa wanawake walijeruhiwa na ilibidi kukimbizwa na ambulensi hospitalini.

Ilichukua zaidi ya dakika 30 kwa hali ya kawaida kurejea uwanjani.

Takriba watu 50 walijeruhiwa wengi wao wakiwa wanawake na watoto. Picha|Wycliffe Nyaberi

Kulikuwa na ubishi mkubwa mitandaoni baina ya mashabiki wa timu hizo mbili kabla ya siku ya mechi hiyo kuwadia.

Mashabiki hao wote walikuwa wakijinadi kuhusu atakayeibuka mshindi.

Kutokana na wafuasi wengi wanaoshabikia timu hizo mbili, klabu cha Gor Mahia ilitaka mchezo huo uandaliwe katika uwanja mkubwa zaidi ya ule wa Gusii ndiposa usheheni mashabiki wengi.

Lakini Shabana walisisitiza kwamba mechi hiyo inapaswa kuchezwa katika uwanja wao wa kuchukua mashabiki 12, 000 liwe liwalo.

“Mashabiki kutoka timu zote mbili wamekuwa wakizozana mitandaoni kuhusu nani atakuwa mshindi katika mechi hii. Ninashuku kuwa hilo limechangia pia kuzua hasira katika mechi hii,” mchezaji wa zamani wa Shabana Bernard Pepe alisema.

Awali kabla ya vurugu hizo kutokea, shughuli katika mji wa Kisii, ambapo uwanja wa Gusii unapatikana zilisimama huku mashabiki wa Shabana na Gor Mahia wakimiminika uwanjani.

Mashabiki hao walianza kuwasili mapema saa moja asubuhi kwa ajili ya mechi inayotarajiwa kuanza saa nane mchana.

Ilipofika saa tano unusu asubuhi, uwanja ulikuwa tayari umejaa huku mashabiki wengine wengi wakiwa wamepanfa foleni nje wakisubiri kukata tikiti za kushuhudia pambano hilo lililopewa jina la “Debi ya Nyanza”.

Mashabiki wa Shabana na K’ogalo walizozania maeneo ya kukaa katika majukwaa ya raia wa kawaida, maarufu kama terraces. Picha|Wycliffe Nyaberi

Kwa mara ya kwanza katika historia yake, Uwanja wa Gusii uliwekwa televisheni za LED kwa matangazo na uidhinishaji mwingine.

Fataki zinatarajiwa katika pambano hilo.

Ushindi kwa upande wowote utakuwa muhimu katika kutafuta taji ambalo kihisabati linaweza kushindwa na timu hizo mbili.

Shabana wamekuwa kwenye kiwango kizuri wakicheza nyumbani. Wameufanya uwanja huo kuwa “jahanamu” kwa  timu geni hasa tangu kuteuliwa kwa kocha Peter Okidi ambaye alichukua mikoba ya Sammy “Pamzo” Omollo mnamo Januari.

Shabana wapo nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi wakiwa na pointi 46 huku Gor Mahia wakiwa juu yao katika nafasi ya ratu na pointi 50.

Shabana imeshinda mechi zake nne zilizopita na wamekuwa kwenye mfululizo wa michezo nane bila kufungwa.