Habari za Kitaifa

Tumejipanga kumpeleka Ruto nyumbani – Upinzani

Na MWANGI MUIRURI May 5th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

VIONGOZI wa upinzani wanaolenga kuandikisha historia ya kumfanya Dkt William Ruto kuwa Rais wa kwanza kuhudumu kwa muhula moja pekee Jumapili walijumuika kwa ibada maalum kumuomba Mungu awape ushindi.

Walikongamana katika boma la aliyekuwa Naibu wa Rais Bw Rigathi Gachagua lililoko kijiji Cha Wamunyoro, Kaunti ya Nyeri. Upekee wa ibada ni kwamba japo uliongozwa na viongozi wa Kikristo, ilishuhudia pia mseto wa nyimbo za kitamaduni na Kikristo.

Vinara wa upinzani waliojumuika na Bw Gachagua katika ibada hiyo ni kiongozi wa Wiper Bw Kalonzo Musyoka, pamoja na aliyekuwa Waziri wa Usalama wa ndani Bw Fred Matiang’i anayeungwa mkono na rais mstaafu Bw Uhuru Kenyatta na aliyekuwa Waziri wa Utumishi wa Umma Justin Muturi.

Wengine walikuwa kiongozi wa chama cha Peoples’ Liberation Party (PLP) Martha Karua, Eugene Wamalwa (DAP-K) na wabunge wa zamani Kwanza Noah Wekesa (Wekesa) na Kipruto arap Kirwa (Cherangany). Ujumbe wa viongozi kutoka Kajiado ukiongozwa na Seneta Senku Ole Kanar pia walikuwepo.

Bw Gachagua alikariri kujitolewa kwa viongozi wa muungano huo kumuunga mkono mgombeaji mmoja katika kinyang’anyiro cha urais atakayemwangusa Rais Ruto 2027.

Alisema yeye ni kiongozi wa kitaifa tofauti na dhana iliyoendelezwa na “wale walionitoa afisini”.

“Walionitimua mamlakani wakiniita mkabila sasa wajionee kwa macho urafiki ambao ni wa kitaifa na unaonizingira hapa wote ukitaka tusaidiane kukomboa nchi hii ambayo imegeuzwa kuwa ya kilio tupu,” akasema Bw Gachagua.

“Utakuwa usaliti hata kwa nafsi zetu kukosa kuelewana jinsi ya kukomboa taifa hili letu. Mungu atujalie neema za kufika 2027 na jibu la kuokoa taifa kutoka kwa udhalimu wa Kasongo tutalitoa,” akaongeza.

Kwa upande wake, Bw Musyoka alipuuza habari kwamba huwa ananyemelea Rais Ruto kisirisiri ili kupata marupurupu ya kuhujumu muungano wa upinzani 2027.

“Mimi na Ruto ni kama maji na mafuta. Utawala ulio na damu ya vijana wetu wa Gen Z siwezi kamwe nikaufanya kuwa wa urafiki. Mimi niko katika mrengo wa Wanjiku, ukombozi wa nchi hii na pia wa uzalendo wa kujua hatuna nafasi ya kuwapa Wakenya matukaini feki,” akasema.

Bi Karua alisema kwamba kwa sasa malengo yote ya Wazalendo wa traifa hili yameelekezwa kwa bidii za kuhakikisha Ruto na wandani wake hawapati muhula wa pili serikalini.

“Nchi imechuuzwa huku maghala yake yakiporwa. Serikali hii haithamini taasisi huru na udikteta wa kutawala kwa vitisho ndio umesheheni. Rais Ruto aambiwe gangaganga za mganga, maombi na imani zote zimeungama kwamba afunganye virago awakome Wakenya,” akasema.

Kwa upande wake Dkt Matiang’i aliwataka wandani wa Rais Ruto kukoma kuingiwa na wasiwasi kuhusu kujitosa kwake katika kinyang’anyiro cha urais akisema “huu ni mwanzo tu.”

“Sasa kile tunaomba ni Wakenya waweke amani, wazidi kuwa na subira na Imani yenu iwe thabiti kwa

Mungu kwamba hili wingu la majonzi litapita na neema ya ukombozi itushukie hivi karibuni”, Dkt Matiang’i akaeleza.

Waziri huyo wa zamani wa Usalama aliongeza mwenge wa upinzani “umeanza kung’aa katika giza la mahangaiko “ni wa kutia moyo na Mungu atafanikisha jitihada zinazosukwa”.

Bw Wamalwa, naye alisema kwamba safari ya kumpeleka Rais Ruto nyumbani iko na nia, uwezo na sababu.

“Huyu tunamkataa kwa kuwa anaongoza serikali ya mauaji dhidi ya vijana na pia ufisadi. Utawala wake umewapa wakulima mbolea feki na amekuwa akinadi Taifa letu kwa makateli ya kimataifa,” akasema.

Kiongozi huyo wa DAP-K aliongeza kwamba iwapo kwa bahati mbaya Rais Ruto ataponea na arejee afisini kwa awamu ya pili badi nyoyo za Wakenya ndizo zitachuuzwa baada ya rasilimali zote kufisadiwa.