Haki hatimaye? DPP aagiza maafisa wa KWS washtakiwe kwa kutokomeza mvuvi Nakuru
MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP), Renson Igonga, amependekeza maafisa sita wa Shirika la Huduma kwa Wanyamapori (KWS) wanaohusishwa na kutoweka kwa mvuvi jijini Nakuru washtakiwe kortini.
Bw Igonga ameamrisha sita hao washtakiwe kwa utekaji nyara kwa kuwa walikuwa na Brian Odhiambo kabla ya kutoweka kwake.
Odhiambo alitoweka mnamo Januari 18 ikidaiwa alinyakwa na maafisa wa KWS.
Polisi hao sita ambao walikuwa wakiwajibikia kazi yao kwenye mbuga ya Ziwa Nakuru ni afisa wa ngazi ya juu wa cheo cha sajini Francis Wachira, na wenzake Abdulrahman Ali Sudi, Isaac Ochieng, Evans Kimaiyo, Michael Wabukala na Alex Lorogoi ambao ni wa KWS.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Idara ya Upelelezi(DCI) Nakuru Mashariki, Samuel Ngeiywo, sita hao wameshakamatwa kuelekea kufikishwa kwao kortini mnamo Jumatatu.
“Walinyakwa Ijumaa lakini wakaachiliwa kwa dhamana wakisubiri kufikishwa kortini Jumatatu,” akasema Bw Ngeiywo.
Mkuu huyo wa DCI Nakuru alifichua kuwa waliandikia DPP ili polisi hao sita washtakiwe kwa mauaji lakini mashtaka yakabadilishwa na sasa watashtakiwa kwa utekaji nyara.
Kwenye mahojiano ya simu, mkewe Bw Odhiambo, Ivy Aoko, alisema walifahamishwa kuhusu kamatakamata hizo na maafisa wa DCI. Bi Aoko alisema kukamatwa kwa maafisa hao sita kumefufua matumaini yake ya kupata haki.
“Nililia niliposikia wamekamatwa na natumai kwa kwa sababu wao ndio walionekana mara ya mwisho na mume wangu, wataeleza korti mahali ambapo yupo,” akasema Bi Aoko.
Mkuu wa Shirika la Kupigania haki za kibinadamu Nakuru (NAHURINET), David Kuria, alifurahia mashtaka dhidi ya sita hao akisema sasa wana matumaini ya kupatikana kwa Bw Odhiambo.
“Familia ya Odhiambo haijakuwa na amani tangu kutoweka kwake. Tunatarajia kuwaona kortini Jumatatu na nina hakika wataeleza aliko,” akasema Bw Kuria.
Kauli yake iliungwa mkono na Khalid Hussein wa VOCAL Afrika ambaye alisema kesi hiyo inastahili kuharakishwa ili familia ya Bw Odhiambo ipate haki.
“Tunataka kujua Odhiambo yuko wapi na tunatoa wito kwa Wakenya wajitokeze na kusimama na familia yake kortini,” akasema BW Khalid.
Mnamo Machi 19, alipotembelea Nakuru, Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen aliahidi kuwa serikali itaingilia kati kuhakikisha kuwa Bw Odhiambo anapatikana.
Pia aliahidi kuwa polisi wa KWS ambao walihusika na kutoweka kwake watawajibikia kitendo chao. Alizungumzia kisa hicho baada ya mamake Odhiambo, Elizabeth Auma kuvuruga hotuba yake Nakuru.
Mnamo Machi 13, Hakimu Mwandamizi wa Nakuru Vincent Adet aliamrisha DCI na KWS ziendeleze uchunguzi wao kisha wafikishe faili kwa DPP ili hatua ichukuliwe ndani ya siku 30. Muda huo ulipita mnamo Aprili 13.
Bw Odhiambo, 33 alitoweka mnamo Januari 18,2025 baada ya kukamatwa na maafisa wa KWS katika mbunga ya wanyama ya Ziwa Nakuru.
Kwa mujibu wa familia yake, alinyakwa kwa kuvua samaki kwenye mbuga hiyo na maafisa wa KWS walimuendea nyumbani kwake Manyani ambapo walimshika.