Habari

Miili ya Wakenya waliofariki UAE yaletwa kwa mazishi

Na KEVIN CHERUIYOT May 5th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

BAADA ya kusubiri kwa muda mrefu, familia za Wakenya waliokufa mwezi jana katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) watapata nafasi ya kuwapa wapendwa wao mazishi ya heshima.

Hii ni baada ya ubalozi wa Kenya kufaulu kutayarisha stakabadhi za kusafirishwa kwa miili hiyo hadi Kenya. Wakenya hao walikufa katika eneo la Sharjah katika ajali ya moto katika makazi ambako walikuwa wakiishi.

Mnamo Jumapili, mwili wa Ian Ndunguare uliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) na kusafirishwa hadi katika hifadhi ya maiti ya Montezuma jijini Nairobi kabla ya mazishi kufanyika Jumamosi wiki hii.

Kulingana na Wakenya ambao wamekuwa wakiendesha mipango ya kurejesha miili hiyo nyumbani, mwili wa Mkenya mwingine, Benjamin Kioko, ulitarajiwa kuwasili Kenya jana asubuhi.

“Wapendwa Wakenya. Tunathibitisha kuwa mwili wa Benjamin utasafirishwa kwa ndege ya KQ 311 na kufiki saa kumi na mbili alfajiri saa za Kenya huku ule wa Kenneth Kamau ukitarajiwa kufika saa tano za mchana saa za Kenya. Kibali kimetolewa kwa usafiri wa miili hiyo miwili,” waandalizi wakasema katika taarifa ya kuwapasha habari Wakenya ambao wamekuwa wakichanga pesa kugharamia usafirishaji wa miili hiyo.

Tarehe za mazishi ya Kioko na Kamau hazijatengwa. Hata hivyo, familia zao zimewashukuru Wakenya wanaoishi UAE kwa msaada wao.

“Ubalozi wa Kenya na afisi ya kibalozi ingependa kutoa shukrani kutokana na umoja ambao Wakenya wanaoishi katika nchi hiyo ya Kiarabu. Tunawaomba kudumisha umoja huo,” ikaeleza taarifa hiyo.

Tangu kisa hicho kilipotokea Aprili 13, Wakenya walioko UAE waliungana kuchanga pesa za kusaidia familia za walioathirika. Pesa hizo zitasaidia familia hizo kuwazika wapendwa wao.

Kufikia Jumapili, jumla ya Sh1.6 milioni zilikuwa zimechangwa, japo kiasi lengwa kilikuwa Sh3.5 milioni.

Wiki jana, ripoti ya polisi katika eneo la Sharjah ilifichua kuwa hitilafu ya umeme ndio ilisababisha moto uliopelekea vifo vya watu watano katika jengo la makazi.