Gen Z aliyerushia Rais Ruto kiatu atambuliwa na kunyakwa
POLISI wamemtambua kijana barobaro ambaye kwa ujasiri wa aina yake alidiriki kumrushia kiatu Rais William Ruto Jumapili, katika Kaunti ya Migori.
Kulingana na taarifa iliyotolewa na Kituo cha Polisi cha Kehancha Jumatatu, Mei 5, 2025, mshukiwa huyo anajulikana kama Paul Mutongori Marwa, wa asili ya Kuria na mwenye umri wa miaka 18.
Ni mkazi wa Kaunti Ndogo ya Kuria Magharibi.
“Yeye ndiye mshukiwa aliyenaswa kwenya kamera akirusha kiatu kwa Rais. Alikamatwa Jumapili jioni katika Smile Bar, mjini Kehancha,” taarifa hiyo ikaeleza.
Wengine waliokamatwa ni; Ezron Muhurai Mwita, 22 na Nicholas Sangonyi Mwita, 20 ambao ni wanaume wa kabila la Kuria.
“Washukiwa hawa wawili, walikuwa wakimzomea Rais alipokuwa akihutubu. Watatu hawa wanatoka Kuria Magharibi, kata za Komasincha na Taranganya. Wamezuiliwa na wanawasaidia polisi katika uchunguzi,” taarifa hiyo ikaongeza.
Kisa hicho ni cha kwanza cha kutishia usalama wa Rais Ruto tangu alipoingia afisini mnamo Septemba 13, 2022.
Kilitokea baada ya kiongozi wa taifa kuhudhuria ibada maalum iliyoongozwa na makanisa mbalimbali katika uwanja wa Shule ya Msingi ya Kadika, eneo bunge la Suna Mashariki.
Kisha Dkt Ruto, ambaye aliandamana na viongozi wa kaunti hiyo wakiongozwa na Gavana Ochilo Ayacko, alifululiza hadi eneo bunge la Suna Magharibi ambapo alizindua ujenzi wa Chuo cha Mafunzo ya Kiufundi cha Piny Oyie.
Shughuli hizi zote ziliendelea kwa amani ambapo kiongozi wa taifa aliwahutubia wananchi akielezea mipango na miradi ambayo serikali yake inatekeleza katika maeneo husika.
Miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa masoko ya kisasa, kuunganishwa kwa nguvu ya umeme maeneo ya mashambani na ujenzi wa miundo mbinu hitajika kwenye fuo za Ziwa Victoria kuwafaidi wavuvi.
Lakini mkosi ulikumba awamu ya mwisho ya ziara yake, siku hiyo, iliyomfikisha katika eneo bunge la Kuria Magharibi.
Mkutano mkubwa wa watu walisongamana hadi karibu na jukwaa la Rais alipokuwa akihutubu na ndipo ghafla bin vu, mtu mmoja alimrushia kiatu na kutatiza hotuba yake kwa muda mfupi.
Hata hivyo, Dkt Ruto alijasirika na kuendelea na hotuba yake hadi akamaliza.
Kutokana na tukio hilo, usalama uliimarisha zaidi Jumatatu, Mei 5, 2025 Rais alipozuru maeneo kadhaa ya eneo bunge la Rongo na Muhuru Bay.
Rais hakuhutubia wanachi katika majukwaa yaliyokuwa wametengenezwa ila alizungumza akiwa kwenye paa la gari lake rasmi.
Maafisa wengine kutoka vikosi mbalimbali ikiwemo kikosi cha cha kupambana na fujo (GSU) walizingira gari la Rais Ruto katika vituo mbalimbali alikosimama kuwahutunia raia.