Jamvi La Siasa

Msipounga mkono Ruto, kiti cha Kindiki kitaenda 2027, Mudavadi aambia Mt Kenya

Na MOSES NYAMORI, CECIL ODONGO May 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KINARA wa Mawaziri, Musalia Mudavadi, ameonya wakazi wa ukanda wa Mlima Kenya kuwa watapoteza wadhifa wa naibu rais ambao sasa unashikiliwa na Profesa Kithure Kindiki iwapo watamtoroka Rais William Ruto kwenye uchaguzi mkuu wa 2027.

Bw Mudavadi amewataka wakazi wa eneo hilo waendelee kuunga mkono utawala wa Rais Ruto kwa sababu wanazidi kunufaika na miradi ya utawala wa Kenya Kwanza.

Rais Ruto alimteua Profesa Kindiki kuchukua mahala pa Rigathi Gachagua ambaye alitimuliwa kama naibu rais mnamo Oktoba mwaka jana.

Profesa Kindiki amekuwa akiendeleza mikutano mbalimbali na viongozi kutoka ukanda wa Mlima Kenya ili kuhakikisha bado wanaunga mkono Rais mnamo 2027.

Baada ya kuonekana kupoteza uungwaji mkono wa Mlima Kenya, Rais anaonekana kuelekeza macho yake katika ngome za Kinara wa Upinzani Raila Odinga katika eneo la Nyanza.

Baadhi ya wandani wa Bw Odinga tayari wanahusishwa na nafasi ya kuwa mgombeaji mwenza wa Rais Ruto akiwemo Gavana wa Homa Bay, Gladys Wanga.

Bw Mudavadi hivi majuzi alivunja chama chake cha ANC na kuungana na kile cha UDA na mwenyewe pia ametajwa kama anayesaka kuwa mgombeaji mwenza wa rais 2027.

Akiongea katika Kanisa la AIPCA Othaya, Nyeri, Bw Mudavadi alisema eneo la Mlima Kenya linastahili kujihadhari kwa sababu kuna watu wengi kutoka maeneo mengine ambao wanataka kuchukua wadhifa wa unaibu rais.

“Nataka niwapongeze viongozi kutoka hapa Mlima Kenya ambao wameendelea kuunga mkono utawala wa Rais Ruto lakini mkiendelea kucheza, itawatoka,” akasema Bw Mudavadi.

“Ndege unaye mkononi ni bora kuliko yule aliye msituni. Kuna Wakenya hapa nje ambao wangependa kuwa tu na robo ya kile mnachoshikilia sasa,” akaongeza.

Aliwataka wakazi na viongozi wa eneo hilo waendelee kufanya kazi kwa kushirikiana na rais, akisema kiongozi wa nchi ana imani kuwa wakazi wa eneo hilo bado wanaunga mkono serikali yake.

Bw Mudavadi alitoa kauli hiyo huku Profesa Kindiki ambaye alikuwa akizungumza kwenye hafla tofauti akisema eneo hilo halitayumbishwa na siasa za shutuma na za ubabe ambazo zinaendelezwa na mrengo wa Bw Gachagua.

“Kwa sasa sisi hatumakinikii siasa za uchaguzi wa 2027. Tuna kipimo kinachokuja ambapo tutaulizwa iwapo tulimaliza miradi tuliyoahidi na kile tulichofanya kuboresha maisha ya Wakenya,” akasema Profesa Kindiki.

Alikuwa akiongea wakati wa mkutano wa kiuchumi katika eneo la Igegania, Gatundu Kaskazini, Kaunti ya Kiambu. Naibu Rais aliongeza kuwa watakuwa tayari kukabiliana na wapinzani wao mnamo 2027 lakini kwa sasa wanamakinikia kuimarisha utoaji wa huduma kwa raia.

“Namakinika sana kufanya kazi na umakinifu wangu hautavurugwa na yeyote. Kibarua kilichoko ni kumsaidia rais atekeleze ahadi zake kwa Wakenya, aimarishe maisha ya wakulima, abuni nafasi za ajira na kupunguza gharama ya maisha,” akaongeza Profesa Kindiki.

Kwa mujibu wa mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Javas Bigambo Mlima Kenya Mashariki (Embu, Meru na Tharaka-Nithi) kwa sasa hawamtaki Rais Ruto na Profesa Kindiki akitolewa kama mgombeaji mwenza basi hatakuwa na lake 2027.

“Siasa ni karate na bado kutakuwa na kambi kadhaa ambazo zitachipuka kuelekea siasa za 2027. Ruto anahitaji uaminifu wa Profesa Kindiki hasa Mlima Kenya Mashariki na itakuwa vigumu sana amwaachilie,” akasema.

“Kwa upande mwingine wakazi wa Mlima Kenya Mashariki  wataona heri waunge Rais na kusalia na Profesa Kindiki kama mgombeaji mwenza badala ya kuenda kambi ya Rigathi Gachagua ambako hawakaribii hata wadhifa huo.

“Mtu ambaye atakuwa mgombeaji wa Rais Ruto atakuwa mtu mwaaminufu na lazima awe na kura nyingi. Hizi zitaamua iwapo Profesa Kindiki atabaki na Ruto au kiti chake kitaendea ODM  au Mudavadi,” akaongeza.

Naye Martin Andati amekejeli Bw Mudavadi akisema alikuwa apokezwe unaibu rais wakati Bw Gachagua alitimuliwa lakini akawaachilia kiti kikaenda.

“Kulikuwa na makubaliano Musalia apokezwe kiti lakini kwa kutokuwa mkakamavu akawacha kikaenda. 2027 bado ni mapema kwa sababu siasa zinabadilika,” akasema Bw Andati.