Maoni

MAONI: Usalama wa Rais ni usalama wa taifa, haufai kuhujumiwa kwa vyovyote vile!

Na BENSON MATHEKA May 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

USALAMA wa kiongozi wa nchi ni suala linalohitaji kupewa uzito wa hali ya juu, hasa baada ya tukio ambapo Rais William Ruto alirushiwa kiatu na raia katika mkutano wa hadhara uliofanyika Migori.

Tukio hili, pamoja na dalili za kuongezeka kwa hasira miongoni mwa wananchi kutokana na hali ya kiuchumi inayoendelea kudorora na joto la siasa nchini, linaibua maswali mazito kuhusu mikakati ya ulinzi wa viongozi wakuu wa kitaifa na hali ya uhusiano kati ya serikali na wananchi.

Kwa mujibu wa taratibu za kiusalama, Rais anapaswa kulindwa kwa viwango vya juu wakati wote na mahali popote.

Hata hivyo, tukio hilo linaonyesha mapungufu katika kupanga na kutekeleza mikakati ya usalama, hasa katika mikutano ya umma.

Hili ni onyo kwa vyombo vya usalama na mamlaka husika kuimarisha ulinzi wa viongozi bila kupunguza fursa ya wananchi kujumuika nao.

Hasira za wananchi zinazojitokeza wazi si tu tishio kwa usalama wa Rais bali pia ishara ya hali tete inayotokana na ugumu wa maisha, ukosefu wa ajira, ongezeko la ushuru na gharama ya maisha, pamoja na kutoridhika na utendakazi wa serikali.

Serikali inapaswa kuchukulia hali hii kwa uzito, ikitambua kuwa usalama wa Rais hauwezi kutenganishwa na usalama wa wananchi na utulivu wa taifa.

Kwa hivyo, kunahitajika juhudi za haraka kurejesha imani ya wananchi kwa serikali kupitia mazungumzo ya wazi, sera zinazowajali raia moja kwa moja, na utekelezaji wa haki na usawa.

Vinginevyo, hali ya kutamauka ya wananchi inaweza kuendelea kuzua vitendo vya uasi vinavyoweza kuhatarisha si tu viongozi bali pia mshikamano wa kitaifa.

Licha ya haya, Rais anafaa kuheshimiwa kama kiongozi mkuu wa taifa, bila kujali tofauti za kisiasa au hali ya uchumi.

Kitendo cha kurushiwa kiatu si tu tishio kwa usalama wake bali pia ni dhihirisho la ukosefu wa heshima kwa taasisi ya urais.

Heshima kwa Rais si suala la hiari bali ni msingi wa utawala wa sheria na utulivu wa kisiasa.