UDA yabaki gae Embu maafisa wote 89 wakihama
MAAFISA waratibu wote 89 wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) katika Kaunti ya Embu Jumatano walihama chama hicho tawala wakikilaumu kwa kuwatupa baada ya uchaguzi.
Walipokuwa wakihama, maafisa hao walidokeza kuwa huenda wakajiunga na chama kipya cha Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua, ambacho kinatarajiwa kuzinduliwa mwezi huu.
Hatua hiyo ni pigo kubwa kwa uongozi wa kitaifa wa UDA chini ya Rais William Ruto, hasa ikizingatiwa kuwa Gavana wa Embu Cecily Mbarire ni mwenyekiti wa kitaifa wa chama hicho, na wakati huu ambapo uchaguzi mdogo unakaribia kufanyika Mbeere Kaskazini.
Kiti hicho kilibaki wazi baada ya Mbunge Geoffrey Ruku kuteuliwa kuchukua nafasi ya aliyekuwa Waziri wa Utumishi wa Umma, Justin Muturi, aliyefutwa kazi.
Wakiongozwa na Bw Joshua Kanake, mratibu wa UDA kaunti ya Embu, maafisa hao kutoka wadi zote 20 walipitisha azimio la kutokuwa na imani na UDA baada ya kikao cha faragha kilichofanyika katika hoteli ya Izaak Walton mjini Embu.
Walishutumu serikali kwa kuwaacha mara tu baada ya UDA kushinda uchaguzi wa 2022 na kusema sasa “wanasikiliza sauti ya wananchi” na hivi karibuni watatangaza mwelekeo wao mpya wa kisiasa.
“Tulipigia debe Kenya Kwanza mashinani, tukatumia rasilimali zetu, nguvu na muda wetu, lakini baada ya uchaguzi tukasahaulika kabisa,” alisema Bw Kanake.
Aliendelea kusema: “Tulijaribu mara kadhaa kufikia viongozi wakuu wa chama lakini tulipuuzwa, hivyo basi hatuwezi kuendelea kuwa ndani ya UDA.”
Bw Kanake, ambaye pia ni Naibu Mweka Hazina wa Kitaifa wa chama tawala anayesimamia mipango maalum, alisema hawakuzawadiwa hata baada ya kufanya kazi nzuri na juhudi zao za kutafuta nafasi ya kusikizwa hazikuzaa matunda.
Kundi hilo lilisema sasa wao ni viongozi wa mashinani walio huru, walio tayari kushirikiana na watu wengine “wenye nia sawa,” huku Bw Kanake akisema kuwa “UDA Embu imekufa na kuzikwa.”
“Tumechoka na uongo na uongozi mbaya wa serikali, tumeachana na UDA. Wakati wa uchaguzi tuliahidiwa mbingu lakini tukajikuta motoni. Kwa sasa sisi ni watu huru na tuko tayari kushirikiana na watu wengine hata kama ni Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua na timu yake,” alisema Bw Kanake.
“Tumetendewa vibaya na kudharauliwa na hatuwezi kuendelea kubaki ndani ya UDA. Uamuzi wetu wa kukihama chama ulikuwa mgumu lakini hatukuwa na chaguo. Kwa sasa tunawasikiliza wananchi kwa makini ili watuelekeze njia sahihi ya kisiasa,” alisema Bi Joyce Murekio, mratibu wa Wadi ya Mbeti Kusini.
“Tunataka kuonyesha kutoridhika kwetu na UDA. Tulikijenga chama kuanzia chini lakini hatukutambuliwa. Tuna serikali ya ubinafsi sana na hatuwezi kuendelea kujifanya kila kitu kiko sawa. Tumeamua kuhama UDA na kuendelea mbele,” aliongeza.
Mratibu wa UDA wa Mbeere Kusini Dkt Gerald Ireri, alisema kuwa uongozi wa UDA umegeuka kuwa wa mtu mmoja, wakidai hata wananchi wamekikataa chama hicho tawala.
Walisema pia hawaridhishwi na visa vya kutekwa kwa vijana, mauaji ya kiholela, na usimamizi mbaya wa rasilimali za taifa.
“Yale yanayofanyika nchini Kenya hayawezi kuvumilika. Tumepumbazwa na serikali hii kwa sababu hatujafaidika na chochote na Kenya Kwanza hata baada ya kuwarai wananchi kuichagua,” alisema Dkt Ireri.