Raila pabaya wabunge, raia wakimponda kwa msimamo wake kuhusu hela za CDF
KINARA wa chama cha ODM, Raila Odinga amejipata kona mbaya kufuatia kauli yake ya kutaka Hazina ya Kitaifa ya Maendeleo ya Maeneobunge (NG-CDF) ihamishwe kwa serikali za kaunti.
Wabunge na wananchi wameungana kuunga hazina hiyo kukitwa katika Katiba chini ya usimamizi wa Wabunge.
Katika vikao vya kukusanya maoni kuhusu mswada unaolenga kukita hazina hiyo katika katiba, wabunge walimkosoa vikali Bw Odinga kwa kutaka pesa hizo ziwekwe chini ya magavana.
Wabunge hao wanasema Bw Odinga anatoa matamshi ya kupotosha kuhusu umuhimu wa hazina hiyo ambayo kwa miaka mingi imechangia maendeleo ya msingi katika maeneo ya mashinani.
NG-CDF ilianzishwa rasmi mnamo 2015 chini ya Sheria ya NG-CDF kwa kubadilishwa jina kutoka Hazina ya Maendeleo ya Maeneobunge (CDF) iliyoanzishwa mnamo 2003, chini ya utawala wa Rais Mwai Kibaki.
Lengo kuu la Hazina hii ni kufanikisha miradi ya maendeleo kama vile ujenzi wa madarasa, vituo vya afya, na miundombinu ya usalama katika maeneobunge.
Hata hivyo, hatma ya hazina hii sasa imo mashakani baada ya Mahakama Kuu mnamo Septemba 2024, kutangaza kuwa ni kinyume cha Katiba.
Hii imezua mjadala mkali nchini kuhusu ikiwa inafaa kuondolewa au kujumuishwa rasmi kwenye Katiba kupitia marekebisho yanayopendekezwa.
Bw Odinga ameunga mkono uamuzi wa mahakama na kutaka fedha hizo ziende moja kwa moja kwa kaunti, akidai wabunge wanatumia hazina hiyo kuingilia majukumu ya ugatuzi.
“Ugatuzi haufanyi kazi kwa sababu wabunge wanaingilia majukumu ya kaunti,” alisema mwezi jana akiwa kwenye mazishi katika Kaunti ya Siaya.
Lakini wabunge kama Mabw Peter Nabulindo (Matungu) na Peter Salasya (Mumias Mashariki), wamemkosoa vikali Bw Odinga, wakisema anapotosha ukweli na kuhatarisha maendeleo mashinani.
“Tumemuomba kiongozi wetu aachane na mjadala huu. Hii sio siasa; ni kuhusu maisha ya watu wetu. Wacha tuzungumze na magavana tupate mwafaka,” alisema Bw Nabulindo.
Bw Salasya naye alisema serikali za kaunti zimeonyesha kushindwa kutekeleza hata majukumu rahisi kama ujenzi wa madarasa ya chekechea.
“Watoto wengi bado wanakaa chini na kusomea chini ya miti. Kama kaunti zinashindwa na hili, vipi zitashughulikia miradi mikubwa?” alihoji.
Katika mikutano ya kukusanya maoni kutoka umma kuhusu hatma ya NG-CDF, wakazi wa maeneo kama Mumias waliunga mkono marekebisho ya Katiba kupitia Mswada wa Marekebisho ya Katiba2025 unaolenga kukita NG-CDF ndani ya Katiba.
Walisema NG-CDF ni “hazina ya wananchi” inayogusa maisha ya watu moja kwa moja. Mbunge Johnson Naicca alisisitiza kuwa, NG-CDF imebadilisha maisha ya wengi, hasa wanafunzi kutoka familia maskini.
Alitaka fedha zinazotengewa NG-CDF ziongezwe kutoka asilimia 2.5 hadi 5.
Katika maeneo bunge ya Laikipia Kaskazini na Laikipia Mashariki, wananchi walizungumza kwa kauli moja wakitetea fedha za maendeleo kupitia ofisi za wabunge, wakisema mfumo huo unahakikisha usawa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo mashinani.
Mbunge wa Laikipia Kaskazini Sarah Korere aliunga sheria mpya ya hazina hiyo naye Mbunge wa Tetu Geoffrey Wandeto aliwahimiza wananchi kuunga mkono NG-CDF akisema inabeba uzito mkubwa katika maendeleo ya mashinani.
“Wale wanaopinga hazina hii wanapaswa kuja wasikie wananchi. Mahakama zetu hasa, zinapaswa kuwauliza wananchi ikiwa wanataka NG-CDF iondolewe. Tunataka kuweka Hazina hii ndani ya Katiba ili ilindwe kwa kuwa ina manufaa ya kweli mashinani,” alisema.
Mbunge wa Runyenjes, Eric Muchangi alimshambulia Bw Odinga kwa kupinga hazina hiyo.
“Hii ni usaliti wa kushtua kwa Wakenya wa kawaida. Hauwezi kukaa Nairobi na kuwaambia wazazi maskini kuwa basari haina maana. NG-CDF si tu hazina — ni msingi wa matumaini,” alisema.
Mbunge wa Manyatta, Gitonga Mukunji, alishangaa ni kwa nini hazina hiyo ambayo imeinua elimu moja kwa moja katika shule nyingi inapingwa.
Naye Mbunge wa Kibwezi Magharibi, Mwengi Mutuse, alimpuuza Bw Odinga akisema manufaa ya hazina hiyo kwa raia maskini hayawezi kuingizwa siasa.