Jamvi La Siasa

Ushindi bomba wa Gachagua kortini

Na  SAM KIPLAGAT May 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua alipata ushindi Ijumaa baada ya Mahakama ya Rufaa kuamua kwamba, Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu hakuwa na mamlaka ya kuteua jopo la majaji kusikiliza kesi zilizopinga kuondolewa kwake madarakani.

Majaji Daniel Musinga, Mumbi Ngugi na Francis Tuiyott walisema jukumu la kuteua jopo la majaji limetwikwa Jaji Mkuu na Katiba, na kwamba kuwapangia majaji kazi si mojawapo ya majukumu ya kiutawala ambayo Jaji Mkuu anaweza kumpa Naibu Jaji Mkuu.

“Inapaswa kukumbukwa kuwa jukumu la kuteua jopo la majaji limetwikwa Jaji Mkuu kwa mujibu wa Katiba, na hatuoni kuwa ni mojawapo ya kazi za kiutawala ambazo Jaji Mkuu anaweza kumpa au kuhamishia kwa Naibu Jaji Mkuu kwa mujibu wa kifungu cha 5(2) cha Sheria ya Huduma za Mahakama (JSA),” walisema majaji hao.

Majaji hao walisema kifungu cha 5(4) cha JSA kinaweka wazi hali tatu pekee ambazo zinaruhusu Naibu Jaji Mkuu kuchukua nafasi ya Jaji Mkuu — ikiwa ni kuondolewa, kujiuzulu au kifo cha Jaji Mkuu.

Uamuzi huo ulipokelewa kwa furaha na mawakili wa Bw Gachagua wakisema unafuta maamuzi yoyote yaliyotolewa na jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu waliojumuisha majaji Eric Ogolla, Anthony Mrima na Freda Mugambi.

Wakili Ndegwa Njiru alisema kwa maoni yake, Bw Gachagua bado ni Naibu Rais kwa sababu Mahakama ya Rufaa imebaini kuwa naibu jaji mkuu hakuwa na mamlaka ya kuwateua majaji.

“Jopo hilo halikuundwa kisheria kulingana na uamuzi wa Mahakama ya Rufaa. Kwa hivyo, lolote lililotolewa na jopo hilo ni batili tangu mwanzo. Mahakama haikufaa kufuta agizo lililositisha kuapishwa kwa Kithure Kindiki kama Naibu Rais,” alisema.

Bw Andrew Muge alikubaliana naye akisema uamuzi huo unafuta maamuzi yote yaliyotolewa na mahakama hiyo.Hata hivyo, Mshauri Mkuu wa Serikali, Emmanuel Bitta, alipuuzilia mbali madai hayo akisema majaji wa Mahakama ya Rufaa walikataa kufuta maagizo yaliyotolewa na Mahakama Kuu.

“Ombi la kufuta agizo hilo lilikataliwa na mahakama,” alisema.Bw Gachagua, kupitia wakili Paul Muite, alikuwa amepinga uamuzi wa Mahakama Kuu uliosema kuwa Naibu Jaji Mkuu alikuwa na mamlaka ya kuteua jopo la majaji.

Majaji hao watatu wa Mahakama Kuu walikuwa wameamua kuwa jukumu la Jaji Mkuu chini ya Ibara ya 165(4) ya Katiba — kuhusu uteuzi wa majaji kushughulikia masuala mazito ya kikatiba — ni kazi ya kiutawala na kwamba DCJ anaweza kuwateua majaji anapotekeleza majukumu ya kikatiba kwa niaba ya Jaji Mkuu.

Jopo hilo lilisema jukumu la kikatiba la Jaji Mkuu ni la kiutawala na Naibu Jaji Mkuu anaweza kulitekeleza pale ambapo Jaji Mkuu hayupo, ili kuhakikisha kuwa majukumu ya kikatiba yanaendelea bila kukwama.

“Kwa mtazamo wetu, na kwa kuzingatia dhana ya mwendelezo wa uongozi, waandalizi wa Katiba yetu walilenga kuhakikisha utekelezaji wa majukumu na Katiba haviingiliwi,” walisema majaji hao.

Hata hivyo, Mahakama ya Rufaa haikukubaliana nao ikisema hakuna ushahidi kuwa Naibu Jaji Mkuu alikuwa akikaimu kama Jaji Mkuu, wala kuwa kulikuwa na hali za kipekee zilizomruhusu Jaji Mwilu kutekeleza jukumu hilo lililowekwa kikatiba kwa Jaji Mkuu.

“Sheria ya Huduma za Mahakama inatambua hali tatu ambapo Naibu Jaji Mkuu anaweza kuwa kaimu Jaji Mkuu: kuondolewa, kujiuzulu au kifo cha Jaji Mkuu.

Hatuna shaka kuwa Naibu Jaji Mkuu, anapokuwa akikaimu ndani ya maana ya kifungu cha 5(4), anaweza kutekeleza jukumu hilo la kikatiba chini ya Ibara ya 165(4),” walisema majaji.

Majaji hao walikubali ombi moja tu kati ya yale yaliyowasilishwa na Bw Gachagua kwa kufuta agizo la Naibu Jaji Mkuu Oktoba 18, 2024 ambalo aliwateua majaji watatu kusikiliza tatu kati ya kesi kumi zilizopinga kuondolewa kwake.