Ruto azongwa na shida moja baada ya nyingine kwenye utawala wake
RAIS William Ruto anaonekana kama kiongozi aliyezingirwa na changamoto nyingi tangu alipoingia mamlakani mnamo Septemba 22, 2022.
Tangu alipomrithi Uhuru Kenyatta, amekumbwa na wakati mgumu kwa kupoteza kesi kadhaa mahakamani, maasi ya vijana wa kizazi cha sasa Gen Z, upinzani kutoka kwa makundi ya kijamii na katika uwanja wa siasa na hata ndani ya serikali yake.
Rais Ruto anapodhani kuwa ameshinda shida moja, nyingine huchipuza na kutikisa misingi dhoofu ya utawala wake.
Kwa mfano, hatua ya Rais huyo kuteua mwenyekiti na makamishina sita wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC) imelakiwa kwa pingamizi badala ya furaha.
Hii ni licha ya kwamba taifa hili liko katika hatari ya kukumbwa na mzozo wa kikatiba ikizingatiwa kuwa tume hiyo imesalia bila makamishina kwa zaidi ya miaka miwili tangu Januari 17, 2023.
Tangu wakati huo, maeneo 19 wakilishi yamesalia wazi kwa sababu IEBC haiwezi kuendesha chaguzi ndogo bila kuwepo kwa angalau kamamishna watu.
Katika hatua iliyowashangaza wengine, Rais Ruto aliamua kuwaweka kando watu wenye majina makubwa kama aliyekuwa msajili wa Idara ya Mahakama Anne Amadi na aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati ya Utekelezaji wa Katiba (CIC) Charles Nyachae na kumteua mwanasheria Erastus Ethekon kuwa mwenyekiti wa IEBC.
Bw Ethekon aliwahi kuhudumu kama Mkuu wa Idara ya Sheria katika Serikali ya Kaunti ya Turkana.
Dkt Ruto pia aliwateua Msajili wa Vyama vya Kisiasa Anne Nderitu, Moses Mukhwana, Mary Karen Sorobit, Hassan Noor Hassan, Francis Odhiambo Oduol na Fahima Araphat Abdallah kuwa makamishna wa IEBC.
Hata hivyo, Kundi la Kuangalia Uchaguzi (Elog) sasa linataka ripoti kamili ya shughuli ya usaili wa watu walioshindania nyadhifa hizo ichapishwe.
Kundi hilo lilisema kando na ripoti hiyo kuwasilishwa kwa Rais Ruto ilipaswa pia kutolewa kwa umma.
Kulingana na kundi hilo la kutetea kuendeshwa kwa chaguzi kwa uwazi na kisheria, ripoti hiyo isipotelewa baadhi ya watu watashuku kuwa huenda haki haikuzinatiwa wakati wa uteuzi wa watu hao.
“Kwa hivyo, tunataka ripoti kamili ya shughuli za uteuzi itolewe. Uwazi na uwajibikaji ni muhimu katika utawala na hivyo kutotolewa kwa ripoti hii kutaibua hofu kwamba haki, maadili na sheria hazikuzingatiwa wakati wa uteuzi huo,” ikasema taarifa ya Elog iliyotolewa Alhamisi.
Wanasiasa wa upinzani wakiongozi wa kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka na Eugen Wamalwa pia walihojia uteuzi huo wakisema mashauriano hayakufanywa.
Madai yameibuliwa kuwa baadhi ya walioteuliwa ni wandani wa Rais Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga; wawili hao wakiendeleza ukuruba chini ya serikali jumuishi.