Makala

Daktari ambaye havalii viatu, na amezuru mataifa mengi akitembea mguu chuma

Na FRIDAH OKACHI May 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

DAKTARI Hamisi Kote Ali kutoka eneo la Kasarani Kaunti ya Nairobi, anazuru mataifa mbalimbali bila kuvalia viatu.

Bw Kote anaeleza sababu ya kutembea miguu chuma kwa muda wa miaka sita ni kutokana na utafiti aliofanya akiwa chuo kikuu nchini Italia, kuwa kutembea miguu chuma kunachangia afya bora kwa mifupa ya binadamu.

“Taaluma yangu ni ya udaktari kuhusu mifupa na viungo vya mwili…Nilipojiunga na chuo hicho, wale wazungu wasomi wenza walitaka kufahamu mbona Wakenya hupenda kukimbia bila viatu?” alihoji Bw Kote.

“Ulikuwa ni mjadala mkubwa kwenye darasa langu mwaka 2006,” aliongeza Kote.

Mjadala huo ulimpa wazo la kuanza kutembea mguu chuma, japo akianza kutumia viatu vyepesi vinavyoitwa five fingers. Alisema viatu hivyo vilimpa umbo la mguu chuma kutokana na uwepesi wake.

Kutembea mguu chuma alianza rasmi mwaka wa 2019. Wakati huo, alikuwa na nia ya kutafuta njia ya kusaidia mwili wake kujenga kinga zaidi.

Bw Kote wakati wa mahojiano na Taifa Leo, Kasarani, Nairobi, Mei 1, 2025. Picha|Fridah Okachi

“Nilipatwa na shida kwenye mguu wangu. Kulikuwa na mgwaruzo wa kiatu, unaoitwa Cone. Mgwaruzo huo ambao ulitokana na kufinywa na kiatu ulinipea uchungu kwenye sehemu yangu ya mgongo. Nilitafuta tiba mbalimbali lakini maumivu hayakupungua hadi pale niliamua kutembea mguu,” alidokeza Bw Kote.

Utulivu wa maumivu hayo, ulimpa uamuzi wa kupeana viatu vyake kwa marafiki pamoja jamii yake. Kupeana vyatu hivyo, ilikuwa kutoa fursa ya njia ya kutembea mguu chuma kwa muda mrefu.

“Maumivu yote yaliniishia. Mwezi wa kwanza, mgongo uliacha kuniuma, nikaona kuwa kulala pia nalala vizuri.”

Bw Kote alianza kutoa mafunzo kwa wagonjwa wake kuwa na mazoea ya kutembea mguu chuma, ili kustawisha hali yao ya afya.

Alieleza kuvalia kwa viatu kuna manufaa mawili kwa binadamu ikiwa ni urembo na kuzuia ajali. Alisisitiza kuwa asimilia 90 ya kuvalia viatu husababisha ugonjwa.

“Leo hii, ukimaliza kazi na uende nyumbani, jambo la kwanza utakalo fanya ni kuvua viatu. Mbona usipumzike navyo?” alihoji.

Huu ukiwa ni mwaka wake wa sita kutembea mguu chuma, Bw Kote alithibitishia Taifa Dijitali kuwa husafiri mataifa mbalimbali bila kiatu. Mataifa hayo yanakubaliana na hali yake.

Anoonyesha Taifa Dijitali picha kadhaa akiwa Dudai, Vegas na Amerika bila viatu.

 “Mwaka jana nilizuru Vegas mji wa Sin City bila viatu wakatu huo kulikuwa na joto la hali ya juu. Kisha nikazuru Dubai, nilikuwa na dhana kuwa huenda ikabambuka. Lakini haikuwa hivyo, kisha nikaelekea Saudi nikarejea nyumbani Kenya ikiwa sawa.”

Ili kuepuka ajali kwenye miguu yake, Daktari Kote humakinika anapotembea kwa kuhakikisha kuna usambamba anapotazama na anapokanyaga ardhi.

Miguu ya Bw Kote ambayo havalii viatu, Kasarani, Nairobi, Mei 1, 2025. Picha|Fridah Okachi

“Macho yangu na miguu yangu imekuwa marafiki wa chanda na pete. Lazima niangalie sehemu ambayo mguu wangu utakanyaga. Ukivalia viatu, kwa uhakika utapuuza kujua unafaa kukanyaga wapi,” alieleza Dkt Kote.

Mwanzoni jamii ilimchukulia kuwa huenda alipatwa na matatizo wa akili, wengine wakimtazamia kuwa anatumia dawa za kulevya. Hata hivyo, alisema kutembea bila viatu hatafuti umaarufu wowote.

“Sitembei bila viatu kupata umaarufu hapana. Natembea kuimarisha afya yangu. Kando na hilo nataka kusaidi yule ambaye angependa kuishi muda mrefu duniani, mwili wake uweze kumsaidia kadri umri unavyoogezeka. Magojwa ya mifupa kwa asilimia kubwa huambatana na miguu.”

Kulingana naye, umuhimu wa kutembea bila viatu uhakikisha viungo vyote vya mwili kuwa kwenye sehemu sawa, jointi za mifupa mbalimbali kuwa kwa njia ambayo haiwezi kuathirika wakati unapofanya kazi.

Alisema kuwa baadhi ya watoto nchini kuwa na miguu isiyokuwa na upinde (Flat foot) hutokana na wazazi wengi kuwa kuwavalisha watoto viatu

Alihimiza jamii kutumia muda wa dakika ishirini pekee ili kuimarisha afya yao ya mwili.

“Unapovalia viatu kwa muda mrefu unachangia shepu ya mguu kupotea. Kuna zile misuli hutoka kwenye nafasi yake na kufanya miguu ya binadamu kuwa na ulegevu fulani. Vile vimisuli vidogovidogo vinafanya sehemu za mwili kama vile magoti, mgongo kuwa na udhaifu fulani na kusababisha mwili kutoka kwenye nafasi yake na kuanza kushikana.

Kwenye kituoa cha Afya cha Human Garage, wafanyakazi wake wanamuiga kwa kukosa kuvalia viatu. Bw Mwaura Muriithi, sasa amekamilisha miaka mitatu kwa kutembea miguu chuma.

Mwanzoni, Bw Muriithi alifahamu kuwa kutembea kwa miguu chuma kunahusishwa na ufukara na kuona kuwa wale ambao hufuata mbinu hiyo hawakuwa wanaelewa wanachofanya.

“Niliona manufaa mbalimbali ambayo yalinivutia kujiunga na kundi hilo la kutembea miguu chuma. Watu wengi hulalamika kuwa na maumivu kwenye mabega na miguu bila kufahamu kuwa ni viatu vinavyowaumiza,” alieleza Bw Muriithi.

Bw Muriithi ambaye anaishi na ulemavu wa kuona alisema kwa miaka hiyo mitatu sasa amejifunza kutembea bila kutatizika. Pia, mbinu anayotembea humwepushia kupata ajali kazini na nyumbani.