Mafuriko yahamisha mamia ya wakazi Nyamasaria, Kapuothe, Kisumu
MAMIA ya familia zinazoishi Kapuothe na Nyamasaria katika Kaunti ya Kisumu wikendi walilazimika kukesha kwenye baridi baada ya mvua kubwa kusababisha mafuriko eneo hilo.
Mvua hiyo ilisababisha Mto Auji kuvunja kingo zake na maji kujaza nyumba na mashamba ya watu ambayo yapo nyanda za chini.
Kati ya maeneo yaliyoathirika vibaya ni Butter Toast, Nile Resort na sehemu ya Mowlem.
Katika eneo la Nyamasaria, wakazi walihangaika na kuishi kwa hofu. Joan Akinyi, mama wa watoto wawili alisema hakuamini nyumba yake ilivyojaa maji.

“Nilikuwa naandalia familia yangu chajio na nikateleza kwenye sakafu. Kwa mashangao, nilipata maji yamejaa na hata sikumaliza kupika,
“Pamoja na watoto wangu wawili tulilazimika kusaka msaada kwa rafiki yetu mtaa wa Lolwe,” akasema.
Katika eneo la Kapuothe, Nyalenda, wamiliki wa biashara ndogo ndogo kama Guil Obange waliathirika vibaya. Bw Obange, 30 ambaye anafanya kazi kwenye kinyozi alikuwa akiyaondoa maji yaliyokuwa yamejaa duka lake.
“Duka limejaa maji ilhali hapa ndiyo nategemea. Itabidi sasa nifanye kazi chini ya mti nikisubiri maji yapunge na leo nimeumia kwa sababu nimetengeneza Sh50 pekeee,” akasema.
Katika eneo la burudani la Dondez, jijini Kisumu, wengi walijipata wakiyachota maji badala ya kustarehe. Wafanyakazi na waliofika kujiburudisha walijipata wote wakichota maji hayo.
Miundomsingi jijini Kisumu iliathirika, miti ikianguka mtaa wa Milimani huku umeme ukipotea maeneo mbalimbali jijini Kisumu. Mlingoti wa umeme ulianguka karibu na uwanja wa ndege wa Kisumu kutokana na upepo mkali.
Mafuriko hayo yamesababisha wakazi waitake serikali ya kaunti ya Kisumu ihakikishe kuwa mabomba ya kupitisha maji yapo katika hali sawa.
“Kisumu ina mabomba mabovu ya kupitisha majitaka. Ikinyesha jiji hili hufanana na Kabonyo Kanyagwal ambayo inafahamika kwa mafuriko,” akasema Job Okinyi.
Wakazi sasa wametoa wito kwa maafisa wa kaunti watathmini uharibifu ambao ulitokea na kuzisaidia familia zilizoathirika.