Habari

IEBC mpya kuanza kazi Juni ikisubiriwa kuandaa chaguzi ndogo, saini za kutimua wabunge

Na CHARLES WASONGA May 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MWENYEKITI mteule wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Erastus Ethekon Edung na makamishna sita wa tume hiyo wataingia afisini mwanzoni mwa mwezi Juni mwaka huu endapo bunge la kitaifa litaidhinisba uteuzi wao.

Hii ni baada ya Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula kuagiza Kamati ya Bunge kuhusu Sheria na Masuala ya Kikatiba (JLAC) kuanzisha taratibu za kuwapiga msasa saba hao na kuwasilisha ripoti yake bungeni mnamo Mei 27, 2025.

“Ikizingatiwa kuwa shughuli ya kuundwa upya kwa IEBC ni ya dharura, kamati hiyo inatarajiwa kuanza mara moja shughuli ya upigaji msasa na kuwasilisha ripoti yake siku ambayo Bunge la Kitaifa litarejelea vikao vyake mnamo Jumanne, Mei 27, 2025. Hii inaliwezesha bunge kuchambua ripoti hiyo ndani ya wakati uliowekwa kisheria,” akasema Jumamosi alipowasilisha majina ya wateule hao kwa JLAC.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Sheria ya IEBC ya 2024, kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Tharaka George Murugara inayo muda wa siku 28 kuendesha vikao vya kuwapiga msasa Bw Edung na wenzake kisha kuwasilisha ripoti katika bunge la kitaifa.

Aidha, bunge hilo limepewa muda wa siku saba kuchambua ripoti hiyo kwa ajili ya kukubaliana na mapendekezo yake au kuyakataa.

Agizo la Spika Wetang’ula kwa kamati ya JLAC linajiri siku mbili baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Rais William Ruto Ijumaa wiki jana na siku moja baada ya kumpendekeza Bw Edung kuwa mwenyekiti wa IEBC.

Dkt Ruto pia aliwapendekeza watu wengine sita kuwa makamishna wa tume hiyo.

Wao ni; Msajili wa Vyama vya Kisiasa Anne Ndung’u, aliyekuwa mkuu wa mkoa Noor Hassan Noor na aliyekuwa Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Kifundi Nchini (TUK) Francis Oduol.

Wengine ni wakili mtajika Moses Alutalala Mukhwana, Bi Mary Karen Sorobit na Bw Fahima Araphat Abdalla.

Rais Ruto alipendekeza majina ya saba hao kwa kuzingatia Kipengele cha 250 (2) (c) cha Katiba na Sehemu ya 5 ya Sheria ya IEBC ya 2024 na kufuatia mapendekezo ya Jopo la Kuteua Mwenyekiti na Makamishna wa Tume hiyo.

Kulingana na Sheria ya Bunge kuhusu Uteuzi hatua ya kwanza ni kwa Karani wa Bunge la Kitaifa Samuel Njoroge kuweka tangazo magazetini kutaka umma kutuma memoranda au hatikiapo za kupinga uteuzi wa watu hao saba waliopendekezwa kuongoza IEBC ndani ya muda wa siku saba.

Baadaye, JLAC itaandaa vikao vya kuwapiga msasa Bw Edung na wenzake kubaini ufaafu wao kutekeleza majukumu ya nyadhifa hizo kisha kuandaa ripoti yao itakayowasilishwa bunge.

Wabunge watajadili ripoti hiyo kisha kuamua, kupitia upigaji kura, kuipinga au kuiunga mkono.