Habari za Kaunti

Viongozi walalama uuzaji pombe haramu ukirejea Mlima Kenya

Na DAVID MUCHUI, GEORGE MUNENE May 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

VIONGOZI na wakazi katika kaunti kadhaa za eneo la Mlima Kenya wamekashifu kurejea kwa biashara ya kuuza pombe haramu katika eneo hilo, huku polisi wakilaumiwa kwa kuhusika katika biashara hiyo.

Viongozi wakiwemo machifu pia wamelalamikia kunyanyaswa na washukiwa wanaowakamata lakini wanaishia kuachiliwa na mahakama baada ya kulipa faini ndogo au dhamana ya pesa taslimu.

Wiki iliyopita, watu watatu walilazwa hospitalini baada ya kunywa pombe inayoshukiwa kuwa na kemikali za sumu katika eneo la Kangai kaunti ya Kirinyaga.

Watatu hao walianza kulalamika kuhusu maumivu ya tumbo na kizunguzungu walipokunywa pombe hiyo katika baa moja iliyoko soko la Kangai Kaunti Ndogo ya Mwea Magharibi.

Muda mfupi baadaye, walianguka na kukimbizwa katika vituo mbalimbali vya afya eneo hilo.

Wawili kati ya waathiriwa walilazwa katika hospitali ya rufaa ya Kerugoya huku wa tatu akipelekwa katika Kituo cha afya cha Njegas.

Wakiongozwa na diwani wa eneo hilo, Bw Wambu Njiru, wakazi waliandamana wakisema suala hilo linafaa kuchunguzwa kwa kina ili kubaini chanzo cha pombe hiyo yenye sumu.

“Tunataka kujua wanaotaka kuwaua watu wetu tena katika eneo hili,” akasema Bw Njiru.

Wakazi waliwasuta polisi na maafisa wa kaunti ya Kirinyaga, wakiwashutumu kwa kulala kazini.

“Pombe haramu zinauzwa katika baa na polisi pamoja na maafisa wa kaunti hawafanyi lolote. Hii ni tishio kwa maisha ya binadamu,” mmoja wa wakazi hao Bw Dennis Murimi alisema.

Mkuu wa polisi katika Kaunti Ndogo ya Kirinyaga Magharibi, Bi Millicent Mburu, alisema kisa hicho kinachunguzwa ili kubaini ukweli.

Mnamo Februari 5, 2024, kisa cha kutatanisha kilitokea katika eneo hilo hilo.

Takriban watu 17 walifariki baada ya kunywa pombe ya sumu iliyokuwa ikiuzwa katika baa iliyoanzishwa eneo hilo huku wakazi wakisema tukio la hivi majuzi linafaa kushughulikiwa kwa haraka.

“Hatutaki marudio ya tukio hili ambalo lilituacha na mshangao. Serikali inafaa kuingilia kati na kukomesha biashara hii haramu,” alisema Bi Serah Njeri, mkazi.