Habari za Kitaifa

Watetezi wa haki wamrukia Ruto kwa kudai hakuna utekaji Kenya

Na BENSON MATHEKA May 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KAULI ya Rais William Ruto kwamba watu wote waliotekwa nyara na kutoweshwa kwa nguvu nchini waliachiliwa kuungana na familia zao imezua hisia kali kutoka kwa viongozi na watetezi wa haki za binadamu wakimkosoa kwa kukiri kwamba serikali yake ilihusika na uovu huo.

Jaji Mkuu mstaafu David Maraga alishangazwa na kauli ya rais na kutaka kufanyika kwa uchunguzi wa kina na wahusika kufikishwa mahakamani huku kiongozi wa chama cha Peoples Liberation Party Martha Karua akitaja kauli ya rais Jumatatu kama ‘kukubali bila kujali’ suala la utekaji nyara.

Katika taarifa tofauti, wawili hao walisema kuwa watu wengi walitekwa nyara nchini Kenya mwaka jana, na kwamba Ruto alitoa kauli zake licha ya mzigo wa kihisia unaoandama familia za waathiriwa na wapendwa wao.

Maraga alikosoa kauli ya Ruto kwamba hakuna tena visa vya utekaji nyara vinavyoendelea, na ahadi yake ya kumaliza kabisa tatizo hilo. Alitoa mfano wa Brian Odhiambo, ambaye alitoweka kwa njia ya kutatanisha akiwa mikononi mwa maafisa wa Huduma ya Wanyamapori Kenya (KWS) na hajawi kupatikana.

“Ni jambo lisilokubalika kusikia Rais akidai, bila hata kuomba msamaha kwa waathiriwa, wazazi, na familia, kwamba hakuna visa vya kutoweshwa kwa lazima au mauaji ya kiholela, na kwamba kuna mifumo ya uwajibikaji inayoendelea,” alisema Maraga.

“Mama ya Brian Odhiambo bado anatafuta mwanawe aliyechukuliwa miezi minne iliyopita. Kuna vilio vingine vingi vya kutafuta haki, kama tulivyoona katika ombi lililowasilishwa Siku ya Akina Mama na wazazi wa vijana waliouawa wakati wa maandamano ya Juni 2024.”

Maraga alisisitiza umuhimu wa kuheshimu Katiba inayotoa utawala wa sheria unaoheshimu haki za binadamu.

Jaji Mkuu huyo wa zamani pia alishinikiza serikali kuheshimu mkataba wa kimataifa wa kulinda watu wote dhidi ya kutoweshwa kwa nguvu, na kupitisha sheria ya kitaifa ya kuzuia na kufanya hilo kuwa kosa la jinai.

Alisema hili linatokana na uanachama wa Kenya katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa.

Katika taarifa yake, Karua alimshinikiza Ruto kukiri waziwazi jukumu la maafisa wa usalama katika utekaji nyara na kutoweshwa kwa nguvu. Alitaka pia maafisa waliorekodiwa kwenye kamera, kama ilivyofichuliwa katika makala ya “Blood Parliament” ya BBC, kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Sasa kwa kuwa William Ruto amekiri kuwepo kwa utekaji nyara, anapaswa pia kukubali ukweli wa mauaji ya kiholela na kutoweshwa kwa nguvu, pamoja na kuhusika kwa maafisa wa usalama, na kuchukua hatua za kuhakikisha wote waliohusika, wakiwemo waliorekodiwa kwenye makala ya BBC, wanawajibika,” alisema.

Mnamo Jumatatu Rais Ruto alizua mjadala mkali baada ya kudai kuwa kila aliyetekwa ameunganishwa tena na familia yake. Aliahidi kuwa visa vya utekaji nyara, kutoweshwa kwa lazima, na mauaji vimekoma.

Mnamo Mei 7, mashirika 10 ya kutetea haki za binadamu Kenya yalitoa ripoti ambayo ilifichua ongezeko la visa vya mauaji ya kiholela na kutoweshwa kwa lazima iliyotaja visa 159 vilivyothibitishwa.

Kati ya hivyo:104 (asilimia 65) ni mauaji yaliyofanywa na polisi 55 (asilimia 35) ni visa vya kutoweshwa kwa lazima.