Ombi Jaji Mwilu afutwe kazi kwa kusababisha Gachagua kupokonywa kiti
NAIBU Jaji Mkuu Philomena Mwili anakabiliwa na tishio jingine la kuondolewa afisini kwa mienendo mibaya ya kuingilia mamlaka ya bosi wake, Jaji Mkuu Martha Koome.
Hii ni baada ya kuteua majaji kushughulikia kesi kuhusu kutimuliwa kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Hatua hiyo inajiri majuma mawili baada ya Bi Mwili, pamoja na majaji wengine sita wa Mahakama ya Juu, kupata afueni kuhusiana na pendekezo kwamba watimuliwe afisini.
Mahakama Kuu iliamua kuzuia Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) kuendelea na mchakato wa kuwaadhibu majaji hao kwa njia ya kutimuliwa kwao afisini, kufuatia malalamishi yaliyowasilishwa dhidi yao na aliyekuwa Rais wa Chama cha Mawakili Nchini (LSK) Nelson Havi na Waziri wa zamani Raphael Tuju.
Ombi jipya la kutimuliwa kwa Bi Mwilu liliwasilishwa kwa JSC jana.
Kulingana na ombi hilo, Naibu huyo wa Jaji Mkuu anatuhumiwa kukiuka Katiba na Kanuni ya Maadili na Utendakazi wa Maafisa wa Idara ya Mahakama ya 2020.
Limewasilishwa na mkazi mmoja wa Nairobi Bi Belinda Egesa.
Anadai Bi Mwilu alidhihirisha utepetevu kazini kwa kufasiri visivyo Kipengele cha 165 (4) cha Katiba kuhusu mamlaka ya Jaji Mkuu kuteua majaji wa kushughulikia kesi inayohusu ufasiri wa kina wa kisheria.
Ombi la Bi Egesa linatokana na uamuzi wa wiki jana wa Mahakama ya Rufaa kwamba, Naibu Jaji Mkuu alikiuka Katiba na kanuni za Idara ya Mahakama kwa kuteua majaji Erick Ogolla, Anthony Mrima na Fridah Mugambi kusikiza kesi iliyowasilishwa katika Mahakama Kuu ya Kerugoya ya kupinga kutimuliwa kwa Gachagua.
Kesi hiyo iliyowasilishwa na wakazi wawili wa Kirinyaga ilitaka kuzuia kuapishwa kwa Naibu Rais Kithure Kindiki kuchukua nafasi ya Bw Gachagua.