Habari

Hii hapa ndio sababu Wakenya wajakazi huishia kuteswa Saudi Arabia – Amnesty International

Na ELVIS ONDIEKI May 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAKENYA, hasa wanawake, wanaoajiriwa wajakazi nchini Saudi Arabia wanapoendelea kusimulia mateso wanayopitia, ripoti mpya ya Amnesty International imefichua mzizi wa janga hili ambao ni mfumo wa kafala.

Mfumo huu ambao unampa mwajiri mamlaka ya kuwa mlezi wa kisheria wa mfanyakazi, unafanana kwa karibu na biashara ya utumwa iliyoendeshwa kutoka Pwani ya Afrika Mashariki karne zilizopita.

Ripoti hiyo inaeleza mateso ya wanawake 72 Wakenya waliorejea nchini kati ya mwaka wa 2020 na 2024. Wengi wao walipitia madhila makubwa: kupigwa, kubakwa, kula mabaki au chakula kilichooza, kulazimishwa kulala kwenye vyumba vinavyofanana na magereza, na kunyimwa hata fursa ya kutumia simu au intaneti.

“Karibu wote walisema hawawezi kurudi Saudi Arabia kamwe, hata wakipewa fursa nyingine,” inaeleza ripoti hiyo.

Peace, mmoja wa waathiriwa, alisema alidanganywa kuwa angeenda kuhudumia familia ya watu watano. Alipofika, alikuta familia ya watu 14 na kazi yote ilikuwa yake.

Jamila alifanya kazi bila siku ya mapumziko kinyume na ilivyoandikwa kwenye mkataba wake kwa nusu ya mshahara aliotarajia. Muna, ambaye alidanganywa kuwa angeajiriwa kama mwalimu wa Kiingereza, alipewa kazi zote za nyumbani.

Lucia alipelekwa Saudia kama msaidizi wa kampuni lakini alihudumu kama mfanyakazi wa nyumbani katika nyumba nne tofauti bila kulipwa hata senti.

Mfano wa ukatili wa kutisha ulielezwa na Catherine, ambaye mwajiri wake alimwambia: “Nilikununua. Wewe ni mali yangu, lazima ufuate ninachosema.” Alipewa mabaki ya chakula au wakati mwingine hakupewa chochote. Alipojaribu kupika, chakula hicho kilitupwa kwenye pipa kwa madai ya ‘harufu mbaya’. Alilazimika kuishi kwa kula biskuti pekee.

Kafala ni mfumo unaoweka mfanyakazi wa kigeni chini ya usimamizi wa mwajiri wake kwa kila hatua kuanzia kuingia nchini Saudia, kupata visa, makazi, hata ruhusa ya kubadilisha kazi au kuondoka nchini. Mara nyingi, pasipoti ya mfanyakazi hushikiliwa na mwajiri, ikimwacha mfanyakazi bila uwezo wa kujinasua.

“Mfumo huu unawapa waajiri mamlaka makubwa mno kuhusu wafanyakazi na kuwaweka katika mazingira ya kuteseka, na kubaguliwa,” Amnesty inaeleza.

Kufikia sasa, wafanyakazi wote wa nyumbani nchini Saudi Arabia ni raia wa mataifa ya kigeni, wengi wao kutoka Afrika na Asia. Takriban Wakenya 200,000 wanaishi nchini humo – zaidi ya 150,000 wakiwa ni wafanyakazi wa nyumbani, kulingana na takwimu za serikali ya Kenya.

Ripoti hiyo inalinganisha kafala na ukoloni ulioendelezwa na Waingereza katika karne ya 20, ambapo mfumo huu ulianzishwa. Hadi leo, mfumo huu unapatikana pia katika mataifa mengine kama Qatar na Lebanon.

Ripoti inaangazia kuwa wanawake weusi, hasa kutoka Afrika, wako kwenye hatari kubwa ya kunyanyaswa kwa sababu ya mitazamo ya kibaguzi na kijinsia.

Amnesty International inataka kufutwa kwa mfumo wa kafala kikamilif, wafanyakazi wa nyumbani wajumuishwe kwenye sheria za kazi, waajiri wanaowanyanyasa waadhibiwe kisheria, Serikali ya Kenya itenge rasilmali kusaidia wafanyakazi walio katika hatari ughaibuni na serikali ya Kenya iangalie upya masharti ya uhamiaji na ajira nchi za Ghuba.

Kenya, ripoti inasema, imechochea uhamiaji wa vijana wake kwa matarajio ya kusaidia familia, lakini imeshindwa kutoa ulinzi madhubuti kwao wakiwa nje ya nchi.