Uchanganuzi: Sumu fiche katika Mswada wa Fedha ipo kwenye mabadiliko ya sheria za kodi
MPANGO wa serikali wa kuongeza mapato mwaka ujao kuanzia Julai—yaani Mswada wa Fedha wa 2025—umeelezwa kuwa unaoepuka hatua kali za ushuru kama zile za Mswada wa Fedha wa 2024 ulioondolewa kufuatia maandamano ya kitaifa yaliyosababisha vifo vya vijana kadhaa.
Hata hivyo, chini ya mwonekano huu wa mswada wa fedha wa wastani, kuna mabadiliko yenye uchungu ambayo huenda yakaathiri Wanjiku, wakiwemo wakulima, wagonjwa, wakopaji wa mikopo ya kidijitali, na wamiliki wa kwanza wa nyumba nafuu, kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali walizungumza na Taifa Leo.
Cha kutia wasiwasi zaidi ni jaribio lingine la Hazina ya Kitaifa kujaribu kukwepa matakwa ya kikatiba yanayoitaka serikali kupata kibali cha mahakama kabla ya kupata taarifa nyeti kutoka kwa walipa kodi.
Marekebisho makubwa zaidi katika Mswada wa Fedha 2025 ni mabadiliko katika Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), ambapo baadhi ya bidhaa zilizokuwa kwenye orodha ya msamaha wa VAT zimeondolewa.
VAT, inayotozwa kwa kiwango cha asilimia 16, hutozwa bidhaa na huduma zinazotumiwa kila siku na Wakenya.
Hata hivyo, bidhaa ghafi zinazotumika kutengeneza dawa na chakula cha mifugo; usafirishaji wa miwa kutoka mashambani hadi viwandani; simu zinazotengenezwa hapa nchini; baiskeli za umeme; pamoja na betri za jua zimekuwa kwenye orodha ya bidhaa hizo.
Hii ina maana kuwa wafanyabiashara hawatozi VAT ya asilimia 16 kwa watumiaji, lakini hulipa kwa Mamlaka ya Mapato (KRA) na baadaye huwa wanarudishiwa.
Hali hii inatarajiwa kuongeza gharama ya bidhaa muhimu na huduma kama chakula na huduma za afya, ambazo mabadiliko ya bei huathiri zaidi familia maskini.
Serikali ya Rais William Ruto inalenga kupunguza pesa ambazo serikali inapoteza kwa kutokusanya kodi fulani—na urejeshaji wa VAT kwa wazalishaji wa bidhaa.
Serikali ya Ruto inadai kuwa kurejesha VAT kumekuwa kukitumiwa vibaya, kwani baadhi ya wafanyabiashara hawapitishi faida hiyo kwa watumiaji.
Kwa kawaida, bidhaa na huduma chini ya miradi ya msaada wa kigeni au mkopo wa masharti nafuu huwa hazitozwi VAT.
Lakini kwa mujibu wa mabadiliko katika mswada huo, mafuta na vilainishi vitatozwa VAT ya asilimia 16, hali itakayoongeza gharama za miradi ya msaada.
Katika hatua nyingine ya kujidhuru kisera, serikali ya Kenya Kwanza inapendekeza kutoza VAT ya asilimia 16 kwa vifaa vya ujenzi wa nyumba nafuu—mradi mkuu wa serikali—jambo ambalo litaongeza gharama ya nyumba hizo.
Serikali pia inalenga sekta pana ya mikopo ya kidijitali, hasa ile inayotolewa na mashirika ya nje, kwa kupanua wigo wa ushuru unaotozwa kwenye huduma za kidijitali zinazotolewa na watu au mashirika yasiyo ya hapa nchini.
Mswada huo pia unafafanua “mtu asiye mkazi” kuwa ni mtu aliye nje ya Kenya.
Marekebisho hayo, kwa mujibu wa Dkt Lyla Latif Mkurugenzi Mkuu wa Lai’Latif & Co Advocates, yataongeza viwango vya riba ambavyo wakopaji wa mikopo ya kidijitali hulipa.
Mnamo 2024, takriban Wakenya 668,491 walikopa mikopo ya kidijitali kupitia apu walizopakua kwenye simu zao, ongezeko kutoka 583,263 mnamo 2021, kulingana na utafiti wa pamoja wa Benki Kuu ya Kenya na Shirika la Taifa la Takwimu (KNBS).
Hata hivyo, baadhi wanaona upanuzi huu kama njia ya kuweka usawa wa ushuru kwa kampuni za kidijitali za Kenya zilizokuwa zikiathirika.
“Hii inaunda uwanja wa ushindani ulio sawa kwa watoa huduma wa Kenya,” ilisema kampuni ya ukaguzi ya Grant Thornton kuhusu Mswada wa Fedha wa 2024.
Hazina ya Taifa pia inajaribu tena kupata ruhusa ya kisheria kuweza kufikia taarifa binafsi bila kibali cha mahakama, kama njia ya kupanua wigo wa ushuru kwa kufuatilia shughuli za kibiashara.
Wanapendekeza kubadilisha Sheria ya Taratibu za Ushuru ya 2024 kwa kufuta kifungu kinachozuia KRA kupata taarifa nyeti wakati wa kuunganisha mifumo yao na ya wafanyabiashara ili kupata taarifa kwa wakati halisi.
Hii imewafanya Wakenya wengi kuwa na wasiwasi kuhusu ukiukaji wa faragha.
Kwa sasa, sheria inaruhusu KRA kuunganisha mifumo yake na ya biashara, lakini inakataza kufikia “siri za kibiashara” na “taarifa za kibinafsi.”
Waziri wa Fedha John Mbadi anasisitiza kuwa sheria haijafafanua dhana hizo mbili, hivyo KRA haiwezi kupata taarifa yoyote muhimu.