Habari

Jinsi kesi ya mauaji iliyomhusisha Aisha Jumwa iliporomoka

Na BRIAN OCHARO May 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KESI ya mauaji iliyokuwa imemhusisha aliyekuwa Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, imetamatika baada ya msaidizi wake wa zamani, Bw Geoffrey Otieno Okuto, kuondolewa mashtaka.

Bw Okuto alishtakiwa kwa mauaji ya mfuasi wa chama cha ODM, Jola Ngumbano, wakati wa uchaguzi mdogo wa Wadi ya Ganda, Malindi mwaka wa 2019.

Awali, Bi Jumwa alikuwa mshtakiwa-mwenza lakini akaondolewa punde baada ya kuteuliwa waziri na Rais William Ruto.

Upande wa mashtaka uliambia mahakama kuwa baada ya kupitia ushahidi, ilibainika kwamba Bi Jumwa hakuhusika na mauaji ya Bw Ngumbao.

Mahakama Kuu ilimuachilia huru Bw Okuto mnamo Jumatano baada ya kuchambua ushahidi wa mashahidi 12, ukijumuisha ripoti ya uchunguzi wa kisayansi wa bunduki iliyoshukiwa kutumika katika mauaji hayo.

Jaji wa Mahakama Kuu Wendy Micheni, alisema kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kuwasilisha ushahidi wa kuthibitisha Bw Okuto ndiye aliyefyatua risasi iliyomuua Ngumbao.

“Upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kesi ya mauaji dhidi ya mshtakiwa bila shaka lolote. Kwa hivyo, mshtakiwa anaachiliwa huru kuhusu kosa la mauaji,” alisema jaji huyo.

Jaji Micheni alisema kati ya mashahidi 12, ni shahidi mmoja pekee aliyedai kumuona Bw Okuto akifyatua risasi katika boma la mjomba wa marehemu, Bw Reuben Katana, ambako ODM ilikuwa ikifanya mafunzo kwa maafisa wa uchaguzi mdogo.

Hata hivyo, jaji alitupilia mbali ushahidi huo akisema haungeaminika kwani shahidi alitoa maelezo yasiyowiana.

Kwa upande mmoja, shahidi alidai kumuona Bw Okuto akifyatua risasi mara mbili, lakini katika maelezo mengine akasema ilikuwa ni mara tatu.

Aidha, mahakama ilisema ripoti ya uchunguzi wa bunduki na maganda ya risasi yaliyopatikana katika eneo la tukio na kutoka kwa Bw Okuto, haikuthibitisha ni bunduki ipi iliyofyatua risasi iliyomuua marehemu.

Mashahidi kadhaa, wakiwemo polisi, waliiambia mahakama kuwa vurugu na milio ya risasi ilianza baada ya aliyekuwa Waziri wa Jinsia, Jumwa kuvamia mkutano huo.

Katika utetezi wake, Bw Okuto alisimulia jinsi alivyomshawishi Bi Jumwa asivuruge mkutano huo lakini hakuweza kumzuia.

Alikiri kufyatua risasi hewani katika jitihada za kumwokoa bosi wake, ambaye aliingia moja kwa moja katika umati wenye hasira.

“Nilipokuwa nikijaribu kumwokoa, milio ya risasi ilianza kusikika. Maafisa wa polisi waliokuwepo pia walifyatua risasi hewani kuwatawanya vijana waliokuwa wakileta vurugu,” alieleza alipokuwa akiongozwa na wakili wake, Jared Magolo.

Bw Okuto alisema alikuwa na bastola aina ya Ceska iliyokuwa na risasi karibu 14, lakini akasisitiza kuwa alipiga risasi hewani na kuwa risasi ya bunduki yake haikumpata wala kuua marehemu.