Maradhi yanavyoendelea kusambaa Afrika kutokana na habari feki, ufadhili duni
HUKU bara la Afrika likiendelea kukumbwa na janga la mkurupuko wa maradhi kila mara, Kituo cha kudhibiti na kuzuia maradhi barani Afrika (Africa CDC), kimetaja tatizo la kuenea kwa habari zisizo sahihi, vile vile zile za kupotosha kama baadhi ya vichocheo vikuu vya tatizo hili.
Kulingana na Kaimu Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Africa CDC, Dkt Raji Tajudeen, habari hizi zimeathiri kiwango cha imani na kusababisha wagonjwa wengi kukawia kwenda hospitalini, huku akionya kwamba mchanganyiko kati ya maradhi kama vile homa ya M-pox, surua na tetekuwanga, mara nyingi umesababisha utambuzi mbovu, suala linalosababisha waathiriwa kukawia kupokea matibabu na unyanyapaa.
“Watu wanapokosa kuelewa masuala wanayokumbana nayo, hofu hujaza pengo hilo, na haya ni mazingira tosha kwa habari potovu kuenea,” alisema Dkt Tajudeen katika uzinduzi wa warsha ya pili ya wanahabari iliyoandaliwa na Muungano wa Afrika, jijini Addis Ababa, Ethiopia, huku akizungumzia umuhimu wa wanahabari katika kukabiliana na shida hii.
“Kando na habari za aina hii kuwa changamoto kwa mawasiliano, ni tishio kwa afya ya umma, na ndiposa ni muhimu wa kuwepo kwa ushirikiano baina ya wanahabari na taasisi za kiafya katika makabiliano dhidi ya habari zisizo sahihi na za kupotosha,” asema.
Kinachoshangaza ni kwamba kuna baadhi ya vyombo vya habari ambavyo vimekuwa vikichangia tatizo hili kwa kujua au kutojua.
Kwa mfano, utafiti wa mwaka wa 2014 kwa jina Emerging Infectious Diseases uliodadisi habari kuhusu maradhi ya Ebola zilizochapishwa na vyombo vya habari nchini Amerika, ulionyesha kwamba asilimia 96 ya habari hizi zilieneza jumbe zisizo sahihi au potovu kuhusu maradhi haya huku asilimia 32 pekee ya habari hizi zikijumuisha taarifa sahihi za kisayansi kuhusiana na ugonjwa huu.
Kulingana na Profesa Yap Boum II, naibu msimamizi katika kikundi cha kutoa ushauri kuhusu maradhi ya homa ya M-pox katika kitengo cha Africa CDC, hapa barani, changamoto kuu inashuhudiwa katika mawasiliano ya masuala ya sayansi – kama vile data, misamiati ya kisayansi, na lugha.
Hasa Prof Boum anataja lugha kama kizingiti kikuu hasa ikizingatiwa kuwa tafiti nyingi za kisayansi huchapishwa kwa lugha ya Kiingereza, suala ambalo ni tatizo kuu kwa mataifa yasiyowasiliana kupitia lugha ya Kiingereza.
“Kwa mfano, hebu fikiria kufanya utafiti wa maradhi ya malaria nchini Gabon na kuuchapisha kwa kutumia lugha ya kitaalam ya Kingereza. Kuna uwezekano mkubwa kwamba huenda matokeo ya utafiti huu yasiwafikie watu wanaouhitaji zaidi,” Prof Boum alieleza, huku akiongeza kwamba hii ni mojawapo ya sababu sasa kituo cha Africa CDC kinapigania machapisho ya kisayansi kuwepo kwa lugha zote zinazotumika katika Muungano wa Afrika (AU).
Lakini kando na masuala ya kuenea kwa habari zisizo sahihi na potovu, Dkt Tajudeen pia anazungumzia changamoto za kimuundo ambazo zimeendelea kuongeza mzigo wa maradhi barani Afrika.
“Mifumo dhaifu ya afya, kutokuwepo kwa mifumo thabiti ya kuchunguza maradhi, bara hili kukosa uwezo wa kutengeneza bidhaa za kimatibabu, na ufadhili duni, ni baadhi ya changamoto ambazo bara hili linashuhudia,” aeleza.
Kulingana na mtaalamu huyu, vizingiti hivi haviathiri tu jitihada za kukabiliana na mkurupuko wa sasa wa maradhi kama vile homa za M-pox, Ebola, na Marburg, bali pia ni mazingira tosha kwa mkurupuko wa maradhi mengine katika siku za usoni.
Visa vya mkurupuko wa maradhi barani vimekuwa vikiongezeka katika miaka ya hivi majuzi. Kwa mfano, kulingana na Africa CDC, mwaka wa 2024 pekee, bara la Afrika lilinakili visa 213 vya mkurupuko wa maradhi.
Idadi hii ni ongezeko kutoka visa 152 vilivyoshuhudiwa mwaka wa 2022, ambapo takwimu hizi zinawakilisha ongezeko la asilimia 40.
Japo mataifa kama vile Rwanda na Uganda yalifanikiwa kudhibiti mkurupuko wa maradhi kama vile homa za Marburg na Ebola, wataalam wanahofia kwamba hali inaendelea kuwa mbaya zaidi.
“Afrika bado inasalia kuwa kiini cha mkurupuko wa maradhi ulimwenguni, licha ya hatua na mikakati mingi ambayo imewekwa tokea mkurupuko wa virusi vya COVID-19,” Dkt Tajudeen aonya.
Ili kukabilian ana janga hili, Africa CDC imezindua miradi kadha wa kadha, ikiwa ni pamoja na kikundi rasmi barani cha kufuatilia na kutoa ushauri kuhusiana na mkurupuko wa maradhi (Continental Surveillance Advisory Group). Kikundi hiki kinanuiwa kuimarisha uwezo wa bara hili kutabiri mkurupuko wa maradhi mapema.
Lakini pia Dkt Tajudeen asema kwamba kando na ala za kiteknolojia, muundo msingi thabiti wa kiafya katika bara hili lenye idadi ya watu zaidi ya bilioni 1.4 litahitaji ufadhili thabiti na wajibu kutoka kwa wanasiasa.
Mojawapo ya changamoto kuu za mifumo ya afya barani ni kutegemea ufadhili kutoka nje.
Mwaka wa 2022, mataifa yenye mapato ya chini kusini mwa jangwa la Sahara, yalitegemea msaada kutoka nje ili kufadhili asilimia 31 ya gharama za mifumo ya afya– kiwango ambacho ni ongezeko la asilimia 11, ikilinganishwa na ilivyokuwa mwaka wa 2003.
Haya yakijiri, matumizi ya kiafya kutoka kwa serikali za maeneo haya yalipungua kutoka asilimia 33 mwaka wa 2002 hadi tu asilimia 21.
Sasa wataalam wa masuala ya kiafya wana wasiwasi kwamba utegemeaji wa ufadhili wa nje kupindukia unaendelea kuhatarisha mifumo ya afya barani, hasa mazingira ya kisiasa ulimwenguni yanavyozidi kubadilika.
“Kwa mfano, kujiondoa kwa Amerika kutoka kwa Shirika la Afya Duniani na kupunguza misaada katika kitengo cha ustawi wa kimataifa cha USAID, kunatarajia kuongeza mapengo ya ufadhili hasa kwa mipango kama vile PEPFAR, unaotoa dawa za kukabiliana na makali ya virusi vya HIV barani,” aeleza Bi Katie Dain, mkurugenzi mkuu mtendaji wa shirika la kimataifa kuhusiana na maradhi yasiyoambukizwa (NCD Alliance).
Kutokana na haya, Dkt Tajudeen anatoa mwito kwa serikali za mataifa ya Afrika kuangazia umuhimu wa kuwekeza katika sekta ya afya.
Mwezi uliopita, kituo cha Africa CDC kilizindua ripoti ya ufadhili, huku kikirai mataifa wanachama kutimiza Azimio la Abuja, la kutenga asilimia 15 ya bajeti ya serikali zao kwa afya.
Kufikia sasa, ni nchi tatu pekee —Rwanda, Botswana na Cape Verde—ambazo zimetimiza lengo hili.
Lakini pia changamoto nyingine ni kuwa bara la Afrika limekuwa likitegemea sana uagizaji wa bidhaa za kimatibabu kutoka nje.
Janga la COVID-19 lilifichua jinsi bara hili linakumbwa na ugumu wa kufikia bidhaa za kimatibabu, kama vile chanjo na magwanda ya kujilinda.
Katika awamu za mapema za maradhi haya, baadhi ya mataifa ya Afrika yalikuwa yametoa chanjo kwa chini ya asillimia moja pekee ya raia wake, ilhali katika baadhi ya mataifa tajiri ya Ulaya, asilimia 90 ya watu walikuwa washapokea chanjo.
“Kwa sasa, bara la Afrika linaunda asilimia moja pekee ya chanjo inazotumia na hili sharti libadilike,” asema Dkt Tajudeen.
Hata hivyo, kulingana na kitengo cha Africa CDC, kwa sasa hatua nyingi zimechukuliwa kuhakikisha kwamba Afrika inaongeza viwango vya chanjo inayotengenezwa hapa.
“Tayari viwanda 25 vya kuzalisha chanjo barani vinafanya kazi huku mataifa manane yakiwa yamefikia kiwango cha tatu cha kuidhinishwa—idadi ambayo ni maradufu mambo yalivyokuwa mwaka uliopita,” aeleza Dkt Tajudeen.