Wandayi, Oburu waungana dhidi ya Orengo vita vya ubabe vikichacha
Huku kaunti nyingine katika ngome ya aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga ya Nyanza zikifurahia utulivu wa kisiasa uliojiri na ushirikiano mpya kati ya ODM na serikali ya Kenya Kwanza, Siaya imegeuka kuwa uwanja wa vita vya ubabe wa kisiasa.
Vita hivi vinahusisha gavana wa Siaya James Orengo, ambaye kwa muda mrefu ameheshimiwa kama gwiji wa siasa, dhidi ya Waziri wa Kawi Opiyo Wandayi na Seneta Oburu Oginga.
Mzozo kati ya Wandayi, Orengo na Oginga ulianza tangu kampeni za ugavana za mwaka 2017 na 2022. Kampeni za mwaka 2027 zimeanza mapema, huku mjadala mkubwa ukiwa ni kuhusu kuunga mkono au kupinga serikali Jumuishi
Mapambano ya ubabe wa kisiasa yalionekana mapema wiki hii pale madiwani walipokataa kuandamana na Dkt Oburu na viongozi wengine Ikulu gavana Orengo akiwa nje ya nchi kwa shughuli rasmi.
Ingawa madiwani walikanusha baadaye kuwa walikataa mwaliko wa kwenda Ikulu, Taifa Leo ilithibitisha kuwa mwaliko huo uliotumwa kupitia Dkt Oburu ulikataliwa kwa misingi kuwa ulikuwa wa ghafla na wengi wao hawakuwa wamejiandaa.
‘Hatukukataa mwaliko, tulikubaliana tuusongeze hadi wiki ijayo ili tupate muda wa kujiandaa vyema,’ alisema Edwin Otieno, kiongozi wa wengi katika Bunge la Kaunti ya Siaya.
Diwani mwingine aliambia Taifa Leo kwamba, ‘Tulikuwa kwenye mapumziko mafupi ujumbe ulipotumwa kupitia karani wa bunge kuwa kulikuwa na kikao muhimu sana ambacho madiwani walitakiwa kuhudhuria Jumatatu Mei 12, na ajenda ingejadiliwa bungeni.’
Diwani huyo, ambaye hakutaka kutajwa jina, aliongeza kuwa, ‘Tulipofika bungeni, hoja iliyokuwa mezani ilikuwa ni kuhusu ziara iliyopangwa ya kwenda Ikulu Jumatano Mei 14, iliyopangwa na Dkt Oburu. Kikao hicho kilikuwa kimehusisha pia wabunge waliokuwa na mkutano kama huo Nairobi Jumamosi Mei 10.’
Wengi wa madiwani walikataa mwaliko huo kwa sababu gavana Orengo alikuwa nje ya nchi, na alikuwa ameanza mipango ya ziara hiyo kabla ya kuondoka.
Kwa madiwani, kwenda Ikulu bila Bw Orengo, kungeonekana kama kutomheshimu kama kiongozi mkuu wa kaunti.
Bw Orengo, ambaye amekuwa akipinga vikali ushirikiano wa UDA na ODM, sasa ametajwa kama ‘adui wa maendeleo’ na Bw Wandayi.
Akihutubia waombolezaji wiki iliyopita katika kijiji cha Upanda, tarafa ya Ugunja, ambako watu tisa walifariki katika tukio linaloshukiwa kuwa la kuchoma nyumba kwa makusudi, Waziri Wandayi hakumsaza gavana kwa maneno.
“Gavana wa Kaunti ya Siaya sasa anapaswa kuacha uanaharakati na aelekeze nguvu katika kuwahudumia wananchi waliomchagua. Wabunge na hata maseneta ndio wanapaswa kushughulikia masuala anayojaribu kufanya,” alisema Waziri huyo.
Aliendelea: “Ukilinganisha na kaunti nyingine za eneo hili, Siaya ni fedheha; hakuna dawa kwenye vituo vya afya wala huduma zinazotolewa kwa kiwango kinachostahili. Hivyo basi, gavana anapaswa kufanya kazi aliyochaguliwa kufanya, siyo siasa za umaarufu.”
Awali, katika hafla nyingine, Seneta Oburu Oginga alimshambulia vikali gavana Orengo kwa kumtaka ajiuzulu na kujiondoa ODM ili aendelee na ukosoaji wake dhidi ya serikali jumuishi.
“Kwa nini anatutapikia akiwa bado ndani? Hawezi kutoka nje na kututapikia akiwa huko? Hilo litathibitisha yuko nje, si sahihi kuendeleza uanaharakati wake akiwa ndani ya chama cha chungwa,” alisema Dkt Odinga.
Kwa upande wake, Gavana Orengo ameendelea kukemea ushirikiano huo akisema nchi inaelekea vibaya, jambo ambalo halijapokelewa vyema na viongozi wengine.
Orengo alikosoa ODM kwa kuridhika haraka na uteuzi wa nafasi sita ilizotengewa na Rais Ruto.
“Msiridhike eti mmoja wenu ni Katibu, msiridhike kuwa baadhi yenu mmekuwa Mawaziri, wakati fulani nilikuwa waziri katika nchi hii, tulikuwa na Jaramogi kama Makamu wa Rais wa kwanza, hata Raila alikuwa Waziri Mkuu, msiridhike na hayo,” alisema gavana alipohutubia wakazi katika eneo lake la Ugenya wiki mbili zilizopita.