Michezo

Ahoya apigwa breki nusu-fainali ya J30 Nairobi

Na GEOFFREY ANENE May 17th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MCHEZAJI pekee wa Kenya aliyesalia katika kitengo cha wasichana cha mchezaji mmoja kila upande, Seline Ahoya, amebanduliwa katika nusu-fainali ya tenisi ya J30 Nairobi/Extreme Parklands Junior Circuit I baada ya kupoteza kwa mchezaji wa nafasi ya juu Janvi Asawa, 17, kutoka India kwa seti 6-3, 6-1 uwanjani Parklands Sports Club mnamo Ijumaa, Mei 16, 2025.

Asawa, ambaye anashikilia nafasi ya 771 kwenye viwango vya Kimataifa vya Shirikisho la Tenisi (ITF), alitathmini mchezo wake dhidi ya Ahoya (nambari 1,850 duniani).

“Nilicheza naye wiki mbili zilizopita nchini Rwanda, jambo ambalo lilinipa ujasiri kidogo kuingia kwenye mechi hii. Bila shaka, naye alikuwa amechambua mchezo wangu, jambo ambalo lilikuwa changamoto kidogo kwangu. Lakini nadhani nilicheza vizuri — nilianza kutawala mechi tangu mwanzo na nilikuwa nikipata pointi haraka,” alisema Asawa, akithibitisha kuwa alimshinda Seline kwa seti 6-2, 6-3 kwenye robo-fainali ya mashindano ya pili ya J30 Kigali mnamo Mei 1.

Alipokutana tena na Ahoya mjini Nairobi, Asawa, ambaye alishinda mashindano ya kwanza ya J30 Kigali mnamo Aprili 21, alikiri kuwa kulikuwa na presha ya kucheza dhidi ya mchezaji wa nyumbani.

“Ni nchi yake ya nyumbani, kwa hiyo nilihisi presha kidogo. Lakini niliimudu vizuri,” alisema.

Mmoja wa makocha wa Tennis Kenya, Tony Kipruto, anayefanya kazi na wachezaji chipukizi akiwemo Ahoya, alizungumzia mechi hiyo na mafunzo waliyopata.

“Mechi ilikuwa ngumu. Seline alikuwa anacheza dhidi ya mchezaji wa nafasi ya juu, na Janvi ni mchezaji mwenye akili ya kiufundi, thabiti sana, na hufanya makosa machache,” alisema Kipruto.

“Mkakati wetu ulikuwa ni kudumu kwenye ‘rally’ na kujaribu kumsukuma nyuma ya uwanja ili tupate nafasi ya kutawala pointi. Mara kadhaa tulifanikiwa, lakini Janvi alibadilisha mchezo wake haraka na kuwa mkali zaidi — hicho ndicho kilichompa faida,” alieleza Kipruto kabla ya kusifu Ahoya katika ‘serve’ zake ikilinganishwa na siku iliyotangulia.

“Leo tumefanya makosa ya kupiga neti ama mipira mirefu mara moja au mbili pekee, tofauti na jana ambapo tulikuwa na makosa kadhaa. Hata hivyo, tulikuwa na changamoto ya kutumia mipira mifupi vizuri. Seline alionekana kuwa na woga, huenda ni kutokana na ukosefu wa kujiamini. Kama tungefaidika na mipira hiyo mapema kwenye mechi, mambo yangekuwa tofauti.”

Kipruto pia alieleza kuhusu changamoto ya muda mdogo wa mazoezi.

“Seline yuko shule ya bweni, kwa hiyo hufanya mazoezi mara moja au mbili kwa wiki pekee. Wakati huo huo, mpinzani wake anacheza kila siku. Hiyo ni tofauti kubwa katika maandalizi,” alisema Kipruto ambaye humfundisha Ahoya mtaani Loresho, Nairobi.

Licha ya changamoto hiyo, timu sasa imeelekeza macho kwenye duru ya pili ya mashindano hayo itakayofanyika Mei 20-24 uwanjani humo, wakiwa na matumaini ya kufanya vyema zaidi.

Katika J30 Nairobi/Extreme Parklands Junior Circuit I, Wakenya wengine waliowakilishwa katika wasichana moja kwa moja ni Ashley Wafula, Jenerica Thuku, Michelle Murage, Inaaya Virani, Tumelo Kimunya, Daniella Muna na Nancy Kawira, lakini wote walitolewa katika raundi mbili za kwanza.

Katika upande wa wavulana, Kenya iliwakilishwa na Aum Chandarana, Reyan Bulsara, Ruhan Bhandari, Jeff Okuku, Ayush Bhandari na Mark Murage. Ni Ayush pekee aliyeingia raundi ya pili, ambako alipoteza kwa seti 6-4, 6-3 dhidi ya Mhindi Dhruveer Grover.

Mashindano haya yalivutia wachezaji kutoka Kenya, India, Ufaransa, Marekani, Uswizi, Ujerumani, Tunisia, Japani, China, Ireland, Uingereza, Hong Kong, Lithuania, Urusi, Denmark, Uhispania na Romania.