Karua: Serikali ya Kenya haikunitetea nikiwa nimezuiliwa Tanzania
KINARA wa PLP Martha Karua amewasili nchini baada ya kuzuiwa kuingia Tanzania.
Bi Karua ambaye aliwasili kwa ndege ya KQ kutoka Dar es Salaam asema alizuiliwa kwa saa sita katika uwanja wa ndege wa Julius Nyerere.
Amemtaka Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kufuata sheria huku pia akikashifu serikali ya Kenya kwa kutoingilia kati na kumnusuru na masaibu.
Bi Karua anasema kuna jaribio katika nchi za Afrika Mashariki kunyamazisha upinzani. Asema hatua ya serikali ya Kenya kukosa kuingilia kati inaweza kufasiriwa kwamba inaunga mkono kunyanyaswa alikopitia kwa kunyimwa uhuru wake akiwa nchi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Amefananisha kisa hicho na jinsi mwanasiasa wa upinzania nchini Uganda Kizza Besigye alinyakwa na kusafirishwa akiwa ziarani Kenya.