Walimu washangaa pesa za kusimamia mtihani kunyofolewa kutoka kwa bajeti yao
CHAMA cha Walimu Nchini (KNUT) kimeitaka Bunge la Kitaifa kurejesha Sh62 bilioni ambazo zimekatwa kwenye makadirio ya bajeti ya 2025/2026 kwa sekta ya elimu.
Katibu Mkuu wa KNUT Collins Oyuu jana aliwaongoza viongozi wa KNUT kutaka bunge liangazie upya suala hilo ili Wizara ya Elimu isikabiliwe na ukame wa fedha kwa miradi yake mbalimbali mwaka unaokuja wa kifedha.
“Elimu ndiyo msingi wa maendeleo nchini na wizara ya elimu inahitaji pesa kutimiza malengo yake kwa walimu. Tunarai bunge na serikali kuu ziangazie upya mgao wa sekta ya elimu,” akasema Bw Oyuu.
“Tunaangalia haki ambapo pesa za mitihani na walimu wanaosimamia mitihani imeondolewa kwenye makadirio ya bajeti. Hii haijawahi kufanyika na tuna matumaini bunge na serikali, zitarejesha pesa hizo kwenye bajeti,” akaongeza Bw Oyuu.
Alikuwa akiongea kijiji cha Olereko, Kilgoris Kaunti ya Narok Jumamosi wakati wa mazishi ya Mwenyekiti wa Baraza la KNUT ukanda wa Bonde la Ufa John Sampoti Musere.
Maraehemu aliaga baada ya kuugua kwa muda mrefu. Bw Oyuu alisema mageuzi katika sekta ya elimu hayawezi kuafikiwa bila ufadhili kwa sekta hiyo.
“Kungáa au kuporomoka kielimu kwa serikali hii kunategemea jinsi ambavyo serikali inachukulia elimu. Tuna matumaini Rais William Ruto ataingilia kati na kurejesha ufadhili huo,” akasema Bw Oyuu ambaye alikuwa ameandamana na viongozi wengine wa KNUT.
Katibu wa Elimu Profesa Julius Bitok aliambia kamati ya bunge kuhusu elimu inayoongozwa na Mbunge wa Tinderet Julius Meli, kwamba makato hayo kwa wizara yalifanywa na afisa wa Hazina Kuu ya Kifedha kutimiza makataa ya Baraza la Mawaziri.
Profesa Bitok alisema Sh12.5 bilioni za kusimamia mitihani ziliondolewa pamoja na Sh1.8 bilioni na Sh21.85 bilioni kwa elimu ya bure kwenye shule za msingi na upili, pia hazijawekwa kwenye makadirio ya serikali.
Katika makadirio hayo, Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC) imetengewa Sh387.7 milioni za kuwaajiri walimu 24,000 mnamo Januari mwakani.