Habari za Kitaifa

Serikali yatishia kumkamata Gachagua kwa uchochezi

Na WAANDISHI WETU May 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

UTAWALA wa Rais William Ruto umetishia kumtia mbaroni aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kwa kuchochea ghasia, hatua ambayo ikichuliwa itazidisha uhasama kati ya viongozi hao wawili waliofanya kazi pamoja na kutwaa uongozi wa nchi 2022.

Wikendi, Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki na Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen walimwonya Bw Gachagua, wakisema anapandisha joto la kisiasa kutimiza ajenda yake ya kisiasa kuelekea uchaguzi wa 2027.

Wawili hao walisema Bw Gachagua ambaye aliondolewa mamlakani na bunge mnamo Oktoba mwaka jana baada ya kuhudumu kama naibu rais kwa miaka miwili, hayuko juu ya sheria.

Serikali ilisisitiza kuwa haitasita kumnyaka Bw Gachagua iwapo ataendelea kuwa tishio kwa usalama wa nchi. Inasema kuwa Bw Gachagua sasa anatumia masaibu yake ya kibinafsi kisiasa kueneza fujo na taharuki kwa kisingizio kwamba anasaka umaarufu wa kisiasa.

Serikali imemjibu Bw Gachagua kutokana na matamshi yake kwamba Kenya huenda ikatumbukia katika ghasia za uchaguzi kama 2007 iwapo IEBC itatumika kuiba kura 2027.

“Wacha mwanaume huyo (Gachagua) aendelee kupiga kelele na kuwachochea Wakenya. Tutamkamata.  Siku ile alituambia kuwa akiondolewa basi kutakuwa na ghasia, kulikuwa na ghasia?” akasema

“Alipoona hakukuwa na ghasia, alienda nyumbani na kusema kuwa aliwatuliza watu. Tutamkamata,” akasema Bw Murkomen akiwa Iten Kaunti ya Elgeyo Marakwet.

Alirudia matamshi hayo akiwa Kaunti ya Trans Nzoia alisema Bw Gachagua hayuko juu ya sheria na serikali itawaandama viongozi ambao wanawachochea raia na kuiharibia serikali sifa.

“Wajue kwamba wataguswa. Tunamakinika kuhakikisha amani na usalama wa taifa wala hatutatishwa na yeyote akifikiria tutamwacha kwa sababu ya nafasi yake,” akaongeza Bw Murkomen kwenye mazishi Matisi Kitale mnamo Jumamosi.

“Wale wanaoeneza uoga kwa Wakenya watakabiliwa kwa sababu hawako juu ya sheria. Hukuna mtu atakayeruhusiwa kusema kile anachotaka na kutishia amani,” akasema.

Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki naye naye alimwonya Bw Gachagua akimkashifu kwa kuyatoa matamshi yanayoweza kuchoma nchi kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

Profesa Kindiki alisema serikali ya Rais William Ruto haitakubali Kenya irejee kwenye mkondo wa ghasia tena. Alifananisha kiongozi yeyote mwenye nia ya kuanzisha ghasia na kundi la kigaidi la Al Shabaab au majangili wanaowaua watu na kusababisha majeraha Kaskazini mwa Bonde la Ufa.

“Nchi yetu haiku katika hatari ya machafuko kabla na baada ya uchaguzi jinsi ilivyokuwa 2007. Wale ambao wanatabiri hilo ni maadui wa Wakenya na wanastahili kukataliwa kabisa,” akasema.

Profesa Kindiki alikuwa akiongea Amagoro eneobunge la Teso Kusini Kaunti ya Busia wakati wa ibada ya maombi akiwa ameandamana na viongozi kadhaa kutoka eneo hilo.

Bw Gachagua jana aliwajibu Profesa Kindiki na Bw Murkomen kuhusu vitisho kuwa atakamatwa. Badala yake aliwataka wawili hao washughulike na kukomesha utekaji nyara na mauaji ya kiholela.

“Sikuamrisha mtu yeyote ajihami na mwenyewe si mtu wa kueneza ghasia au fujo. Nilionya tu Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC) kwa siasa zetu zina uhasama mkali na hakuna nafasi yoyote ya udanganyifu kwenye kura ya 2027,” Bw Gachagua akasema Jumapili.

Ghasia za 2007 zilisababisha mauaji ya Wakenya zaidi ya 1000 huku wengine wengi wakihama makwao. Rais Ruto na mtangulizi wake Uhuru Kenyatta ni kati ya waliofikishwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kutokana na ghasia hizo lakini kesi zao zikaporomoka.

RIPOTI ZA MWANGI MUIRURI, SHABAN MAKOKHA, EVANS JAOLA NA TITUS OMINDE