Siaya yageuka uwanja wa fujo vita vya ubabe vikitishia kuvunja ‘bedroom’ ya Baba
KAUNTI ya Siaya sasa imekuwa kitovu cha uhasama wa kisiasa wakati ambapo kaunti nyinginezo za Luo Nyanza zinashuhudia utulivu hasa wakati huu ambapo ODM inashirikiana na serikali ya Kenya Kwanza.
Ubabe mkali wa kisiasa sasa ni kati ya Gavana James Orengo kwa upande moja na Seneta Dkt Oburu Oginga na Waziri wa Kawi Opiyo Wandayi kwa upande mwingine.
Huku Dkt Oginga na Bw Wandayi wakiunga mkono Serikali Jumuishi, Gavana Orengo amekuwa mkosoaji wa ushirikiano huo akitaka ODM irejelee maasi dhidi ya serikali.
Hata hivyo, imebainika kuwa uhasama huo una mizizi yake kutokana na kampeni za kusaka kiti cha ugavana 2017 na 2022.
Uhasama huo ulijitokeza wiki hii wakati ambapo madiwani walikataa kuandamana na Dkt Oginga na viongozi wengine kwenye mkutano na Rais William Ruto katika Ikulu ya Nairobi bila Bw Orengo.
Gavana huyo alikuwa nje ya nchi kwa shughuli za kikazi.
Hata hivyo, imebainika kwamba madiwani walikataa mwaliko huo ambao walifikiwa na Dkt Oginga kwa kisingizio kwa ulikuja kwa dharura na wengi wao hawakuwa wamejiandaa.
“Hatukukataa mwaliko, lakini tukakubali kuahirisha hadi wiki ijayo ili kuwe na nafasi ya kujiandaa kwa upande wetu,” akasema Kiongozi wa Wengi kwenye Bunge la Kaunti ya Siaya Edwin Otieno.
Baadhi ya madiwani ambao walizungumza na Taifa Leo walisema hawangeenda ikulu bila Bw Orengo ambaye walifichua alikuwa ameanza kupanga safari kama hiyo kabla ya ziara yake nje ya nchi.
Mkutano ambao ulikuwa uandaliwe ikulu pia ungehudhuriwa na wabunge wote wa kaunti hiyo ambayo pia ni nyumbani kwa Kinara wa Upinzani Raila Odinga.
Kwa mujibu wa Bw Wandayi, gavana huyo amegeuka kuwa adui wa maendeleo kutokana na msimamo wake wa kupinga Serikali Jumuishi.
Akiongea na waombolezaji katika kijiji cha Upande, Ugenya wakati wa kuzikwa kwa watu sita ambao waliteketea baada ya nyumba yao kuchomwa, Bw Wandayi aliyaelekeza maneno makali kwa Bw Orengo.
“Gavana wa Siaya lazima akomeshe uanaharakati na amakinikie utoaji wa huduma kwa watu waliomchagua. Wabunge na kwa kiasi fulani Senata ndio wanastahili kufanya ukosoaji ambao gavana amekesha akiufanya,” akasema Bw Wandayi.
“Ukilinganisha na kaunti nyingine, hapa Siaya ni aibu tupu. Hakuna dawa hospitalini na huduma hairidhishi. Kwa hivyo, gavana lazima amakinikie uwajibikaji badala ya siasa za uanaharakati,” akaongeza waziri huyo.
Dkt Oginga naye wakati wa ziara ya Rais Ruto katika Kaunti ya Migori alimtaka gavana ajiuzulu na aondoke ODM iwapo ataendelea kukosoa Serikali Jumuishi.
“Mbona anatutapikia kama yupo ndani? Afanye hivyo akiwa nje kwa sababu si nzuri aendelee na uanaharakati ikiwa yupo ndani ya ODM,” akasema Dkt Oginga.
Viongozi wa kijamii, raia na wale wa mashirika mbalimbali Siaya wanadai cheche kali kati ya viongozi kunalemaza maendeleo eneo hilo.
“Kaunti nyingine kama Migori na Homa Bay maendeleo inaendelea na kunufaikia Serikali Jumuishi lakini hapa viongozi wetu wanapigana,” akasema John Ogeya, Mwenyekitiwa Muungano wa Wanakandarasi Siaya.