Upinzani UG, TZ na Sudan Kusini unavyoumia, huku wa Kenya akijivinjari Ikulu
WAKATI ambapo Kenya inaendelea kushuhudia amani na ushirikiano kati ya upinzani na serikali, kwa majirani watatu katika ukanda wa Afrika Mashariki mambo yanaendelea kuteketea huku viongozi wa upinzani wakikabilia na mashtaka ya uhaini na kuzuiliwa.
Baada ya maandamano ya Gen Z mnamo Juni mwaka uliopita, Kinara wa ODM Raila Odinga alianzisha ushirikiano na Rais William Ruto ambaye alimshinda kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.
Kwa sasa wandani watano kutoka chama cha ODM wanahudumu ndani ya serikali ya Kenya Kwanza ambao walipinga hapo awali na hata kuikosoa vikali. Raila mwenyewe ana uhusiano wa kuridhisha na Rais Ruto.
Hata hivyo, kwa majirani Uganda, Tanzania na hata Sudan Kusini ambayo ina uhusiano wa kuridhisha wa kidplomasia, viongozi wa upinzani wanaendelea kuzuiliwa au kuwekwa hata chini ya kifungo cha nyumbani.
Kule Uganda, kiongozi wa upinzani Dkt Kizza Besigye kufikia leo atakuwa amekaa korokoroni kwa siku 178 baada ya kukamatwa Nairobi mnamo Novemba 20 mwaka jana jijini Nairobi.
Kenya ilikashifiwa vikali kwa kusaidiana na Uganda katika kukamatwa kwa Dkt Besigye, 69 ambaye ni kiongozi mkongwe na alikuwa mkosoaji mkubwa wa Rais Yoweri Museveni.
Dkt Besigye amekuwa mshindani mkali wa Rais Museveni katika chaguzi za Uganda na inakisiwa kuwa atawania urais tena mnamo Februari 2026 dhidi ya kiongozi huyo ambaye ametawala Uganda tangu 1986.
Mnamo Aprili 11, Mahakama Kuu ya Kampala ilikataa kumwaachilia Dkt Besigye na msaidizi wake Hajj Lutale kwa dhamana kwenye kesi ya uhaini ambayo inamkabili.
Kwa mujibu wa nakala ya mashtaka, Dkt Besigye na Lutala wanadaiwa walipanga kupindua serikali kati ya 2023 hadi Novemba 2024. Inadaiwa walipanga njama hiyo Geneva (Uswizi), Athens (Ugiriki), Nairobi (Kenya) na Kampala.
Jaji Rosette Kania alisema mashtaka ya uhaini dhidi ya Besigye ni mazito, yalifanyika maeneo mbalimbali Uganda na akiwaachiliwa, basi atavuruga mashahidi au kuhitilafiana na uchunguzi.
Kule Tanzania, hali si hali kwa Kiongozi wa Upinzani Tundu Lissu ambaye pia ameshtakiwa kwa uhaini ambayo hukumu yake ni kifo.
Lissu alishtakiwa kwa uhaini mnamo Aprili 10 baada ya kukamatwa kwenye mkutano wa kisiasa ambapo inadaiwa alitoa wito kwa raia wa Tanzania wasusie uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Kiongozi huyo wa Chadema aliingizwa kwa gari la polisi baada ya kumaliza kuhutubia mkutano wa umma Mbinga Kusini mwa Tanzania.
Jana Kiongozi wa PLP Martha Karua alizuiwa kuingia Tanzania kushiriki kesi ya Lissu leo. Chama chake cha Chadema nacho kimezuiwa kushiriki uchaguzi wa Oktoba baada ya kukataa kutii mwongozo wa uchaguzi.
Mnamo 2017, Lissu alinusurika mauti baada ya kupigwa risasi mara 16 ambapo alilazimika kuenda kupokea matibabu ngámbo.
Huku serikali ya Sudan Kusini ikikanusha habari za mauti ya Rais Salva Kiir, Makamu wa kwanza wa Rais wa Riek Machar naye amekuwa akitumikia kifungo cha nyumbani tangu Machi 27.
“Rais Kiir aliamrisha Dkt Riek Machar awekwe chini ya kifungo cha nyumbani,” akasema Msemaji wa Serikali Michael Makuei wakati huo.
Makuei alisema Machar alihusika na ghasia jijini Nasir, jimbo la Upper Nile ambako wanajeshi waaminifu kwake wanadaiwa kuvuruga amani ili kuhakikisha uchaguzi hauandaliwi na taifa hilo linarejea vitani.
Pia wanajeshi wake walidaiwa kumuua jenerali wa jeshi na watu wengine 10 baada ya kuvamia kambi ya jeshi la Nassir
Rais William Ruto kama mwenyekiti wa EAC mnamo Machi 29 alimtuma Bw Odinga Sudan Kusini lakini waziri huyo mkuu akazuiwa kumwona Machar huku akikutana tu na Rais Kiir.
Kando na Tanzania, Uganda na Sudan Kusini, mataifa mengine kama Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Rwanda yanaonekana kunyonga upinzani.
DRC, Rais Felix Tshisekedi na mtangulizi wake Joseph Kabila hawaonani uso kwa macho kutokana na ghasia ambazo zimekuwa zikishuhudiwa Mashariki mwa nchi hiyo.
Wapiganaji wa M23 ambao wanadaiwa kuungwa na Rwanda na pia Kabila, waliteka miji ya Goma na Bukavu Mashariki mwa DRC na juhudi za kupatikana kwa amani bado zinaendelea.
Rwanda nayo ni kama hakuna upinzani, Rais Kagame mara nyingi hushinda uchaguzi kwa zaidi ya asilimia 90 za kura.
“Hapa Kenya tuna nafasi ya demokrasia na Raila ambaye amekuwa sura ya upinzani ana karata kali ya kisiasa kutokana na ufuasi sugu na ana uungwaji mkono wa karibu nusu ya nchi. Kwa hivyo ni sawa na kuwa rais ndiposa yeyote anayeongoza hawezi kumtenga au kumwepuka,” akasema mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Javas Bigambo.