Habari

Kasisi aliyempokea Gachagua wiki mbili zilizopita apatikana ameuawa

Na WAIKWA MAINA May 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MAKACHERO kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) katika Kaunti ya Nakuru wameanzisha uchunguzi kuhusu kifo cha kasisi mmoja wa Kanisa Katoliki ambaye alimpokea na akawa mwenyeji wa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua wiki mbili zilizopita.

Mwili wa Kasisi John Maina ulipatikana Alhamisi Mei 15 katika eneo la Kikopey, eneobunge la Gilgil, kando mwa barabara kuu ya Nakuru-Nairobi.

Mwili huo ulipatikana mita 50 kutoka Kanisa la Kanisa Katoliki la Igwamiti, anakohudumu lililoko chini ya Dayosisi ya Nyahururu, kaunti ya Laikipia.

Wiki mbili zilizopita, kasisi Maina alikuwa mwenyeji wa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua katika Kanisa hilo.

Mkuu wa DCI eneo la Gilgil Rahamad Wasilwa aliambia Taifa Leo kwamba wameanzisha uchunguzi lakini wanasubiri ripoti ya upasuaji wa maiti ili kupata maelezo zaidi.

Afisa huyo alisema maafisa wake wanashuku kuwa huenda kasisi huyo aliuawa kwingine na mwili wake ukatupwa Kikopey.

“Huenda kasisi huyo wa Kanisa Katoliki aliuawa mahala pengine kisha mwili wake ukatupwa mahala hapo. Wapelelezi wameanzisha uchunguzi. Lakini ripoti ya upasuaji wa maiti ndiyo itatoa maelezo kamili yatakayotumiwa katika uchunguzi,” akasema afisa huyo.

Awali, mwili huo haungeweza kutambuliwa haraka hadi watu wa familia yake walipowasili na kuutambua.

Bw Wasilwa alisema mwili huo umepelekwa katika hifadhi ya Hospitali ya Kimisheni ya St Benedict kusubiri kufanyiwa upasuaji.

Maafisa wa polisi pia hawajapata gari la kasisi huyo linaloaminika kutumiwa na wauaji kusafirisha maiti hiyo na kuitupa karibu na barabara.

Wapelelezi pia wanachunguza maelezo kwenye simu yake kuwatambua watu ambao aliwasiliana nao kabla ya kuuawa kwake.

“Tunashirikiana na kampuni ya mawasiliano ya Safaricom kubaini yule ambaye kasisi huyo aliwasiliana naye kabla ya mwili wake kupatikana Kikopey. Aidha, watu waliotangamana naye kabla ya kuuawa kwake watachunguzwa. Hatimaye ripoti ya upasuaji itatoa kamili chanzo cha kifo chake,” Bw Wasilwa.