Habari za Kitaifa

Saa tano za ghasia na uharibifu Kitale polisi wakimtafuta Natembeya

Na TITUS OMINDE May 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

VIJANA wenye ghadhabu waliharibu magari manne ya maafisa ya Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) na Huduma za Kitaifa za Polisi NPS katika makazi ya Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya, Jumatatu.

Vijana hao waliharibu magari hayo walipokuwa wakizuia maafisa hao kupekuwa makazi ya Bw Natembeya mjini Kitale kwa madai ya ufisadi na matumizi mabaya ya mamlaka.

Vijana hao walishutumu maafisa wa EACC kwa kumwinda Gavana Natembeya kisiasa kwa kutumia tuhuma za ufisadi.

Wakiongozwa na mwakilishi wadi ya Hospital Erick Wafula, walipinga kukamatwa kwa Bw Natembeya wakitaja kama hatua ya kisiasa ya kumnyamazisha gavana huyo ambaye amekuwa mkosoaji mkuu wa serikali.

“Kama MCA hatujawahi kuona hoja yoyote inayohusu ufisadi kuhusiana na gavana Natembeya ikijadiliwa katika bunge letu la kaunti. Hii ni siasa inayolenga kumnyamazisha gavana wetu kama mtetezi wa raia,” akasema Bw Wafula.

Bw Wafula alionya kwamba hatua yoyote ya kuendelea kumzuilia Bw Natembeya itapingwa na wakazi wote wa Magharibi mwa Kenya ambao wameidhinisha Bw Natembeya kuwa kiongozi wao.

Akizungumza na wanahabari mjini Kitale, Bw Wafula alitaka serikali kuachana na Natembeya huku akionya kuwa kumkamata gavana huyo kutachochea maandamano zaidi mjini Kitale na Magharibi mwa Kenya kwa jumla.

“Tunaipa serikali saa tatu kuachana na Natembeya la sivyo tutafanya maandamano makubwa,” alisema Bw Wafula.

Hisia kama hizo zilitolewa na wafanyabiashara mjini Kitale wakiongozwa na Martin Waliaula ambaye alitaja hatua hiyo ya maafisa wa EACC kama iliyolenga kuwachokoza wakazi wa Trans Nzoia.

“Hivi si vita dhidi ya ufisadi bali ni vita vya kisiasa vinavyolenga kuwanyamazisha wapinzani wa serikali,” akasema Bw Waliaula.

Awali, kulishuhudiwa ghasia mjini Kitale pale wafuasi wa Bw Natembeya walipowasha moto barabarani wakiimba nyimbo za kukashifu utawala wa Rais William Ruto.

Ililazimu maafisa wa polisi wa kupambana na ghasia kutumia vitoa achozi ili kutawanya waandamanaji.

Kwa takriban saa tano kulishuhudiwa makabiliano kati ya polisi na waanadamanaji ambao walifunga barabara kuu ya Eldoret-Kitale.

Hatimaye hali ya utulivu ilirejelewa mjini humo huku waandamanaji wakiapa kurejelea maandamano baadaye iwapo gavana huyo ataendelea kuhangaishwa.