Wakuzaji miwa Kisumu wakaidi viongozi, wataka viwanda vikodishwe mara moja
BAADHI ya wakulima wa miwa kutoka Nyando, Kaunti ya Kisumu, wamewakashifu wanasiasa kutoka eneo hilo ambao wanapinga hatua ya serikali ya kitaifa ya kukodisha viwanda vya sukari kwa wawekezaji wa kibinafsi.
Viongozi wa eneo hilo wiki jana walikashifu serikali kwa kukodisha viwanda hivyo kwa wawekezaji wa kibinafsi wakihoji mpango huo hautasaidia kuvifufua, wakidai pia wakulima hawakushirikishwa.
Kabla ya kukodishwa kwa viwanda vya Chemelil na Muhoroni kwa wawekezaji wa kibinafsi, Gavana Anyang Nyong’o na baadhi ya wabunge wa Kaunti ya Kisumu waliandaa kikao na wanahabari na kupinga hatua hiyo.
Wabunge James Nyikal (Seme), Aduma Owuor (Nyakach), Joshua Oron (Kisumu Central), Shakeel Shabir (Kisumu Mashariki) na Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kisumu Ruth Odinga walipinga kukodishwa kwa viwanda vya Chemelil na Muhoroni wakisema hakukuwa na uwazi katika shughuli nzima.
Mbunge wa Muhoroni Onyango K’Oyoo alishutumu serikali kwa kuharakisha kutoa usimamizi wa viwanda vya Chemelil na Muhoroni kwa wawekezaji wa kibinafsi bila kuwahusisha washikadau.
“Tunawaumiza wasagaji miwa iwapo tunatoa usimamizi wa viwanda kwa kampuni ambazo hazina rekodi nzuri ya kuvisimamia. Ni viwanda hivi vimewasaidia wakazi wa eneo hili kiuchumi kwa miaka mingi,” akasema Bw K’Oyoo.
Hasa alipinga kukodishwa kwa kiwanda cha Chemelil kwa kile cha Kibos na Muhoroni kwa Kampuni ya Sukari ya West Valley.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Muungano wa Kitaifa wa Wakulima wa Miwa, Kilion Osur, amewalaumu viongozi hao kwa kukataa kutoa mwongozo kwa sekta hiyo kwa miaka mingi.
“Tunakaribisha hatua ya kukodishwa kwa viwanda hivi. Badala ya kuunga ufanisi, viongozi tuliowachagua wanapinga bila kutoa suluhu mbadala,” akasema Bw Osur.
Aliongeza kuwa wakulima sasa wameweka matumaini yao kwa viwanda vya kibinafsi kusaidia kuimarisha sekta ya sukari, kuongeza uzalishaji na kuwalipa wakulima kwa wakati.
“Kile ambacho wakulima wanahitaji ni kulipwa kwa wakati kwa miwa wanayowasilisha na Kibos inafanya hivyo,” akasema mkulima John Okita kutoka Sidho, Muhoroni.
Bw Okita alisema kuporomoka kwa viwanda vya sukari vya umma kama Miwani kumechangia umaskini na kulemaza maisha ya raia.
“Maisha hayajakuwa sawa tangu Miwani iporomoke na sasa tunaona mabadiliko kupitia Kibos,” akaongeza.
Francis Wangara, Katibu wa Muungano wa Wakulima na Wafanyakazi katika Sekta ya Kilimo cha Miwa (KUSPAW) aliwahakikishia wafanyakazi kuwa haki zao zitalindwa na hakuna atakayeachishwa kazi bila sheria kufuatwa.
Bw Wangara yupo kwenye kamati ya mpito ambayo itafanya kazi na wawekezaji wapya kwa kipindi cha miaka 12 kuhakikisha mchakato wote wa kisheria na utendakazi unafuatwa.
“Wakulima wamekuwa wakiumia kwa sababu hawalipwi. Kwa usimamizi huu mpya tunatarajia watalipwa vizuri,” akasema Bw Wangara.