Habari

Kikosi kikali, chenye usiri kilichovamia maboma ya Gachagua

Na KAMORE MAINA May 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MAAFISA kutoka Shirika la Kitaifa la Ujasusi (NIS) na Idara ya Upelelezi Nchini (DCI) walikuwa kwenye maboma ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, Taifa Leo imebaini.

Duru ziliarifu kuwa kikosi hicho kikali cha siri tena kikali cha usalama, kilitumika wakati wa maandamano ya Gen Z mnamo Juni mwaka jana.

Kikosi chenyewe kinajumuisha wanaume ambao wamepewa mafunzo ya juu na duru zinaarifu kilipanga kutwaa bunduki mikononi mwa wandani wa Bw Gachagua wakati walivamia maboma yake Jumapili.

Uvamizi huo ulitekelezwa Wamunyoro eneobunge la Mathira, Nyeri na mtaani Karen Nairobi.

Duru ziliarifu kuwa baadhi ya silaha ambazo zilitumiwa na walinzi wa Bw Gachagua Jumanne wakipambana na wahuni ni za hali ya juu na hazikufaa kuwa mikononi mwa raia.

Walinzi hao walipambana na wahuni waliovamia mkutano wa uzinduzi wa chama cha DCP mtaani Lavington Nairobi. Duru hizo ziliarifu polisi hao walitaka kutwaa silaha hizo kwenye maboma ya Bw Gachagua lakini wakabaini kuwa pamoja na walinzi hao, hawakuwa nyumbani Jumapili usiku.

Jana, Bw Gachagua alionekana kuthibitisha madai hayo akisema kulikuwa na lengo la kuvamiwa kwake na kitengo cha polisi ambacho kinajumuisha wale wanaotoka DCI, NIS, kile cha Kupambana na Fujo (GSU)  na Polisi wa Utawala (AP).

“Nikihudhuria ibada ya kanisa Gatanga nilipata ripoti za kijasusi kuwa kikosi cha mauaji kutoka Tume ya Hudumu za Polisi kutoka NIS na ikiandamana na DCI na polisi wa kawaida, walitumwa,” akasema Bw Gachagua.

“Walizuia maeneo yote ya kutoka na walikuwa wamejihami huku wengine wakiwa wamejifunika nyuso licha ya kuwepo kwa mwongozo kuwa lazima wavae sare,” akaongeza.

Pia alitoa madai kuwa kulikuwa na mpango wa serikali kuondoa leseni ya kumiliki bunduki kwa baadhi ya walinzi wake wa kibinafsi kama sehemu ya kulemaza usalama wake.

“Hatukuwa na habari kuhusu operesheni hiyo,” akasema Msemaji wa Polisi Muchiri Nyaga kwenye mahojiano na Taifa Leo.

Jumapili usiku Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka kupitia mitandao ya kijamii alitangaza kuwa maboma ya Bw Gachagua yalikuwa yamevamiwa na kulikuwa na mpango wa kumkamata.

Mwaka jana, Taifa Leo iliripoti kuhusu kikosi kilichoundwa kufuatia mkutano wa kiusalama Nairobi, kusaka njia ya kupambana na Gen Z waliokuwa wakiandamana kupinga Mswada wa Fedha 2024.

Kikosi hicho kilianza kazi chini ya kachero wa zamani wa DCI ambaye kwa sasa yupo NIS. Pia katika katika kikosi hicho kulikuwa na kikosi cha operesheni kutoka makao makuu ya DCI wanaofanya kazi na maafisa wa NIS.

Pia katika kikosi hicho hicho kulikuwa na wataalamu wa teknolojia kutoka NIS ambao walikuwa wakifuatilia mitandaoni kuangalia machapisho ya watu maarufu waliokuwa wakikashifu serikali.

Baada ya kikosi hicho cha teknolojia kutambua mlengwa, walikuwa wakiwasilisha maelezo yake kwa kikosi  kikuu ili atekwe nyara.

Wanachama wa kikosi hicho wamekuwa wakiendeleza shughuli zao kwa njia ya siri katika makao makuu ya DCI.