Jinsi wakosoaji wa serikali ‘wanakapitia’
HATUA ya maafisa wa usalama kuvamia makazi ya Gavana wa Trans Nzoia, wengine kuzingira makazi ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na kukamatwa na Mbunge wa Mumias Mashariki Peter Salasya imeendeleza dhana kuwa serikali imetumia vyombo vya dola kuwaadhibu wapinzani wake.
Katika siku za hivi karibuni, viongozi wanaosawiriwa kuwa wakosoaji wa utawala wa Rais William Ruto wamelengwa na asasi za serikali kwa tuhuma za ufisadi na kutoa matamshi ya uchochezi.
Hali hii inafanana na enzi za rais mstaafu Uhuru Kenyatta ambapo wakosoaji wa utawala wake na wandani wa Dkt Ruto, aliyekuwa naibu wake, walikamatwa kwa tuhuma za hizo hizo za ufisadi ya uchochezi wa chuki.
Kukamatwa kwa wanasiasa hao kulishika kasi zaidi baada ya Bw Kenyatta kutofautiana kisiasa na Dkt Ruto baada ya handisheki yake na kiongozi wa ODM Raila Odinga mnamo Machi 9, 2018.
Kando na Bw Gachagua, Bw Natembeya na Bw Salasya, mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi pia anamulikwa na asasi za serikali.
Hii ni baada ya kampuni moja ambako anamiliki hisa, Kencont Container Freight Station (CFS) iliyoko Mombasa kuvamiwa na polisi walioandamana na maafisa wa Shirika la Reli Nchini kwa tuhuma kwamba kampuni hiyo inamiliki ardhi kinyume cha sheria.
Mnamo jana, Bw Salasya alifikishwa katika Mahakama ya Milimani, Nairobi, ambapo alisomewa mashtaka ya kutoa matamshi ya uchochezi.
Mahakama ilimwachilia huru kwa dhamana ya Sh500,000 au dhamana ya pesa taslimu ya Sh200,000.
Mbunge huyo aliyekamatwa mwishoni mwa wiki iliyopita alituhumiwa kuchochea chuki na uhasama wa kikabila kupitia jumbe alizoweka kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X mnamo Mei 10.
Kupitia mawakili wake, Mbunge huyo alilalamikia jinsi alikamatwa, akidai magurudumu ya gari lake yalitobolewa kwa kupigwa risasi na maafisa waliomkamatwa na wakadinda kujitambulisha.
Mahakama iliambiwa kuwa Bw Salasya alipelekwa kusikojulikana kabla ya kusafirishwa hadi Nairobi na kuzuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Central.
Visa vingine vya viongozi kuvamiwa na kukamatwa vilitokea siku chache baada ya wanasiasa hao kutishwa na watu wanaohudumu serikalini, au wanasiasa wandani wa Rais Ruto.
Hatua hii inaafiki madai ya viongozi wa upinzani kwamba Kenya Kwanza imeamua kutumia asasi za usalama kuwatisha wakosoaji wake.
Kwa mfani mnamo Jumapili, Waziri wa Usalama Kipchumba Murkomen akiwa Kitale alionekana kumwonya Gavana Natembeya akimtaka kumheshimu Rais.
Bw Murkomen alimtaka Gavana huyo kukomesha mtindo wake wa kisiasa wa kudunisha serikali na kumkosea heshima Dkt Ruto.
“Seneta Chesang ukikutana na gavana Natembeya mwambie aonyeshe tabia za mtu ambaye amewahi kuhudumu katika afisi kubwa serikalini. Akome kutoa matamshi kiholela,” Waziri huyo akasema.
“Nimebaini kuwa mienendo ya baada ya viongozi hao ni mibaya kiasi kwamba wao huandamana na magenge ya wahalifu wanapohudhuria mazishi na hafla zingine za kijamii. Hii ni makosa na sharti tuikomeshe kwa sababu tunataka siasa za kistaarabu,” Bw Murkomen akasema katika Kanisa la Nuru AIC mjini Kitale.
Mwishoni mwa wiki jana Bw Murkomen na Naibu Rais Kithure Kindiki pia walimtisha Bw Gachagua kwamba angekamatwa.
“Mtu asijaribu kupiga kelele akiwatisha Wakenya. Tutamkamata. Wakati ule alituambia kuwa akiondolewa mamlaka fujo zitatokea nchini; je, kulikuwa na fujo? La. Alipogundua kuwa hakukuwa na fujo alienda nyumbani na kujifanya kama anayewatuliza watu. Tutamkamata,” Bw Murkomen akasema kwa lugha ya Kalenjin katika hafla moja mjini Iten Jumamosi.
Baadaye alirudia tishio hilo kwa lugha ya Kiingereza.
Bw Gachagua alikuwa ameonya kuwa ghasia mbaya zaidi zitatokea nchi kuliko zile zilizoshuhudiwa baada ya uchaguzi wa 2007 pale matokeo ya uchaguzi wa urais yalipobishaniwa.
Bw Gachagua alionya kuwa hali kama hiyo itashuhudiwa nchini ikiwa makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ambao uteuzi wao haujaidhinishwa na bunge watasimamia vibaya uchaguzi mkuu wa 2027.
Mnamo Jumapili usiku, wandani wa Gachagua walidai kuwa maafisa wa polisi walivamia makazi yake katika mtaa wa Karen, Nairobi na Wamunyoro, Nyeri.
-Imetafsiriwa na Charles Wasonga