TAHARIRI: Taasisi zetu zisitumike kwa maslahi ya kisiasa
KATIKA siku za hivi majuzi, Kenya imeshuhudia mtindo wa kutatanisha wa taasisi za serikali kutumiwa kama silaha na zana za kuwahangaisha viongozi wa kisiasa wanaoonekana kupinga serikali.
Japo hatushabikii ufisadi uliokithiri nchini wala uchochezi unaoendekezwa na wanasiasa, kukamatwa au kuhangaishwa kwa baadhi ya wanasiasa wa upinzani nchini kunachora picha ya matumizi mabaya ya asasi za umma.
Hatua ya Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kumsaka Gavana George Natembeya wa Trans Nzoia kama mhalifu sugu inadhihirisha uwezekano wa matumizi hayo mabaya ya taasisi za serikali.
Ingawa tume ya EACC ina jukumu kuu la kupambana na ufisadi, walengwa wake mara kadhaa wamekuwa wa kutiliwa shaka.
Mbali na Gavana Natembeya, hatua zilizochukuliwa dhidi ya aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua, na uvamizi kisha kufungwa kwa kampuni ya Gideon Moi jijini Mombasa ni ukumbusho tosha wa hali inayotatiza: kutumiwa kwa mashirika ya serikali kama silaha katika kuwalenga viongozi wa upinzani.
Vitendo hivi vinajisawiri kama sehemu ya mkakati mpana wa kukandamiza upinzani na kuwatisha wapinzani wa kisiasa.
Mbinu kama hizi hudhoofisha misingi ya demokrasia yetu.
Katiba ya Kenya inahakikisha haki ya ushiriki wa kisiasa na uhuru wa kujieleza.
Taasisi za serikali zinaposhirikishwa kukandamiza haki hizi, imani ya umma kwa utawala na taasisi hizo hufifia.
Jumuiya ya kimataifa kwa muda mrefu imetambua umuhimu wa taasisi imara na huru katika kulinda michakato ya kidemokrasia.
Ahadi ya Kenya kudumisha kanuni hizi sasa inatiliwa shaka baada ya hatua hizi ambazo huenda zina manufaa kwa umma ila kwa namna fulani zinaonekana kuwa na dosari.
Iwapo mwelekeo wa sasa utaendelea, tuna hatari ya kurudi kwenye enzi ambapo upinzani wa kisiasa ulikabiliwa na ukandamizaji badala ya mazungumzo na maafikiano.
Ni muhimu serikali ikomeshe matumizi ya asasi hizi za serikali kuwalenga wapinzani wa kisiasa.
Badala yake, inapaswa kuzingatia kukuza mazingira ambapo sauti mbalimbali za kisiasa zinaweza kusikika na taasisi hizi muhimu kufanya kazi bila woga au upendeleo wowote.
Hapo ndipo Kenya itakapoweza kudumisha kikweli maadili ya kidemokrasia yaliyowekwa katika katiba yake.
Wakati wa kuchukua hatua ni sasa. Kwa ajili ya demokrasia yetu, silaha za vyombo vya dola lazima ziishe.