Urafiki ulivyozalisha kampuni ya uuzaji ‘mitishamba’ ng’ambo
ADHUHURI moja, Brian Selelo na Cherotich Nzau, ambao ni waanzilishi wa Aromatic Fresh Kenya Limited walikutana kujuliana hali baada ya kukaa kwa muda mrefu bila kuonana.
Walikuwa marafiki wa dhati, na Cherotich alikuwa amesafiri ng’ambo kwa minajili ya kazi. Hata ingawa walikuwa wakiongea kwa njia ya simu, hawakuwa wameonana kwa muda wa miaka miwili. Walipokutana adhuhuri hiyo kwa maakuli ya mchana, kwenye mazungumzo wazo la kilimo liliwajia.
Wawili hao walijadili kilimo, hivyo basi wazo hilo liliegemea shughuli za zaraa. “Mwasisi mwenzangu, alikuwa amejaribu kushiriki kilimo Nanyuki japo hakikufanikiwa kwa sababu alikiendeleza kwa njia ya siku. Alilazimika kutia kikomo kwa muda,” Selelo anasema. Alikuwa akilima mitishamba.

Mkutano wao ukawa jukwaa la kubadilishana mawazo; chaguo bora la kilimo. Mahesabu yaliyokokotolewa yalikuwa aidha wakuze pilipili mboga (capsicums), pili pili hoho (zile kali) au walime mitishamba inayoteka masoko ng’ambo.
Hatimaye, mitishamba iliibuka kidedea baada ya kutathmini faida na hasara zake. Faida zilikuwa kibao, kwa mujibu wa maelezo ya Selelo. “Nilikuwa nimefanya utafiti wa miaka kadhaa. Shukran kwa mwanzilishi mwenza wa kilimobiashara ambaye pia alikuwa amewahi kukuza mitishamba,” anaelezea.
Mwaka 2020, janga la Covid-19 lilipotua nchini, waliingilia kilimo cha mitishamba. Selelo kwenye mahojiano, alidokeza kwamba walileta pamoja akiba zao na kukodi ekari 10 kilomita chache kutoka Kitengela, Kaunti ya Kajiado. “Tulichanga mtaji wa Sh5 milioni,” akafichua. Selelo, ambaye alikuwa katika utumishi wa umma, mapema 2023 anasema kuwa aliacha kazi na kujituma kikamilifu kwenye zaraa.

Cherotich, naye majuzi alijiunga naye – akaacha gange aliyokuwa akifanya majuu. Wote sasa wameelekeza nguvu zao kwenye kilimobiashara cha mitishamba inayoteka soko moto ng’ambo. Miaka mitano baadaye, urafiki wao wa dhati umepelekea kuanzisha kampuni ya kukuza mitishamba.
Aromatic Fresh Kenya Limited, inakuza mitishamba inayouzwa ng’ambo. Kutoka waasisi wawili, sasa wamekuwa jumla ya watatu; wakijumuisha wanandoa wao. Eneo la Enkasiti, kwenye barabara ya Kitengela–Namanga, unapozuru shamba la kampuni hiyo ni lenye shughuli tele.
Unapotua, unakaribishwa na mpangilio maridadi wa vivungulio (greenhouses) ambavyo vinatumika kulima mitishamba ndani kwa ndani. Mitishamba mingine, pia, inalimwa nje.
Wakati wa mavuno, wafanyakazi huwa kwenye pilkapilka za hapa na pale kuhakikisha wanawahi wakati. “Mitishamba inapoanza kuvunwa, ina muda ili isiharibike,” Cherotich anasema.
Shamba la Aromatic Fresh Kenya likiwa na jumla ya ekari 10, vivungulio vimekalia ekari nne. Walianza na vivungulio viwili virusi vya corona vilipokuwa vikitesa Kenya na ulimwengu, na sasa wana jumla ya 56 (greenhouse tunnels).

Vinatumika kuzalish aina tano ya mitishamba, ambayo ni: basil—mtishamba wanayouza kwa wingi ughaibuni, tarragon, oregano, marjoram, na sage.Nayo inayokuzwa eneo tambarare ni; thyme, rosemary, sorrel, lemon balm, lovage, na flat parsley, mimea ambayo huvunwa miaka miwili mfululizo.
Ya vivungulio huvunwa miezi miwili pekee, kisha inang’olewa. “Tumepanga huduma zetu kuhakikisha tuna mazao kila wakati,” Cherotich anaelezea. Ikizingatiwa kuwa Kajiado inaorodheshwa kati ya maeneo kame na nusu-kame nchini (ASAL), kampuni hiyo imekumbatia mfumo wa unyunyiziaji mimea na mashamba maji kwa mifereji.
Wakati wa kiangazi na ukame, hutegemea kisima ambacho maji hupampiwa kwa kutumia nguvu za kawi yaani sola ya jua. “Vilevile, tumekumbatia teknolojia ya mifereji kupulizia mimea dawa dhidi ya wadudu na magonjwa,” Selelo anasema.
Kutambua ikiwa mitishamba wanayokuza ni tayari kuvunwa, hukagua rangi ya majani; yawe ya kijani, nayo matawi yawe dhabiti. Aromatic Fresh Kenya Ltd kwa sasa ina masoko mawili.

“Tunauza Uingereza (UK) kupitia shirika la kuuza mimea inayochukua muda mfupi kukomaa (horticulture) ng’ambo, na soko lingine ni letu la moja kwa moja Netherlands,” Selelo anadokeza.
Kila wiki, huvuna tani mbili za basil. Mitishamba inayolimwa nje – eneo tambarare, kwa jumla huvuna kilo 500, kila wiki.
Kiwastani, Selelo anaambia Akilimali kwamba kilo moja hununuliwa Sh300. Kuwahi soko la ng’ambo, wazalishaji wa mitishamba sharti waafikie vigezo vya Kephis na Global G.A.P, shirika la kimataifa kutathmini ubora wa mimea ya muda mfupi kukomaa inayouzwa ughaibuni.
Vigezo hivyo vinashirikisha jinsi ya kukabiliana na wadudu, matumizi ya kemikali na eneo la ukuzaji. “Isitoshe, wateja wenyewe hufanya vipimo vya ghafla kwenye maabara kutathmini kiwango cha matumizi ya dawa dhidi ya wadudu, kuhakikisha vimeafikia sheria za muungano wa Bara Uropa (EU),” Cherotich anafafanua.
Mamlaka ya ukuzaji wa mimea inayochukua muda mfupi (HCD), ndiyo hutoa leseni kwa wanaouza mazao ng’ambo. Kutuatia mchango wao katika kilimo cha mitishamba, Aromatic Fresh Kenya mnamo Machi 2025, ilitambuliwa na Italian Trade Agency (ITA), shirika linalopiga jeki kampuni zinazohamasisha uhusiano bora kibiashara kati yao na Italia.
Walipata mafunzo ya kibiashara, katika hafla iliyoandaliwa na ITA kwa ushirikiano na HCD, baada ya kutuma maombi wakawa miongoni mwa kampuni 45 za kilimobiashara zilizoteuliwa.
Isitoshe, waliteuliwa kusafiri Italia Mei 2025 kuhudhuria Maonyesho ya mboga na matunda, maarufu kama Macfrut. Aromatic Fresh Kenya, ilianza na wafanyakazi tisa na sasa inajivunia kubuni nafasi za ajira kwa zaidi ya watu 50.
