Mbunge alivyolazimika kutoroka baada ya kugomewa na wafuasi wa Gachagua
MBUNGE wa Mathira, Bw Eric Wamumbi, Jumanne alilazimika kutoroka umati mjini Karatina katika eneobunge lake huku wasaidizi wake wawili wakijeruhiwa vibaya na wafuasi wa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Katika ghasia za siasa zinazoendelea kulaaniwa, shughuli za biashara zilisitishwa wafuasi wa Bw Gachagua walipolalamika na kuzua ghasia Bw Wamumbi alipojaribu kuhutubia baadhi ya wakazi, jambo lililomlazimu kutoroka.
Wakazi waliokuwa na hasira walielekeza ghadhabu zao kwa wasaidizi wawili wa Mbunge huyo waliojeruhiwa katika vurugu hizo.
Wamelazwa katika hospitali ya Karatina Level Four.
Inadaiwa kuwa mmoja wao aligombana na mwanamke ambaye ni mfuasi wa Bw Gachagua katika soko la Karatina.
Mwanaume huyo alilazimika kutafuta hifadhi katika kituo cha polisi cha Karatina huku wakazi waliokuwa na silaha butu wakitaka kumdhuru.
Wabunge wa eneo la Kati mwa Kenya waliopigia kura hoja ya kumuondoa Bw Gachagua, wamekuwa wakikumbana na upinzani mkali kutoka kwa wapiga kura wao wanaowalaumu kwa kumsaliti aliyekuwa naibu rais.
Bw Gachagua amewahimiza wananchi kutowachagua wabunge waliounga mkono kuondolewa kwake katika uchaguzi mkuu 2027.
Hali mjini Karatina ilikuwa tete jana huku wakazi wakifunga barabara kuu ya Karatina-Nairobi na polisi wakijaribu kuwatawanya.
Polisi wa kupambana na ghasia walikuwa bado wanashika doria mjini humo wakati wa kwenda mitamboni jana jioni.
Kamanda wa Polisi wa Mathira Mashariki, Bw Samson Leweri, alisema tukio hilo linachunguzwa huku maafisa wakijaribu kubaini chanzo cha vurugu hizo.
“Niko kwenye kikao cha dharura cha usalama na tutatoa taarifa kwa vyombo vya habari baadaye,” Bw Leweri aliambia Taifa Leo kwa simu.